29.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

Mauaji ya Khashoggi yazigonganisha Saudia, Uturuki na Marekani

Na, OTHMAN MIRAJI, UJERUMANI



MAUAJI ya kikatili aliyofanyiwa mpinzani wa Serikali ya Saudi Arabia, Jamal Khashoggi, huko Istanbul, Uturuki, Oktoba 2, mwaka huu yamezusha mzozo mkubwa  wa kidiplomasia na yamezidisha kutoaminiwa duniani watawala wa Riyadh.

Hali kama hii haijwahi kutokea tangu yalipofanyika mashambulio ya Septemba 11, 2001 nchini Marekani ambayo yaliandaliwa na Osama bin Laden na kutekelezwa na Wasaudi 15 kati ya watekaji 19 wa ndege. Watu wengi duniani hawaondoi uwezekano kwamba mauaji ya Khashoggi ndani yake yana mkono wa Mwana na Mrithi wa ufalme Mohammed bin Salman wa Saudi Arabia, licha ya  wakuu wa nchi hiyo kuikanusha tuhuma hiyo. Cha kushangaza zaidi ni kwamba kila pale watawala wa nchi hiyo wanapojaribu kujizongoa na tuhuma hiyo ndipo vyombo vya habari duniani vinawataka watoe majibu zaidi kuhusu maswali zaidi na zaidi yanayozuka kila siku  juu ya mkasa huo.

Kutoka miji mikubwa ya nchi za Magharibi kumetolewa matamshi makali dhidi ya Serikali ya Saudi Arabia, jambo ambalo si la kawaida, pale Riyadh yenyewe ilipokiri kwamba Khashoggi aliuliwa katika ubalozi wake mdogo mjini Istanbul.

Ilitajwa baadaye kwamba kifo hicho kilitokana na vurumai kubwa iliyojiri pale mwandishi huyo wa habari alipokuwa akihojiwa na makachero wa Kisaudi. Kuna ushahidi kwamba makachero hao waliwasili Istanbul kutokea Saudia siku moja kabla ya kutekelezwa mauaji hayo. Wasaudi walisema maiti ya Khashoggi ilizungushwa ndani ya zulia na kuteketezwa na mtu aliyeshiriki katika mauaji hayo na aliye mwenyeji wa Uturuki. Hapo kabla Wasaudi walidanganya, wakidai kwamba Khashoggi alikwenda katika ubalozi huo mdogo siku hiyo iliyotajwa, lakini baadaye alitoka na haijulikani alipokwenda.

Wakuu wa nchi mbalimbali duniani, kama vile Ufaransa, Uingereza na Canada, hawajaridhika na maelezo yaliyotolewa na Serikali ya Saudi Arabia. Walisema hayatoshi na walitaka kuweko uwazi zaidi kuhusu hali iliyozunguka kifo hicho pamoja na sababu zake. Pia walitaka watu waliohusika na mauaji hayo wachukuliwe hatua. Lakini wakuu wa Ujerumani walikwenda mbali zaidi wakitishia watasitisha kuiuzia silaha Saudi Arabia hadi pale suala la mauaji hayo limewekwa wazi.

Hapo kabla Rais Donald Trump wa Marekani aliyataja matamshi ya mwanzoni ya Saudi Arabia kukanusha kuhusika na mkasa huo kuwa ya kuaminika, lakini baadaye alibadilisha msimamo pale alipoliambia gazeti la Washington Post kwamba kuna uongo uliojificha katika usimulizi wa Serikali ya Riyadh.

Hata hivyo, alisisitiza kwamba nchi yake haitasitisha uhondo wa kuiuzia silaha Saudi Arabia, wala haitaacha kuwekeza katika nchi hiyo ya Kiarabu. Trump aliendelea kushikilia kwamba bado hakuna ushahidi kwamba Mohammed bin Salman anahusika moja kwa moja na mauaji hayo. Licha ya hayo, katika mabunge ya Marekani na Ulaya zilipazwa sauti kutaka Saudi Arabia iwekewe vikwazo vya silaha. Pia nchi na kampuni kadhaa za kimataifa ziliususia mkutano muhimu juu ya uwekezaji katika Saudi Arabia uliofanywa Riyadh.

Viongozi wa Saudi Arabia wamejaribu kujikwamua kutoka sokomoko hili. Mwanamfalme Mohammed ameamrisha vyombo vya usalama vya nchi yake vifanyiwe mabadiliko. Lakini wachunguzi wa mambo wana wasiwasi kama kweli baba yake aliye mzee, Mfalme Salman, anaitambua hatari iliyoko kuhusu mzozo huu. Na japokuwa wandani wawili wa Mohammed wamevuliwa nyadhifa zao kutokana na kisa hiki cha Istanbul, raia wengi wa Saudi Arabia bado wamo katika giza. Hawajui kwa kiasi gani Mohammed amehusika. Na jambo hilo halitajulikana kamwe kutokana na mfumo wa siri wa utawala wa kiimla ulivyo huko Saudi Arabia.

Si chini ya watu wanne kati ya 15 waliosafiri kwenda kumuua Khashoggi huko Istanbul walikuwa walinzi binafsi wa Mwanamfalme Mohammed. Walisafiri pia na daktari bingwa wa masuala ya uhalifu kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani. Kulikuweko ndani ya sanduku lake msumeno wa kukata mifupa. Pia polisi wa Uturuki waliwakamata wafanyakazi wawili na dereva wa ubalozi mdogo wa Saudi Arabia walio raia wa Uturuki.

Inasemekana mtu aliyetoa amri yafanyike yale yaliyotendwa ubalozini dhidi ya Khashoggi ni Maher Abdulaziz Mutrib, ambaye ana pasipoti ya kidiplomasia na ambaye aliwahi kufanya kazi na Khashoggi katika miaka ya zamani kwenye ubalozi wa Saudia mjini London. Mpelelezi wa Kituruki aligundua kwamba kuna chumba ndani ya ubalozi mdogo huo kilichopakwa rangi, yaonesha kuficha alama za damu baada ya kufanyika mauaji hayo. Kulipatikana pia sauti ya mazungumzo yaliyodumu dakika saba wakati Khashoggi anateswa, hasa pale alipokuwa ananyofolewa kucha zake za mikononi. Inatajwa kwamba baada ya kuteswa, aliuliwa kwa sindano ya sumu na kichwa chake kutengwa na mwili.

Rais Trump wa Marekani binafsi ana uhusiano wa kibiashara wa karibu sana na familia ya kifalme ya Saudi Arabia. Alikuwa hana njia nyingine isipokuwa kukiri kwamba kuna mipaka katika kuitetea familia ya kifalme ya Saudia. Serikali ya Washington imeshaanza kulegeza kamba kwa kutangaza kwamba kuna maafisa wa Kisaudi waliohusika na mkasa wa Istanbul ambao hawataruhusiwa kuingia Marekani, hawatapewa viza na kwamba kuna hatua nyingine zitakazofuata ambazo zitachukuliwa. Japokuwa yaonesha Washington haiko tayari katukatu kupoteza uhondo wa dola za Marekani bilioni 110 kwa biashara yake ya silaha na Saudi Arabia.

Serikali ya Uturuki, kutokana na upelelezi ilioufanya, haina shaka yeyote kwamba mauaji hayo ya kikatili yalikuwa ya kisiasa na hao makamando waliotumwa kutokea Saudi Arabia ndio waliofanya uhalifu huo, tena kutokana na amri za juu kabisa za Serikali ya Riyadh. Rais wa Uturuki, Teyyip Erdogan, ametaka watuhumiwa hao warejeshwe Uturuki ili wakabiliane na mkondo wa sheria; pia Saudi Arabia iseme uko wapi mwili wa Khashoggi. Haitarajiwi kwamba Wasaudi watayaridhia matakwa hayo.

Japokuwa Uturuki inadai kwamba ina ushahidi zaidi ambao utaiaibisha Saudi Arabia, haifikiriwi kwamba Uturuki itakwenda umbali mkubwa wa hata kuuharibu kabisa uhusiano wake na Saudi Arabia na pia rafiki wa nchi hiyo- Marekani- kwa sababu tu ya kadhia ya Khashoggi. Huenda Uturuki itaridhika na suluhu, kuona Mohammed Salman anang’atuka na tena asiwe mrithi wa mfalme- ili kuisafisha sura ya Saudi Arabia. Pia fedha zinaweza zikatumiwa. Yaweza Uturuki ikatulizwa kwa kuahidiwa uwekezaji mkubwa wa Saudi Arabia katika uchumi wa Uturuki ambao sasa uko taabani.

Jamal Khashoggi alikuwa mtu wa sura mbalimbali za kisiasa maishani mwake. Mwaka wa mwisho wa maisha yake yaliyodumu miaka 58 alikuwa mwandishi wa makala katika gazeti la Kimarekani la Washington Post akitetea umuhimu wa watu kuwa na uhuru wa kutoa maoni yao pamoja na watu wa Saudi Arabia, Misri na kwengineko kuweza kuarifiwa yanayojiri katika nchi zao. Msimamo wake uliwaudhi watawala wa Riyadh, japokuwa upinzani wake ulitiliwa maanani kwa vile alikuwa si mtu wa kawaida. Alikuwa na uzito na umaarufu huko Saudia na nje ya nchi hiyo.

Familia ya Khashoggi asili yake inatokea Uturuki, japokuwa kwa makarne imeishi Arabuni na kwa miaka mingi imekuwa na maingiliano na wafalme wa Saudi Arabia. Babu yake Jamal alikuwa daktari binafsi wa Mfalme Abdulaziz al-Saud, mfalme wa kwanza wa Saudi Arabia. Ami yake alikuwa maarufu kama dalali wa biashara ya silaha na alitajirika sana kwa kazi hiyo, japokuwa fedha zake nyingi aliziponda kwa kupenda sana maisha ya anasa.

Mjini Riyadh Jamal Khashoggi aliheshimiwa kama mwandishi habari mahiri. Aliwahi kuwa mhariri mkuu wa gazeti la al-Watan lililokuwa linaiunga mkono serikali. Alikuwa na mafungamno na mtu aliyekuwa mkuu wa usalama wa taifa, Mwanamfalme Turki al-Faisal na pia aliwahi kuwa mshauri wake alipokuwa balozi London na Washington.

Nyota ya Khashoggi ilipungua kung’ara tangu mwaka jana. Mrithi mpya wa mfalme, Mohammed bin Salman, hakustahamilia upinzani wa aina yeyote, hata ukiwa mdogo kiasi gani na hasa ule unaowekea alama ya kuuliza uhalali wa familia ya kifalme kuiongoza nchi hiyo. Khashoggi aliamua mwaka jana kukimbilia Marekani na kuanza kuliandikia gazeti la Washington Post. Makala zake zilichapishwa kupitia mtandao wa Internet na kusambazwa pia kwa lugha ya Kiarabu, hivyo kuwafikia watu wa Saudi Arabia, jambo lililoiudhi familia ya kifalme. Pia inasemekana watawala wa Riyadh walijaribu kumshawishi arejee nyumbani kwa kumuahidi kumpa kazi nzuri, lakini alikataa.

Kifo cha Khashoggi hakijamaliza mabishano kuhusu msimamo wake. Kuna wahakiki wanaodai kwamba yeye alikuwa akikitumikia chama cha Udugu wa Kiislamu ambacho kinatuhumiwa kuwa ni cha kigaidi huko Saudi Arabia na Misri. Kwa hakika, Khashoggi katika siku za mwisho alitaka kuweko mdahalo baina ya serikali za nchi za Kiarabu na Udugu wa Kiislamu, chama cha zamani kabisa katika Ulimwengu wa Kiislamu chenye siasa za Kiislamu.

Mtandao wa vyama vya Udugu wa Kiislamu uko katika nchi nyingi za Kiarabu na Kiislamu. Huko Uturuki chama tawala cha AKP cha Rais Teyyip Erdogan ni moja ya vyama  hivyo. Khashoggi alikuwa na marafiki wengi ndani ya chama hicho. Pia safari aliyoifanya Khashoggi siku yake ya mwisho katika ubalozi mdogo wa Saudia mjini Istanbul ilikuwa na madhumuni ya kupata karatasi za kuruhusiwa ili aweze kumuowa mchumba wake wa Kituruki, Hatice Cergiz.

Haioneshi kwamba Khashoggi alielemea katika siasa kali za Kiislamu, licha ya kutajwa kwamba alipokuwa ripota mnamo miaka ya thamanini aliandika juu ya Osama bin Laden na Wataliban wa Afghanistan. Huo ulikuwa wakati ambapo Osama bin Laden na pia wapiganaji wa Mujahidin wa Kitaliban walikuwa pia wanaungwa mkono na nchi za Magharibi dhidi ya wavamizi wa Kirusi.

Japokuwa nchi za Magharibi, hasa Marekani, zimeaibika kutokana na mauaji ya Khashoggi kufanywa na watawala wa nchi iliyo rafiki mkubwa wao na pia licha ya Saudi Arabia kugunduliwa namna ilivyo katili sana kwa wapinzani wa serikali yake, wachunguzi wa mambo, hata hivyo, wanaamini kwamba mkwaruzano uliochomoza sasa baina ya pande tatu- Saudia, Uturuki na Marekani ni wa muda tu. Hali itarejea kuwa ya kawaida baada ya muda. Pande zote hizo zinahitajiana. Hazitapoteza maslahi makubwa ya kibiashara, kisiasa na kijeshi baina yao kwa ajili ya tu mtu mmoja aliye na jina la Khashoggi.

Nchi za Magharibi zinaihitaji Saudi Arabia kama ufunguo wa kuweko utulivu katika Mashariki ya Kati. Nayo Saudi Arabia ina asilimia 20 ya hifadhi ya akiba ya mafuta duniani. Lakini kuna swali: utulivu gani huo ambao unazungumziwa? Mrithi wa Mfalme Mohammed ana ugomvi na Qatar, anaendesha vita vya kikatili huko Yemen ambako maelfu ya raia wasiokuwa na hatia wanakufa, aliwahi kumlazimisha waziri mkuu wa Lebanon ajiuzulu na sasa anatajwa kuwa na mkono wake katika kuuliwa mpinzani wa serikali yake. Je, nchi za Magharibi zitaendelea hadi lini kujificha nyuma ya  msamiati wa utulivu? Je,nchi za Magharibi zitaendelea hadi lini kuustahamilia ufalme wenye kuwakandamiza wanawake na wapinzani?

Mwanamfalme Mohammed bin Salman amefaulu hadi sasa kuwafanya Wamarekani na pia watu fulani barani Ulaya waamini kwamba Saudi Arabia ni tu chini ya uongozi wake itakayoweza kuwa mtoaji wa kuaminika wa mafuta na kubakia kuwa dhamana wa utulivu katika Mashariki ya Kati unaotakiwa na nchi za Magharibi. Pia kuwa usoni katika kupambana na kupanuka ushawishi wa Iran- hasimu mkubwa wa Marekani- katika eneo la Ghuba. Mwanamfalme Mohammed anatumia mabilioni ya dola kununua silaha za nchi za Magharibi, hivyo kulinda maelfu ya nafasi za kazi katika nchi hizo.

Muono wa Mwanamfalme Mohammed ni kuifungua nchi yake iwe na uchumi wa kiliberali. Hilo nalo si rahisi kutekelezeka. Shida kubwa ni kwamba nchi za Magharibi zinatafautiana na watawala wa Saudia pale wanapolitafsiri neno utulivu, japokuwa hadharani pande zote mbili zinadai zinaelewana juu ya tafsiri ya msamiati huo. Khashoggi alitaka kuifahamisha dunia juu ya ukweli ulivyo. Utawala katili wenye kuwanyima raia wake uhuru, wenye kuuwa waandishi wa habari na kudanganya mchana kweupe hupoteza heshima yake mbele ya macho ya jamii ya kimataifa.

Ni wakati sasa umewadia kwa nchi za Magharibi kuiangalia upya Mashariki ya Kati na zilipe tafsiri mpya neno utulivu. Kwani tafsiri zinazoitumia hadi sasa kuhusu neno hilo imekuwa ikidhuru zaidi kuliko kuboresha maslahi yao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles