YERUSALEM, ISRAEL
WANASAYANSI nchini hapa wanaamini wanakaribia kupata tiba ya kutokomeza virusi vya Ukimwi (VVU).
Imani hiyo imekuja baada ya timu ya watafiti kumaliza jaribio la kimaabara mwilini mwa binadamu, ambalo wanasema limetoa matokeo mazuri ya kushangaza.
Watafiti hao walitangaza jana kuwa katika hatua ya kwanza ya jaribio, dawa ijulikanayo kama Gammora ilitokomeza asilimia 99 ya virusi ndani ya wiki nne za matibabu.
Kampuni ya tiba ya Zion ya Israel imeshirikiana na Chuo Kikuu cha Hebrew cha Yerusalem na kampuni ya Sirion Biotech ya Ujerumani katika majaribio hayo.
Matokeo hayo ya kufurahisha yalionesha kuwa dawa iliua seli zilizoambukizwa VVU katika mwili wa mwanadamu bila kuathiri seli zenye afya.
Awamu hii ni ya kwanza ya majaribio, iliyotumia kiwango kidogo cha washiriki kwa kuanzia, ilitoa matumaini makubwa ya uwezekano wa tiba ya VVU, ambavyo viliibuka mara ya kwanza miaka 35 iliyopita.
“Matokeo ya kwanza ya kimaabara yalikuwa kinyume na matarajio yetu na yanatoa matumaini ya kupata tiba ya maradhi haya,” alisema Dk. Esmira Naftali, mkuu wa maendeleo wa Kampuni ya Zion.
Virusi hivyo hatari ambavyo kwa kiasi kikubwa husambazwa kwa njia ya kukutana kimwili, huambukiza seli za mfumo wa kinga ziitwazo ‘seli T’.
Julai na Agosti mwaka huu, wagonjwa tisa katika Hospitali ya Kumbukumbu ya Ronald Bata nchini Uganda walipewa dozi za Gammora kwa wiki kati ya nne hadi tano.
“Sehemu kubwa ya wagonjwa walionesha kupunguza kwa mzigo wa virusi hadi kwa asilimia 90 wakati wa kipindi cha wiki nne za kwanza,” alisema Dk. Naftali.
Katika sehemu ya pili ya majaribio iliyofanyika wiki mbili baadaye, wagonjwa walipatiwa tiba ya ziada ya ARV kwa wiki nyingine nne hadi tano.
Matokeo yalionesha kwamba muunganiko wa tiba ulitokomeza hadi asilima 99 ya virusi katika wagonjwa hao katika wiki nne.
Wagonjwa walioshiriki katika majaribio hawakukumbwa na dalili za athari zozote zinazotokana na utumiaji huo wa dawa.
Wakati wa jumla ya wiki 10 za utafiti, wagonjwa wa makundi yote mawili walionesha ongezeko la idadi ya seli T, ambazo ni muhimu katika utendaji wa mfumo wa kinga.
“Kutokana na ukomo wa utafiti huu, tunafurahi kuwa tuko tayari kuthibitisha ufanisi wa dawa yetu katika awamu ya pili itakayoshirikisha idadi kubwa ya washiriki na kudumu kwa kipindi kirefu,” alisema Dk. Naftali.
Hata hivyo, wakati matokeo ya Gammora yakitia moyo, inaweza kuchukua miaka mingi kabla ya dawa hiyo kuwa tayari sokoni.
Majaribio na mapitio zaidi yanahitajika kabla ya tiba mpya kuthibitishwa rasmi kwa matumizi.