27.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

Watekaji wa Mo pasua kichwa, polisi kuwanasa?

Na ANDREW MSECHU


ZIMETIMIA siku 18 tangu kutekwa hadi kupatikana kwa mfanyabiashara maarufu nchini, Mohammed Dewji (Mo), na hadi sasa waliohusika hawajapatikana.

Kutopatikana kwa watekaji hao kumeendelea kuibua maswali mengi kutoka kwa wanajamii hasa baada ya Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP) Simon Sirro, kueleza kuwa ana uhakika na weledi wa jeshi lake na kwamba hakuna haja ya kuomba msaada wowote kutoka nje.

Taarifa za awali tangu siku alipotekwa, Oktoba 11, mwaka huu zilieleza kuwa waliohusika na utekaji huo ni raia wa kigeni wanaodhaniwa kuwa wazungu, suala ambalo liliwaduwaza wengi.

Tangu kuachiwa kwa Mo Dewji usiku wa kuamkia Oktoba 22, mwaka huu, hadi sasa hakuna taarifa yoyote zaidi kuhusu watuhumiwa waliokamatwa tofauti na watu wanane waliotajwa na Sirro katika mkutano wake wa Oktoba 21, mwaka huu.

Katika mkutano huo na wanahabari, Sirro amesema kati ya watuhumiwa 27 waliokuwa wamekamatwa tangu kutekwa kwa Mo, ni wanane tu waliokuwa wakiendelea kushikiliwa na Jeshi la Polisi akiwamo kapteni wa boti.

Katika mazungumzo yake na gazeti hili siku moja baada ya kupatikana kwa Mo, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa, alisema hata baada ya kupatikana kwake, operesheni ya kuwasaka watekaji haitakoma hadi watakapopatikana.

Kauli kama hiyo ilitolewa pia na Sirro alipozungumzia kupatikana kwa Mo, ikiwa ni siku moja tangu alipoitisha mkutano wake wa kwanza kuzungumzia suala hilo, akisema hata kama watekaji hao wamemwachia mfanyabiashara huyo, operesheni ya kuwakamata haitakoma hadi watakapopatikana.

Katika mkutano huo pamoja na kutaja gari Toyota Hilux Surf  iliyokuwa na namba za usajili AGX 404 MC, kwamba ndilo linalodaiwa kutumika kumteka Mo, pia alisema walifanikiwa kupata jina la dereva anayedaiwa kuwa aliingia na gari hilo nchini, Obasanjo Zakarias Junior.

Japokuwa Sirro hakutaka kutaja nchi inapotokea gari hiyo, ilibainika kwamba mfumo wa namba zake hutumia nchini Msumbiji kwa magari yanayosajiliwa katika mji mkuu wa nchi hiyo, Maputo.

Ubalozi wa Msumbiji nchini umesita kuzungumza iwapo wameombwa kutoa ushirikiano wa kumpata mmiliki au hata kusaidia kupatikana kwa taarifa zaidi kuhusu gari hilo, kwa maelezo kwamba hata wao wamesikia tu taarifa hizo katika vyombo vya habari.

Ofisa wa Ubalozi wa Msumbiji nchini, Maria Miceli alilieleza gazeti hili kuwa kwa sasa hawawezi kuzungumza lolote kuhusu suala hilo kwa kuwa hata wao wamesikia tu na kuona kupitia vyombo vya habari.

“Kuhusu aidha tumeombwa kutoa ushirikiano kuhusiana na suala hilo, kwa sasa hatuwezi kuzungumza lolote kwa kuwa hata sisi tumesikia tu na kuona kupitia vyombo vya habari,” amesema.

Ugumu wa kazi hiyo kwa polisi unaendelea kuibua maswali kadhaa ambayo hayana majibu kuhusu ni kina nani hasa waliomteka Mo.

Katika maelezo yake baada ya kuachiwa kwa Mo, Sirro anasema taarifa za awali kutoka kwa mfanyabiashara huyo ni kwamba watekaji hawakuwa Watanzania kwa kuwa baadhi yao walikuwa wakiongea lugha ya Kiingereza yenye lafudhi ya nchi za Kusini mwa Afrika na mwingine alikuwa akiongea Kiswahili kibovubovu.

Bado suala la ustadi uliotumiwa na watekaji hao katika Hoteli ya Colloseum ambalo limezungukwa na majengo mengi yenye ulinzi imara na kutoweka naye, kisha kumrejesha na kumtelekeza katika viwanja vya Gymkana, kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa awali na Kamanda Mambosasa unaendelea kuibua mijadala mizito vichwani mwa watu.

Watekaji hao walimwacha Mo katika eneo la Gymkhana na kutelekeza gari inayodaiwa kutumiwa kumteka. Eneo alipotupwa bilionea huyo ni takriban kilomita moja kutoka yalipo Makao Makuu ya Jeshi la Polisi na Ofisi Kuu za Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi za Dar es Salaam, kabla hazijahamia Dodoma.

Jinsi watekaji hao walivyomchukua na kumrejesha Mo, inaonesha walivyo na uzoefu wa uhalifu wa aina yake.

Ingawa Sirro ameapa kuwatia nguvuni wakiwa hai ama wamefariki, tayari leo zinatimia siku nane tangu Mo apatikane, huku watekaji hao wakiendelea kuvichenga vyombo vya usalama nchini.

 

Utajiri wa MO

Kwa mujibu wa jarida la masuala ya fedha la Forbes, Mo ndiye tajiri namba moja Afrika Mashariki, na tajiri mdogo zaidi Afrika akiwa na ukwasi wa Dola za Marekani bilioni 1.5, akiendesha biashara za viwanda vya kutengeneza nguo, biashara ya mazao, vyakula, vinywaji na sabuni. Pia anaendesha shughuli za uagizaji na usafirishaji bidhaa kutoka na kwenda nje, usagaji nafaka, nishati na petroli na utengenezaji baiskeli.

Kupitia Kampuni ya METL, amekuwa akiendesha shughuli zake Tanzania, Uganda, Sudan Kusini, Burundi, Rwanda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Kenya, Malawi, Msumbiji na Zambia. Ameajiri moja kwa moja watu zaidi ya 28,000 huku akitajwa kuchagia asilimia 3.5 ya jumla ya pato la taifa (GDP) la Tanzania.

Watanzania wengi walianza kumjua Mo mwishoni mwa miaka ya 90 na miaka ya mwanzoni ya 2000 alipojitokeza kuidhamini klabu kongwe ya mpira wa miguu ya Simba, lakini pia alipojitokeza kuwania ubunge wa Jimbo la Singida mjini kwa vipindi viwili, 2005/10 na 2010/15 kabla kutangaza kutogombea tena.

 

Maswali yanayoendelea kutopatikana watekaji

Kutokana na watekaji hao kutopatikana, masuala yanayohusu sababu za kutekwa kwake yanaendelea kuibua mjadala na kutopatikana kwao kunaweza kutoa majibu kuhusu sababu za kutekwa kwake na walichokuwa wamedhamiria watekaji hao.

Baadhi ya vyombo vya habari vya kimataifa vimekuwa vikinukuu vyanzo kutoka Jeshi la Polisi nchini kuwa yawezekana Mo ametekwa kwa sababu za kifedha, ikihisiwa watekaji watadai fedha ili wamwachie huru, suala ambalo katika hatua ya awali, IGP Sirro alilithibitisha alipozungumza na vyombo vya habari mara tu baada ya kupatikana kwa mfanyabiashara huyo.

Sirro alikaririwa na vyombo vya habari akisema bilionea Mo aliwapa nambari ya simu ya baba yake mzazi, Gulamhusein Dewji ili waongee naye juu ya hilo, lakini hawakupiga simu wakihofia kunaswa na polisi.

“Mohammed Dewji amesema watekaji hao walikuwa na wasiwasi sana… Walimwambia wanataka pesa, alipowauliza shilingi ngapi hawakusema. Aliwapa nambari ya simu ili waongee na baba yake, lakini waliogopa kwa sababu wanafahamu ulinzi wetu ni imara na tungewakamata,” alikaririwa IGP Siro baada ya kuachiwa kwa Mo.

Swali jingine ambalo linaendelea kuwa kitendawili hadi sasa ni kuhusu watu waliomteka, ikizingatiwa kuwa tajiri huyo hajawahi kuwa na rekodi ya kukwaruzana na watu kibiashara au kisiasa, akiwa hajawahi kuonesha wazi kuwa katika kundi lolote la kisiasa na akiwa mtu anayeonekana kuwa makini katika kauli zake kuhusu misimamo yake ya kisiasa kwa sasa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles