23.3 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Historia mpya yaandikwa Zanzibar

Na SARAH MOSSI – ALIYEKUWA ZANZIBAR



JUMANNE ya Oktoba 23 mwaka huu, Zanzibar iliingia kwenye historia mpya baada ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) na Kampuni ya Rakgas kusaini Mkataba wa mgawanyo wa Uzalishaji Mafuta na Gesi Asili katika kitalu cha Pemba.

Mkataba huo wa aina yake ni mwanzo wa wa miradi mingi ya Mafuta na Gesi Asilia inayotarajiwa kuja yenye lengo la kuimarisha uchumi wa Zanzibar na watu wake.

Oktoba 23, mwaka huu ni siku ambayo inaungana na siku nyingine chache kwenye orodha ya siku muhimu katika kumbukumbu za Zanzibar. Hiyo ni safari ndefu ya kuweka misingi ya kuhakikisha kwamba rasilimali ya Zanzibar ni kwa ajili ya Wazanzibar na kwamba vizazi vilivyopo na vijavyo vitanufaika na manufaa ya rasilimali hiyo itakapopatikana.

Historia ya kazi ya utafutaji Mafuta na Gesi Asilia

Kazi hii ilianza katika miaka ya 50 ambapo kwa upande wa Zanzibar Kampuni za British Petroleum (BP) na Shell kwa pamoja zilifanya utafiti huo kwa kuchimba visima vya utafiti kadhaa katika visiwa vya Unguja na Pemba.

Utafiti huo ingawa haukukamilika na ulipomalizika katika miaka ya 1962/1963 ulitoa matokeo ya matumaini ya kuendelezwa kwa utafiti wa ziada baada ya kugundulika kuwapo kwa miamba ya mafuta na gesi asilia.

Harakati mpya za kuendeleza utafiti wa mafuta na gesi asilia zilianzishwa tena mwaka 2011, ambapo Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Serikali ya Ras al Khaimah walipoanzisha mazungumzo ya ushirikiano ukiwamo ushirikiano katika sekta ndogo ya mafuta na gesi asilia. Mazungumzo hayo yalikuwa chini ya usimamizi wa Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein.

Novemba 12, 2011 SMZ na Serikali ya Ras al Khaimah walisaini Hati ya Mashirikiano (MoU) kwa lengo la kufanya kazi kwa pamoja na kuleta ufanisi katika maendeleo ya Zanzibar.

Hati hiyo ya Mashirikiano ilikuwa na mambo tisa, moja kati ya hayo ilikuwa ni “Kuanzisha na kuingia katika makubaliano ya utafutaji wa mafuta na gesi asilia ndani ya eneo la mipaka ya Zanzibar”

Katika utekelezaji wa mashirikiano hayo, Serikali hizo ziliunda kamati maalumu ya utekelezaji wa Hati ya Mashirikiano yenye lengo la kusimamia utekelezaji wake huku vikao saba vya utekelezaji wa Hati ya Mashirikiano baina ya Serikali hizo vikifanyika kati ya Januari 31, 2012 na Agosti 22, 2016.

Kati ya mafanikio yaliyopatikana ni kuijengea uwezo sekta ya maji, afya na sekta ya elimu kwa uchimbaji wa visima vya maji na masomo (scholarships) kwa wananchi wa Zanzibar.

Mwaka 2015, Bunge la Jamhuri ya Tanzania lilirishia Sheria ya Mafuta Namba.21 ya mwaka 2015 ambayo imeipa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar mamlaka ya kushughulikia rasilimali za Mafuta na Gesi Asilia wenyewe.

Baada ya kupitishwa sheria hiyo, SMZ ikalazimika kuandaa haraka Sera ya Sheria ya Mafuta ili kusimamia sekta hiyo ambayo kiuhalisia ilikuwa ndiyo kwanza inaanza shughuli Zanzibar.

Sera hiyo iliandaliwa chini ya kikundi kazi maalumu na baada ya kurishiwa sera hiyo mwaka 2015 SMZ ililazimika kuandaa Sheria mbalimbali ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa sera hiyo.

Aidha mwaka 2016 ikaundwa kamati nyingine ya kuandaa Sheria ya Mafuta na Gesi Asilia ambayo ilisainiwa rasmi na Dk. Shein Novemba 15, 2016 na kuwa sheria kamili ya Mafuta na Gesi Asilia namba 6.

Baada ya kukamilika kwa utayarishaji wa Sera na Sheria, Serikali ikaunda kamati maalumu ya majadiliano iliyokuwa chini ya Mwanasheria Mkuu wa SMZ kwa lengo la kufanya majadiliano na Kampuni ya Rakgas kuhusu Mkataba wa Mgawanyo wa Uzalishaji wa Mafuta na Gesi Asilia (PSA) kwa Kitalu cha Pemba Zanzibar.

Ni safari iliyohusisha mijadala na mikutano mingi baina ya SMZ na ile ya Utawala wa Ras al Khaimah hadi kufikia maelewano na maridhiano yatakayonufaisha pande zote mbili kwenye utafutaji, uchimbaji na hatimaye ugawaji wa manufaa yatokanayo na rasilimali yenyewe.

Kati ya Machi 28,2017 na Julai 7,2018 jumla ya vikao vinane vya majadiliano baina ya SMZ na Kampuni ya Rakgas vilifanyika.

Kukamilika kwa kazi hiyo ndiyo matunda ya makataba uliosainiwa Oktoba 23, mwaka huu. Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imeonesha umakini mkubwa katika uteuzi na usimamizi wa kamati hizo. Kazi hiyo imethibitishwa na wataalamu kutoka taasisi mbambali za kimataifa zenye utaalamu na uzoefu wa masuala hayo.

