24.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 24, 2023

Contact us: [email protected]

Zitto aibua tuhuma nzito za mauaji

 


*Serikali yamjibu, yasubiri majibu ya IGP

Na ELIZABETH HOMBO, DAR ES SALAAM

INADAIWA zaidi ya wananchi 100 wa kabila la Wanyantuzu, wamepoteza maisha kwa kupigwa risasi na polisi katika Wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma.

Madai hayo yalitolewa jana Dar es Salaam na Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT-Wazalendo), wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu hali ya usalama nchini.

Alisema mauaji hayo yalitokea katika tukio la mapigano kati ya polisi  na wananchi wa jamii ya Wanyantuzu wilayani Uvinza mkoani Kigoma lililotokea takribani siku 10 zilizopita.

Zitto ambaye pia ni Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, alidai katika tukio hilo, askari wawili wanadaiwa kufariki dunia.

Alidai mapigano hayo, yalitokea baada ya kabila hilo la Wanyantuzu kupeleka mifugo yao katika eneo hilo.

Alipotafutwa Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi, Nsato Marijani ili kuzungumzia suala hilo alisema atafutwe Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma kwa kuwa tukio limetokea katika eneo lake.

Hata hivyo, MTANZANIA ilipomtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, Martin Ottieno simu yake iliita bila kupokelewa.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Brigedia Jenerali mstaafu, Emanuel Maganga naye alimtaka mwandishi wa habari hizi kumtafuta RPC wa Kigoma.

Kutokana na hilo, gazeti hili lilimtafuta Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola ambapo alisema taarifa hizo za wananchi 100 kupoteza maisha si za kweli.

“Mimi ni Waziri wa Mambo ya Ndani, sina taarifa za aina hiyo… haina ukweli wowote, nakiri  kulikuwa na operesheni ya mifugo kule na askari wetu wawili walipoteza maisha…natambua  IGP yuko kule tunasubiri atuletee taarifa.

“Lakini  madai wananchi wameuawa hakuna ukweli wowote…hata kuhusu suala la askari kuuawa sio rahisi kulizungumzia kwa sasa, ninamsubiri IGP aniletee taarifa kamili,”alisema Lugola.

ALICHOSEMA ZITTO

“Wiki iliyopita yalitokea mauaji ya askari wa Jeshi la Polisi katika eneo la Mto Malagarasi, Kijiji cha Mpeta wilayani Uvinza, mkoani Kigoma, ambapo Mkuu wa Kituo cha Polisi Nguruka aliuwawa na wanaodaiwa kuwa ni wananchi.

“Chama chetu kilitoa salamu za rambirambi kwa IGP (Simon Sirro) kutokana na mauaji hayo, kikilaani na kikitaka uchunguzi ufanyike na wahalifu wakamatwe na kufikishwa mahakamani.

“Tumekuwa tukifuatilia kwa kina yote yanayojiri huko Uvinza tangu kuuawa kwa askari polisi wetu. Tunasikitika kusema kuwa taarifa tunazozipata kutoka Uvinza zinaogofya mno.

“Kwani tunaambiwa wananchi zaidi ya 100 wa kabila la Wanyantuzu wamepoteza maisha kwa kupigwa risasi na polisi, wengine wakisemwa kuuawa hata wakiwa kwenye matibabu hospitalini baada ya kujeruhiwa kwenye purukushani na jeshi la polisi.

“Jeshi la Polisi limekalia kimya suala hili, pamoja na IGP kutembelea eneo hilo la maafa. Haiwezekani kamwe tukio kubwa namna hii kutokea halafu Serikali ibaki kimya bila kutoa maelezo yeyote kwa wananchi. Uchunguzi wa kina unapaswa kufanywa ili kutambua nini kimetokea pale Mgeta,”alisema Zitto.

Kutokana na hilo, alisema chama chao kinaendelea kukusanya majina na taarifa za wote wanaodaiwa kuuawa na kitaweka wazi taarifa husika.

“Kwa sasa tunaitaka Serikali ieleze nini hasa kimetokea Mgeta, maelezo hayo yawe ya kina na yawe ya ukweli. Chama chetu kinaendelea kukusanya majina na taarifa za wote wanaodaiwa kuuawa, na kitaweza wazi taarifa husika,”alisema Zitto.

Katika hatua nyingine, Zitto pia alizungumzia matukio ya watu kutekwa, kushambuliwa kwa risasi huku akishangazwa kwa wahalifu kutokamatwa mpaka sasa.

“Tanzania katika miaka mitatu, imekuwa ni nchi ya watu kutekwa, kushambuliwa kwa risasi na ‘watu wasiojulikana’, kuokotwa miili yao ikiwa imeuawa, kuwekwa kwenye viroba na kutupwa kwenye fukwe za bahari na mito yetu. Ni jambo la kawaida sasa mtu kutekwa au askari kufyatulia risasi makumi na mamia ya wananchi.

“Tunayo mifano iliyo wazi, msaidizi wa Kiongozi wa Upinzani, Ben Saanane, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya Kibondo na Diwani wa Kata ya Kagezi, Simon Kanguye na mwandishi wa habari za uchunguzi wa gazeti la Mwananchi, Azory Gwanda wamepotezwa, huku watuhumiwa namba moja wakiwa ni vyombo vya dola.

“Mpaka sasa hakuna yeyote aliyekamatwa kutokana na  tukio la kumpiga risasi nyingi kwa lengo la kumuua Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, pamoja na shambulizi kutokea ndani ya eneo la Bunge. Serikali inadhani kwa kuchagua kukaa kimya, damu ya watu hawa itapotea kimyakimya? Haiwezekani!

“Miaka hii mitatu tumeshuhudia mamia ya wananchi wenzetu wakiuawa na kupotezwa katika eneo la MKIRU (Mkuranga, Kibiti na Rufiji). Hivi karibuni Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Simon Siro, akizungumzia sakata la kutekwa kwa Mohammed Dewji alitoa dondoo kidogo kwamba walilazimika kutumia nguvu kule MKIRU kuwaondosha watu aliodai sasa wamekimbilia Msumbiji. Kwa mara ya kwanza IGP Sirro alikiri  kuna watu wengi waliuawa,”alisema Zitto.

Alisema chama chake cha ACT-Wazalendo kimepaza sauti juu ya masuala hayo ndani ya miaka mitatu, pamoja na Serikali kuamua kutokueleza ukweli au kuchukua hatua kuyazuia, hawatakaa kimya.

Alisema wataendelea kusisitiza kuundwa kwa tume ya kutafuta ukweli wa mauaji ya MKIRU na kupigania watu wote waliochukuliwa misikitini katika Wilaya za Kilwa na Lindi warejeshwe wakiwa hai ama ndugu na jamaa zao waelezwe kama wameuawa.

Pia alisema wataendelea kuhamasisha Watanzania kuendelea kushikamana kuwapigania Azory Gwanda, Simon Kanguye na Ben Saanane mpaka pale watakapopatikana au ukweli juu yao kujulikana.

Alisema ukweli wa mambo ni kuwa mfanyabiashara Mohammed Dewji (MO) asingepatikana bila nguvu ya umma,Watanzania wasingepaza sauti naye angepotezwa tu kama Saanane, Kanguye na Azory.

Aliwataka Watanzania waendeleza mshikamano huo kwa watu wengine ili kukomesha kabisa vitendo hivyo vya utekaji na watu kupotea.

“Tutaendelea kuitaka Idara ya Usalama wa Taifa (TISS) ijitathimini. Kwa muda mrefu tumepigania mageuzi ya kimfumo na ya kiuendeshaji ndani ya TISS. TISS si usalama wa CCM wala serikali. TISS ni usalama wa taifa.

“Yanapotea matukio makubwa yanayotishia usalama wa taifa letu, Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa anapaswa kuwajibika. TISS ikikaa kimya huku matukio yanayotishia usalama wa wananchi yakikita mizizi, hisia kwamba ‘watu wasiojulikana ni TISS’ zitapata uhalali. Wakati umefika kwa wazalendo ndani ya TISS kuamka na kurejesha hadhi ya chombo hicho.

“Tutaendelea kuyasema bungeni na katika kila mahali tutakapopata nafasi ya kupaza sauti yetu. Tutafanya hilo la kupaza sauti pamoja na kutambua unyeti wa usalama wa nchi yetu, lakini tukipinga njia ya kuua, kuteka, kupoteza na kutesa wananchi wenzetu kwa kigezo cha kulinda usalama wa nchi, ni njia inayowajaza hofu tu wananchi.

“Hofu ni ishara ya kukosa uhuru na bila uhuru watu hawawezi kusemwa kuwa wapo salama. Pia, bila uhuru hakuna maendeleo,”alisema Zitto

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
211,074FollowersFollow
563,000SubscribersSubscribe

Latest Articles