BARCELONA, HISPANIA
HATIMAYE nahodha wa klabu ya Barcelona, Lionel Messi, amejiunga na kikosi cha timu hiyo kwa ajili ya kufanya mazoezi ya pamoja baada ya kuwa nje ya uwanja kwa wiki kadhaa kutokana na kuumia mkono.
Mchezaji huyo alipata tatizo hilo kwenye mchezo dhidi ya Sevilla, Oktoba 20 huku Barcelona wakishinda mabao 4-2. Mchezaji huyo anadaiwa kuwa, alivunjika mfupa, hivyo alikuwa nje ya uwanja na kukosa michezo miwili.
Kuumia kwake kuliwapa wasiwasi Barcelona, huku wakiamini anaweza kukaa nje ya uwanja kwa kipindi kirefu, lakini baada ya kuukosa mchezo wa Ligi ya Mabingwa dhidi ya Inter Milan pamoja na mchezo wa Ligi Kuu Hispania dhidi ya wapinzani wao Real Madrid huku Barcelona ikishinda mabao 5-1, mchezaji huyo kwa sasa anaonekana kuwa fiti.
Hata hivyo, Kocha wa timu hiyo, Ernesto Valverde, ameweka wazi kuwa, ataangalia hali ya mchezaji huyo ili aone kama anaweza kupata nafasi ya kucheza katika mchezo wa Ligi dhidi ya Rayo Vallecano, kesho au Jumanne wiki ijayo ambapo Barcelona watakwenda kukutana na Inter Milan kwenye Ligi ya Mabingwa.