Machi 18, 2017, SMZ ilianzisha Mamlaka ya Udhibiti wa Utafutaji na Uchimbaji wa Mafuta na Gesi Asilia Zanzibar, Zanzibar Petrolum, Regulatory Authority (ZPRA) na Juni 14, 2018 ilianzishwa Kampuni ya Maendeleo ya Mafuta na Gesi Asilia Zanzibar. Madhumuni ya taasisi hizo ni kusimamia na kudhibiti shughuli zote za Utafutaji, Uchimbaji, Uendelezaji na Uzalishaji wa rasilimali za Mafuta na Gesi Asilia pamoja na biashara ya bidhaa zinazotokana na uzalishaji kutoka shughuli hizo.

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba, Maji na Nishati Zanzibar, Al Khalil Mussa mkataba uliosainiwa umelezea utaratibu wa majukumu, haki, matumizi, mapato na mgawanyo wake baina ya pande mbili hizo.

SMZ imeamua kutumia mkataba wa PSA kwa sababu unaweza kutoa mfumo mzuri wa kimkataba unaoweza kudhibiti na kutoa uhakika zaidi wa kisheria kwa muda wote wa kufanya shughuli za Mafuta na Gesi Asilia.

Hata hivyo Al Khalil aliwakumbusha wananchi wa Zanzibar kwamba licha ya ishara zote njema za mkataba huo kazi ya uchimbaji wa mafuta na gesi asilia ni mchakato mrefu.

Kwamba anakumbusha kinyume na baadhi wanaodhani kwamba mkataba uliosainiwa ndiyo mwanzo wa kutiririka kwa mapato yatokanayo na rasilimali hizo, anakumbusha kwamba bado ipo safari ya kufikia huko.

Katibu Mkuu huyo alisisitiza kwamba hatua ya utiaji saini Mkataba wa Mgawanyo wa Uzaishaji wa Mafuta na Gesi Asilia umeipita katika hatua zote za kisheria na ni mkataba halali kwa pande zote mbili.

Kauli ya Rais Dk. Shein

Alisema katika hotuba aliyoitoa Novemba 15, 2016 siku ya utiaji saini Sheria ya Utafutaji na Uchimbaji wa Mafuta na Gesi Asilia, alieleza changamoto za kisheria zilizokuwapo awali pamoja na mipango ya kuiendeleza sekta hiyo.

Anaeleza juhudi zilizochukuliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzinar katika kuzitafutia ufumbuzi changamoto zilizokuwapo.

“Kwa kuwa Serikali zote mbili tunayo dhamira ya dhati ya kuliendeleza suala hili, tulilazimika kufanya marekebisho ya sheria muhimu na kutunga sheria mpya zilizo bora zaidi na madhubuti na zenye kuzingatia masilahi ya pande zote mbili za Muungano wetu.

“Nilishirikiana na Dk. Jakaya Kikwete, Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne kwa ajili ya kufikia na kuandaa njia bora itakayoziwezesha pande zote mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kusimamia rasilimali ya mafuta na gesi asilia kwa utaratibu mzuri wa kisheria, juhudi zilizochukuliwa na pande zote mbili, zilitufikisha pazuri katika kulitafutia ufumbuzi suala hili,”alisema.

Dk. Shein alisema mkataba uliosainiwa unahusisha Kitalu cha Pemba Zanzibar tu ambacho kinajumuisha maeneo yaliyopo nchi kavu na baharini.

Hata hivyo viko vitalu ambavyo havimo katika makubaliano yaliyosainiwa na kusisitiza huo ni mkataba wa mwanzo kwa upande wa Zanzibar na palipo majaaliwa mikataba mingine itafuata.

“Hata hivyo, bado ni mapema kuelezea faida zote zitakazopatikana iwapo tutafanikiwa katika suala hili, nawahimiza wananchi kuwa na subira, kwa kutambua suala la utafutaji mafuta na gesi asilia ni kazi inayochukua muda mrefu.

“Suala la utafutaji mafuta na gesi asilia ni jambo linalohusu maendeleo yetu na kamwe halitakiwi lituletee mfarakano katika jamii yetu, badala yake lituunganishe.

“Tujiepushe na watu wachache ambao wameamua kulitumia jambo hili kuwa ajenda ya kuwagawa watu, jambo ambalo ni kinyume na malengo ya Serikali ya kuzishughulikia rasilimali hizi, malengo ya Serikali ni kuhakikisha faida zitakazopatikana kutokana na rasilimali ya mafuta na gesi asilia zinachangia ukuaji wa uchumi wetu na zinawanufaisha wananchi wote bila kuwatenga na kuwabagua wengine,” alisema.

Kauli ya Shaikh Saud bin Saqr Al Qasimi, Mtawala wa Ras Al Khaimah

Akizungumza katika hafla ya utiaji saini, Shaikh Saud alisema wananchi wa Ras Al Khaimah wanawapenda wananchi wa Zanzibar na kila wanalolifanya wanaamini wanalifanya kama ndugu zao wa Zanzibar.

“Ras Al Khaimah tunao uhusiano maalumu kabisa na Zanzibar, mahusiano haya niliyahisi kila ninapokutana na Dk. Shein.

“Niliumia sana jinsi ninavyomuona Dk. Shein anavyoumia na kuwapenda watu wake wa Zanzibar na hivyo nikahisi lazima nije Zanzibar, tunaona fahari kubwa sana kuwa na mashirikiano ya kujenga maendeleo ya watu wa Zanzibar.

“Napenda kusisitiza sana sisi ni marafiki wazuri na tunawapenda Watanzania, hizi juhudi zinazoonekana ni za muda mfupi takribani mwaka mmoja lakini ni juhudi zitakazoleta manufa kwa muda mrefu lwa watu wa Zanzibar.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles