MGOMBEA mwenza wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan amesononeshwa na tabia ya wananchi wa majimbo ya Mchinga na Liwale mkoani Lindi, kushindwa kuwapeleka watoto wao shuleni na kusababisha mkoa huo kukosa wataalamu.
Samia, alisema hayo kwa nyakati tofauti katika mikutano yake ya kampeni aliyoifanya jana.
Akiwa Mchinga, Samia alisema wakazi wake wanaipa kisogo elimu na kuipuuza, huku wakidai kujengewa shule za sekondari.
Aliwaambia wakazi hao kuwa hata, kitabu kitakatifu cha Quraan kimehimiza binaadamu kuthamini elimu kama vile mwenyezi Mungu alivyomhimiza Mtume Muhammad (SAW) juu ya umuhimu wa kusoma.
“Tunadai sekondari, lakini zinakosa wanafunzi, tunadai mabweni ya wasichana hayajai, mabweni yanakuwa makubwa kwa sababu wanafunzi hawajai katika madarasa, lazima watoto waende darasani, Mtume Muhammad aliamrishwa kusoma” alisema.
Alisema wataalamu wengi wakihamishiwa maeneo hayo wanakaa muda mfupi na kukataa kuendelea kuishi maeneo hayo.
“Mnalalamika hatuna wataalamu, kumbe hatupeleki watoto wetu shule, wataalamu wakija kutoka nje hawataki kukaa hapa,”alisema.
Aliwataka wananchi kukataa aina yoyote ya michango watakayotozwa shuleni bila kushirikisha kamati za wazazi.
Akizungumzia suala la afya ya uzazi, Samia aliahidi kusimamia akina mama wajawazito wanaojifungua ili kuepuka vifo visivyokuwa vya lazima.