NA VERONICA ROMWALD, DAR ES SALAAM
VYANDARUA 5,823 kati ya 17,924 vyenye dawa vinavyomilikiwa na kaya nchini kwa ajili ya kujikinga dhidi ya mbu aenezaye ugonjwa wa malaria havitumiwi inavyopaswa, imebainika.
Hayo yamebainishwa katika ripoti ya Utafiti wa Viashiria vya Malaria wa mwaka 2017 iliyozinduliwa hivi karibuni na Waziri waAfya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, katika ukumbi wa Karimjee jijini hapa.
Ripoti hiyo inaeleza asilimia 38 ya vyandarua katika kaya ziishizo katika maeneo ya vijijini na asilimia 24 ya vyandarua katika kaya za mijini hazitumii ipasavyo vyandarua.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa ripoti hiyo, Mtakwimu Mwandamizi kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Cosmas Stephano alisema idadi hiyo ya vyandarua vinavyomilikiwa katika kaya lakini havitumiki ipasavyo ni sawa na asilimia 33.
Stephano alisema utafiti huo ulijumuisha jumla ya kaya 9,330 zilizochaguliwa kitaalamu Tanzania Bara naVisiwani.
Alisema matokeo ya utafiti huo yanaonesha kiwango cha umiliki wa chandarua chenye dawa kimepanda kutoka asilimia 66 mwaka 2015/16 hadi kufikia asilimia 78 mwaka 2017.
“Pamoja na kiwango cha umiliki kuongezeka changamoto inaonekana ipo katika upande wa matumizi sahihi ya vyandarua vyenyewe,” alisema.
Alisema matokeo yanaonesha zaidi ya nusu (asilimia 52) ya watu waliolala katika kaya usiku wa kuamkia siku ya utafiti ndiyo ambao walilala kwenye vyandarua.
Katika ukurasa wa 47 wa ripoti hiyo imeainisha sababu mbalimbali ambazo zilitajwa na kaya zilizohojiwa kuamkia siku ya utafiti kuwa ni pamoja na kuvihifadhi kwa ajili ya matumizi ya baadae, kutopendezwa na harufu yake na hali ya joto kwenye mazingira yao.
Matokeo hayo yanaeleza wana-kaya wengine walidai hawavitumii kwani hakuna malaria katika maeneo yao, uchakavu wa vyandarua vyao, vilikuwa vichafu, ni vidogo, hakuna mbu aenezaye malaria kwenye makazi yao, hofu na wengine walidai walikuwa wamevifua siku hiyo.