NA WINFRIDA MTOI
MWANARIADHA Augustino Sulle, amefanikiwa kuvunja rekodi ya taifa ya marathon, iliyokuwa inashikiliwa na mkongwe, Juma Ikangaa, baada ya juzi kukimbia akitumia saa 2:7:44 katika mbio za Toronto Marathon, nchini Canada.
Sulle alivunja rekodi hiyo ya kukimbia kilomita 42, akimpiku Ikangaa ambaye mwaka 1989 alikimbia mbio za marathon zilizofanyika nchini Marekani akitumia saa 2:8:1.
Katika mbio hizo za Toronto, Mkenya, Benson Kipruto, aliibuka kidedea akiwa mshindi baada ya kutumia saa 2:07:24, nafasi ya pili akishika Sulle, wakati nafasi ya tatu ilichukuliwa na Felix Kandie, pia wa Kenya, aliyetumia saa 2:08:30.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), Wilhelm Gidabuday, alisema ushindi huo ni mkubwa kitaifa licha ya kushika nafasi ya pili katika michuano hiyo ya Canada.
Gidabuday alisema kuanzia sasa Sulle anakuwa mwanariadha mwenye rekodi kubwa nchini hadi pale atakapotokea mwingine na kumpiku.
Alisema mwanariadha huyo anahitaji pongezi kwa sababu mashindano hayo ni makubwa, yanatambulika na Shirikisho la Kimataifa la Riadha (IAAF).
“Sulle anastahili sifa, amefanikiwa kushika nafasi ya pili katika mashindano makubwa na kuweka rekodi mpya kitaifa kwa kuwa mara ya mwisho ilipatikana miaka 29 iliyopita kupitia Juma Ikangaa, hivyo anastahili sifa,” alisema Gidabuday.
Alifafunua kuwa ushindi huo umepokelewa kwa furaha na shirikisho la mchezo huo, pia inawapa nguvu ya kuendelea kutengeneza wanariadha bora ili kuja kuvunja rekodi katika mashindano mbalimbali.
Alisema mwanariadha huyo anatarajia kuwasili nchini kesho, pia wanariadha wengine waliokuwa katika mashindano yaliyofanyika Japan juzi nao watawasili siku hiyo.
“Wapo wanariadha wengine wamepata medali nchini Japan, lakini mashindano yao hayakuwa makubwa na hayatambuliki na shirikisho la kimataifa kama ilivyokuwa kwa Sulle,” alisema.