25.3 C
Dar es Salaam
Friday, January 3, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Uhuru awaza namna atakavyokumbukwa

NA ISIJI DOMINIC



MOJA ya swali ambalo Rais Uhuru Kenyatta hakutarajia kukutana nalo kutoka kwa mwanafunzi wa kidato cha tatu, Joyce Nyawira, limeacha gumzo huku wachambuzi wa siasa wakihoji nafasi ya wabunge kumbana Rais.

Akizindua rasmi shule iliyojengwa na Taasisi ya M-Pesa yenye thamani ya Shilingi bilioni tatu za Kenya (takribani Shilingi trilioni 6.8) ambayo sasa inatambulika kama M-Pesa Foundation Academy iliyopo Thika, Rais Uhuru alimshtukiza mwanafunzi huyo na kumtaka amuulize swali.

Kwa kujiamini, Nyawira alimuuliza Rais anataka akumbukwe vipi muda wake madarakani ukifika kikomo 2022. Ni swali ambalo liliwaacha wageni mashuhuri, walimu, wazazi na wanafunzi wenzake vinywa wazi.

“Natumaini mambo mengi lakini kikubwa ni kuacha taifa lililoungana na jamii inayoshirikiana, na pia kushinda vita dhidi ya ufisadi,” alijibu Rais Uhuru ambaye alioneshwa kufurahishwa na ujasiri wa Nyawira kuuliza swali hilo.

Ni swali ambalo wachambuzi wa siasa wanahoji nini wanachofanya wabunge ambao wapo katika nafasi nzuri ya kutunga sheria na kumbana Rais Uhuru kutimiza ahadi alizozitoa wakati wa kampeni na alipoapishwa kuhudumu muhula wa pili.

Swali aliloulizwa Rais Uhuru na mwanafunzi wa kidato cha tatu limekuja mwaka moja baada ya Kenya kupiga kura ya marudio, Oktoba 26, 2017, kufuatia Mahakama ya Juu kufuta matokeo ya uchaguzi Mkuu uliofanyika Agosti 8 mwaka jana.

Rais Uhuru amebakisha miaka minne na huku akionekana kujitahidi kutimiza ajenda nne kuu (Big 4 Agenda) ambayo anaamini itasaidia kuthibiti ufisadi na kuunganisha Kenya, viongozi wengine wateule wamekuwa wakipiga siasa.

Wabunge, magavana, maseneta, wawakilishi wa wanawake na wajumbe wa kaunti wanawaza uchaguzi mkuu ujao na mijadala yao imejikita zaidi kwenye siasa na miungano mipya badala ya kuwatumikia wananchi ambao wanalalamika gharama za maisha kupanda.

Katika kuunganisha Wakenya, Rais Uhuru amefanikiwa hususani baada ya tukio la Machi 9, mwaka huu alipojitokeza hadharani na kinara wa upinzani, Raila Odinga na wote kwa pamoja kuhutubia taifa.

Tangu wawili hao kukutana na kuahidi kufanya kazi pamoja, siasa kali iliyokuwa ikishuhudiwa kati ya chama cha Jubilee na Muungano wa NASA zimefifia. Hata bungeni, kiongozi wa walio wengi na yule wa wachache wamekuwa wakiongea lugha moja na haikushangaza walivyoshawishi wabunge kupitisha pendekezo la rais ya nyongeza ya ushuru wa bidhaa zote zitokanazo na mafuta kwa asilimia nane.

Rais Uhuru kwa nyakati tofauti siku za hivi karibuni alikutana pia na kiongozi wa Chama cha Wiper, Kalonzo Musyoka, pamoja na wanachama wake ikiwamo pia viongozi kutoka Mkoa wa Magharibi ambao wengi wao wanatoka Chama cha Ford Kenya, lengo likiwa ni kuhubiri amani na kusisitiza jamii mbalimbali kushirikiana.

Mtihani aliyonayo Rais Uhuru ambayo akifanikiwa atazidi kukumbukwa ni vita dhidi ya ufisadi. Hili ni donda sugu na Rais amekabidhi rungu kwa Mkurugenzi wa Mashtaka ya Jinai (DPP) na Mkurugenzi wa Idara ya Upelelezi (DCI) kumchunguza, kumkamata na kumfikisha mtu yeyote hata mwenye cheo kikubwa serikalini endapo watajiridhisha amejihusisha na ufisadi.

Tumeshuhudia magavana, wabunge, waliokuwa mawaziri na watumishi wengine serikalini wakilala rumande na baadaye kufikishwa mahakamani na hata wakati mwingine kunyimwa dhamana. Ila kinachosubiriwa zaidi na Wakenya ni kuona kesi zao zinazohusu ufisadi zikifika tamati na watuhumiwa wakipatikana na hatia wafungwe huku mali walizotafuna kurudishwa ili zifanikishe miradi ya serikali.

Rais Uhuru anataka mawaziri wake kuwajibika ipasavyo na mara mbili ndani ya wiki tatu alimuonya hadharani Waziri wa Kilimo, Mwangi Kiunjuri, kuhusu sakata la malipo ya wakulima wa mahindi.

Utendaji wa Kiunjuri ni mfano tu wa ghadhabu aliyonayo Rais Uhuru dhidi ya watendaji wake wanaoshindwa kutatua matatizo ya wananchi. Mapema mwezi huu, alikataa kusoma hotuba iliyoandaliwa akisema mawaziri na maofisa wengine serikalini wamemuangusha katika kurahisisha ufanyaji kazi kwa wajasiriamali wadogo na wa kati.

Kauli kama hizi za Rais na hasira anayoonesha waziwazi dhidi ya watendaji wake ni kielelezo tosha kuna uwezekano akalazimika kufanya mabadiliko katika baraza la mawaziri. Rais anayo mamlaka ya kuteua na kumfuta yeyote anayeona haendani na kasi yake na ili atekeleza ajenda nne kuu alizojiwekea, Rais anapaswa kufanya kazi na wale wanaomuelewa.

Rais Uhuru alipokuwa anawaapisha mawaziri aliwaambia, “Wakati wowote ukiona mzigo umekuwa mkubwa, sema na tutatafuta Mkenya mwingine mwenye uwezo kuchukua nafasi yako,”

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles