24.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, May 31, 2023

Contact us: [email protected]

Mbio za kumrithi Merkel zapamba moto

BERLIN, UJERUMANI

WATU watatu wametangaza nia ya kugombea wadhifa wa mwenyekiti wa chama cha kihafidhina cha Christian Democratic Union (CDU) baada ya Kansela Angela Merkel kutangaza kutogombea.

Mkutano Mkuu wa mwaka wa CDU ambao pamoja na mambo mengine utamchagua kiongozi wa chama hicho, unatarajia kufanyika mjini Hamburg mapema mwezi ujao.

Watu hao ni Katibu Mkuu wa sasa wa chama hicho, Annegret Kramp-Karrenbauer.

Mama huyo mwenye umri wa miaka 56 anapewa nafasi kubwa katika kinyang’anyiro cha kuiwania nafasi hiyo.

Karrenbauer aliyepewa jina la utani la Merkel mdogo kwenye vyombo vya habari, ni mshirika wa ndani wa Kansela Merkel.

Pamoja na sifa nyingine, Karrenbauer aliwahi kuwa waziri mkuu wa jimbo dogo la Saarland la magharibi mwa Ujerumani. Anawakilisha siasa za mrengo wa kati.

Mwanasiasa mwingine anayepewa nafasi nzuri ya kurithi kiti cha mwenyekiti wa chama ni Friedrich Merz (62) ambaye miaka ya nyuma alikuwa mshindani mkubwa wa Kansela Merkel.

Merz ndiye aliyekuwa wa kwanza kutangaza nia ya kuwa mwenyekiti wa CDU mara tu baada ya Kansela Merkel kutangaza hatawania tena wadhifa huo.

Alisema mwanzo mpya unahitajika katika kambi ya wahafidhina chini ya viongozi vijana na wenye uzoefu.

Merz alisema yuko tayari kuchukua wajibu wa uenyekiti na kwamba atafanya kila linalopasa ili kuimarisha mshikamano ndani ya CDU.

Mtu mwingine anayepewa nafasi ya kuchukua wadhifa huo baada ya Merkel kuondoka ni waziri wa afya wa sasa, Jens Spahn mwenye umri wa miaka 38.

Kijana huyo anayetambulika kuwa mkosoaji mkali wa Angela Merkel hakuficha nia yake ya kumrithi.

Spahn ameshajaribu kuwahamasisha miongoni mwa wahafidhina ndani ya CDU wamuunge mkono kwa kuukosoa msimamo wa wastani wa Angela Merkel juu ya wakimbizi, akitaka kuwepo msimamo mkali juu ya suala la uhamiaji.

Wengine wanaoelezwa kuwa na nia ya kutangaza ni pamoja na Waziri Mkuu wa Jimbo la North Rhine Westphalia, Armin Laschet ambaye ni mshirika wa ndani wa Merkel.

Laschet anatarajiwa kutangaza mwishoni mwa wiki hii iwapo atajitosa katika kinyang’anyiro hicho.

Pia mwanasiasa mkongwe mwenye tajiriba kubwa ya kisiasa, Wolfgang Schauble ataweza kujiliwaza ikiwa atachaguliwa kuwa mwenyekiti wa CDU mwezi ujao.

Schauble mwenye umri wa miaka 76 aliwahi kushika nyadhifa mbalimbali serikalini ikiwamo kuwa waziri wa fedha kabla ya kuchaguliwa kuwa Spika wa Bunge la Ujerumani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
213,208FollowersFollow
567,000SubscribersSubscribe

Latest Articles