24.4 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

Waliohama Chadema wateuliwa CCM

         Na ANDREW MSECHU Dar es Salaam

Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), imewateua waliojiuzulu uanachama wa Chadema na ubunge kwenye majimbo manne, kutetea nyadhifa zao kupitia chama hicho tawala katika uchaguzi mdogo unaotarajiwa kufanyika Desemba mwaka huu.

Taarifa iliyotolewa jana na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole baada ya Kikao cha Kamati Kuu Maalum ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, ilieleza kuwa kikao hicho kimeamua kuwateua wanachama hao wapya kuwa wagombea katika majimbo yao ya awali.

“Chama Cha Mapinduzi kinapenda kuujulisha umma wa wana CCM na Watanzania kwamba Kamati Kuu Maalum ya Halmashauri Kuu ya Taifa-NEC, imeketi leo (jana) jijini Dar es Salaam chini ya ndugu John Pombe Joseph Magufuli, Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Kikao cha Kamati Kuu Maalum pamoja na mambo mengine, kimefanya uteuzi wa wana CCM ambao watasimama katika uchaguzi mdogo wa ubunge kwa tiketi ya CCM,” alieleza Polepole katika taarifa yake.

Alisema katika uteuzi huo, Pauline Philipo Gekul ameteuliwa kuwania ubunge katika Jimbo la Babati Mjini, ambalo awali alikuwa mbunge wake kupitia Chadema hadi alipotangaza kujivua uanachama wa chama hicho na kujiunga CCM Oktoba 13 mwaka huu, hivyo nafasi hiyo kuwa wazi.

Mwingine ni James Kinyasi Millya ambaye ameteuliwa kuwania ubunge Jimbo la Simanjiro. Kabla ya uteuzi huo, Millya alikuwa mbunge wa jimbo hilo kupitia Chadema hadi alipotangaza kujivua uanachama Oktoba 7 mwaka huu.

Mwingine ni Joseph Michael Mkundi ambaye ameteuliwa kuwania ubunge katika Jimbo la Ukerewe. Mkundi alikuwa mbunge wa jimbo hilo kupitia Chadema hadi alipotangaza kujivua uanachama Oktoba 11 mwaka huu na kuhamia CCM.

Mwingine aliyeteuliwa ni Marwa Ryoba Chacha ambaye ameteuliwa kuwania ubunge katika Jimbo la Serengeti. Kabla ya uteuzi huo, Marwa alikuwa mbunge wa jimbo hilo kupitia Chadema hadi alipotangaza kujivua uanachama wa chama hicho Septemba 27 na kuhamia CCM.

Aidha, Polepole alisema Kamati Kuu imeelekeza kuwa Novemba 15 mwaka huu itakuwa mwisho wa kupokea maombi ya uanachama wa CCM ili kupewa dhamana ya uwakilishi kupitia tiketi ya CCM kwa wabunge na madiwani kutoka vyama vingine.

“Ieleweke kwamba baada ya tarehe hii wabunge na madiwani watakaoomba kujiunga na CCM watapokewa na kubaki kuwa wanachama wa kawaida na hawataruhusiwa kugombea ubunge au udiwani mpaka itakavyoamuliwa vinginevyo,” alieleza.

Polepole alieleza kuwa suala la uandikishwaji wa wanachama wapya linaendelea kwa mujibu wa taratibu za kawaida za chama sambamba na usajili wa wanachama na maandalizi ya utolewaji wa kadi za kielektroniki za chama.

Alisema Kamati Kuu pia imeelekeza viongozi wote wa CCM katika maeneo ambayo yanafanya uchaguzi mdogo kushiriki kikamilifu katika kuhamasisha wana CCM na wananchi kujitokeza kwa wingi na kufanikisha ushindi wa CCM.

Kamati Kuu hiyo imetangaza uteuzi wa wagombea hao huku chama kikuu cha upinzani nchini, Chadema na vyama vinavypunda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) vikiwa vimeshatoa msimamo wao kuwa havitashiriki katika uchaguzi mdogo unaoendelea kwa wakati huu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles