26.1 C
Dar es Salaam
Friday, January 3, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Mahiga: Pengine balozi wa EU amepangiwa majukumu mengine

Na ELIYA MBONEA – ARUSHA


WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Balozi Dk. Augustine Mahiga, amesema Tanzania haijamfukuza Mwakilishi wa Umoja wa Ulaya (EU), Balozi Roeland van de Geer na pengine amepangiwa majukumu tofauti.

Juzi usiku kulisambaa taarifa katika mitandao ya kijamii kwamba balozi huyo aliitwa Ubelgiji kwenda kujadili masuala ya kisiasa yaliyotokea hapa nchini hivi karibuni na nyingine zilisema amefukuzwa na Serikali.

Akizungumza jijini hapa jana baada ya kufungua maadhimisho ya taasisi za Umoja wa Mataifa (UN), Mahiga alisema taarifa zilizosambaa katika mitandao ya kijamii kuwa Roeland amefukuzwa hazina ukweli wowote.

“Balozi huyu ameitwa Makao Makuu ya EU huko Brussels, Ubelgiji, tumeshauriana kuhusu kuitwa kwake na tumejulishwa kuwa ameitwa.

“Pengine waliomuita wana jukumu jingine au kazi nyingine wanataka kumpa, lakini ameitwa na ameondoka tayari nchini. Sisi tulijulishwa kuhusu hilo,” alisema.

Kuhusu maadhimisho hayo, alipongeza mashirika hayo ya UN na yale ya kikanda kwa kuweka makao makuu yao Arusha.

“Ni mwaka wa pili mashirika haya yanakutana eneo la Lakilaki yaliyobakia Mahakama ya Rwanda baada ya kufungwa shughuli zao. Ni ushirika mzuri kukutana na wananchi na wakazi wa Arusha.

“Mahakama hii iliyopo chini ya UN imebakiza sehemu inayohusiana na nyaraka za mahakama, hawa wamekaribisha wenzao wa UN na kwa ujumla wao wapo wanane ikiwamo na EAC,” alisema.

Pia alisema kufanyika kwa maadhimisho hayo kunakojumuisha kutembelewa na wakazi wa Arusha kunaonesha umoja wao kwa Serikali ya Tanzania.

Alisema ameyashawishi kuwa kile kinachofanyika hapo kwa maana ya uhifadhi wa nyaraka za mahakama kisijirudie tena.

“Kwa sasa tuna nyaraka zilizobakia, kwamba kosa la mauaji ya kimbari ni kosa kubwa, ni vyema wakati tukiadhimisha hapa tuhakikishe halijirudii.

“Katika historia ya dunia kosa hili liliwahi kutokea nyuma, na kwa bahati mbaya kabisa Afrika likatokea hapa jirani yetu Rwanda.

“Ni vyema tuendelee kukumbushana kwamba ustaarabu wa changamoto za kidunia ni kuhakikisha tunazuia mauaji ya kimbari au kuzuia maneno na vitendo vinavyoweza kusababisha chuki na mauaji ya kimbari.

“Baada ya kumaliza kazi zao bado wana jukumu la kuhifadhi nyaraka za kesi, ilitakiwa nyaraka hizi ziende Rwanda, lakini UN wakasema ziendeelee kubakia Tanzania,” alisema.

Aliwataka wafanyakazi wa UN kuanza kuwajengea uwezo wafanyakazi wa Kitanzania wanaofanya kazi humo.

“Kwamba kuwapo kwa mashirika ya UN isiwe kutengeneza ajira tu, bali wachukue jukumu la kufundisha na kuwajengea uwezo Watanzania ili waweze kufanya kazi hizo na kuyasaidia mashirika hayo,” alisema Mahiga.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles