29.2 C
Dar es Salaam
Saturday, November 16, 2024

Contact us: [email protected]

Mfanyabiashara Kortini kwa mashtaka 75

Na KULWA MZEE-DAR ES SALAAM



MFANYABIASHARA Akram Azizi (75), amefikishwa mahakamani akikabiliwa na mashtaka 75 ya uhujumu uchumi ikiwamo ya kukutwa na nyara za Serikali, silaha 70, risasi 6,496 na kutakatisha Dola za Marekani 9,018.

Mshtakiwa huyo anayedaiwa kutenda makosa hayo juzi na jana, alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam mbele ya Hakimu Mkazi Augustino Rwizile.

Wakili wa Serikali Mkuu, Paul Kadushi alidai mshtakiwa alitenda makosa hayo kati ya Juni na Oktoba 30 na 31 mwaka huu maeneo ya Oysterbay, Dar es Salaam.

Akisoma mashtaka, Kadushi alidai mshtakiwa katika shtaka la kwanza anadaiwa Oktoba 30, mwaka huu maeneo ya Oysterbay alikutwa na meno ya tembo sita yenye thamani ya Sh 103,095,000.

Katika shtaka la pili anadaiwa Oktoba 30, mwaka huu alikutwa na nyama ya nyati kilo 65 zenye thamani ya Dola za Marekani 1,900 bila kuwa na kibali.

Kadushi alidai shtaka la tatu hadi la 72 mshtakiwa anadaiwa kukutwa na silaha mbalimbali aina ya rifle, pistol na shotgun bila kuwa na kibali cha mrajisi wa silaha.

Akisoma shtaka la 73, Wakili wa Serikali Mkuu, Faraja Nchimbi, alidai Oktoba 30, mwaka huu mshtakiwa alikutwa na risasi 4,092 na shtaka la 74 alikutwa na risasi 2,404 Oktoba 31 mwaka huu bila kuwa na kibali.

Faraja alidai shtaka la 75, mshtakiwa anashtakiwa kwa kutakatisha fedha Dola za Marekani 9,018 huku akijua ni zao la kosa tangulizi la biashara haramu ya nyara za Serikali na kukutwa na silaha bila kibali.

Baada ya kusomewa mashtaka hayo, mshtakiwa hakutakiwa kujibu lolote kwa sababu mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo.

Wakili Kadushi aliieleza mahakama kuwa upelelezi kwa baadhi ya mashtaka umekamilika na mashtaka mengine haujakamilika.

Mahakama iliahirisha kesi huyo hadi Novemba 12, mwaka huu kwa kutajwa ili kujua kama upelelezi utakuwa umekamilika ama la.

Wakili wa mshtakiwa, Augustine Shio alidai: “Mashtaka kama yanavyoonekana, makosa yanadaiwa kufanyika jana (juzi) na leo (jana) na mteja wetu kafikishwa mahakamani.

“Mteja anadaiwa kukutwa na silaha na risasi bila kibali, hivyo ni jukumu la Jamhuri kuja kuthibitisha kama mteja wetu hana vibali.

“Mteja wetu hakatai kwamba vitu hivyo vilikutwa nyumbani kwake na ofisini, kazi ya Serikali ni kuthibitisha kama havina vibali.”

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles