25.8 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

Sirro aacha maswali zaidi kutekwa Mo

Na WAANDISHI WETU -DAR ES SALAAM


RIPOTI ya kwanza ya uchunguzi wa awali iliyotolewa jana na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, (IGP) Simon Sirro inayoonyesha kuwa, watu waliomteka  mfanyabiashara Mohammed Dewji (Mo), walitumia gari aina ya  Toyota Surf lenye namba za usajili AGX 404 MC, imeibua mjadala.

Sirro, ambaye hii ni mara yake ya kwanza kujitokeza hadharani kuzungumzia tukio la kutekwa kwa Mo, mbali na kutaja namba za usajili, pia alitoa picha tatu zinazoonyesha gari hilo wakati akizungumza na waandishi wa habari jana katika Ukumbi wa Makao Makuu ya Jeshi la Polisi jijini Dar es Salaam.

Picha hizo, moja inaonyesha gari hilo likiwa limeegeshwa nje ya nyumba (si katika Hoteli ya Colosseum) sambamba na gari jingine la rangi nyeupe, nyingine inaonyesha upande wa ubavu wa gari hilo na ya tatu inaonyesha nyuma ya gari hilo.

Hata hivyo, Sirro hakuweka wazi kama picha hizo alizozitoa ni za CCTV au la!

Akizungumzia mwonekano wa gari hilo lenye rangi ya bluu nyeusi (dark blue) na ufito wa rangi ya shaba kwa chini (ingawa picha zinaonyesha ufito huo ni wa rangi ya fedha), Sirro alisema ulinaswa, lakini katika hali ya kufifia kupitia kamera za CCTV katika eneo la tukio.

IGP Sirro alisema katika uchunguzi wao huo wamebaini kuwa gari hilo liliingia nchini Septemba 1 mwaka huu, likitokea nchi jirani ambayo hakutaka kuitaja kwa sababu ya kulinda uchunguzi.

Ingawa Sirro alikataa kutaja nchi ambayo gari hilo limetokea, uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini kuwa Tanzania imezungukwa na nchi jirani nane na kati hizo, namba hiyo inafanana na zile zinazosajiliwa nchini Msumbiji.

Ukiacha hilo, watu wenye uzoefu wa ama safari za kikazi na maisha katika nchi zinazoizunguka Tanzania wanasema haichukui muda kufahamu gari lilikosajiliwa na mmiliki wake, hususan Msumbiji.

Ubalozi wa Msumbiji nchini haukupatikana jana kuzungumzia hilo, juhudi za kuwatafuta wahusika zinaendelea.

Kwa mujibu wa IGP Sirro, wakati gari hilo likiingia nchini lilikuwa likiendeshwa na dereva aliyetambulika kwa jina la Obasanjo Zacharia Junior.

Hata hivyo, Sirro hakuweka wazi picha ya dereva huyo wala maelezo yake zaidi, licha ya kwamba utaratibu unamwelekeza mhusika/dereva kuacha taarifa muhimu mpakani kabla ya kuingia nchini.

BARABARA ZILIZOTUMIKA

Akielezea barabara ambazo gari hilo ilizitumia baada ya kumteka Mo, Sirro alisema kwa msaada wa CCTV, wamebaini kuwa baada ya watekaji kutekeleza tukio hilo Hoteli ya Colosseum  Alhamisi iliyopita, walipita katika barabara takribani tano tofauti.

“Gari hili lilipita katika barabara za Haile Sellassie, Ali Hassan Mwinyi, Kimweri, Maandazi, Mwai Kibaki na baadaye lilipotelea eneo la Mlalakuwa karibu na mzunguko wa Kawe, bado watu wetu wanaendelea na uchunguzi ili tujue kama gari hilo limeelekea maeneo ya Silver Sand au walielekea maeneo ya Kawe,” alisema IGP Sirro.

Alisema Jeshi la Polisi bado linafanya juhudi kubwa za kupita na kuchunguza jengo kwa jengo katika eneo ambalo wanaamini kwamba gari hilo lilipotelea.

RISASI ZILIZOTUMIKA

Mbali na hilo, alisema uchunguzi wao pia umebaini wahalifu hao walikuwa na silaha aina ya bastola inayotumia risasi zenye ukubwa wa milimita tisa.

“Taarifa zimetuwezesha  kubaini kuwa, bila shaka Mohammed Dewji alitekwa na watu waliokuwa na silaha aina ya ‘pistol’ (bastola), baada ya tukio hilo tulipata risasi mbili ambazo tumezipeleka  kuzichunguza kwenye laboratory forensic (maabara ya kuchunguza silaha), uchunguzi bado unafanyika, lakini tumebaini risasi ile ilikuwa na ukubwa wa milimita tisa,” alisema IGP Sirro, ambaye alisisitiza kuwa, vijana wake hawajalala kwa siku tisa sasa wakiwasaka watekaji.

INTERPOL

Alisema polisi kwa kushirikiana na Polisi wa Kimataifa (Interpol), wanaendelea kufanya msako kuhakikisha wanampata mmiliki wa gari hilo na kazi ambayo anafanya dereva wake.

“Jeshi la Polisi na vyombo vyote vya ulinzi na usalama vimeimarisha ushirikiano katika utafutaji wa mahali alipofichwa mfanyabiashara Mo, pia tumeimarisha ulinzi mipakani ili watekaji wa mfanyabiashara huyo wasiweze kuvuka nje ya mipaka ya nchi yetu,” alisema IGP Sirro.

WATUHUMIWA

Aidha, IGP Sirro alisema kati ya watuhumiwa 27 waliokuwa wamekamatwa, wanane bado wanashikiliwa na Jeshi la Polisi, miongoni mwao yumo kapteni wa boti.

Kutokana na tukio hilo, IGP Sirro amewataka wafanyabiashara wakubwa kuchukua tahadhari za kiusalama  na ikibidi wawe na walinzi wakati wote ili waweze kujilinda pamoja na kutoa taarifa  mapema wanapopata vitisho dhidi ya maisha yao.

“Tulikuwa tunajaribu kupitia taarifa za Mo, tunaamini ana silaha, lakini siku hiyo ya tukio hakuwa nayo, mbaya zaidi hata dereva hakuwa naye siku hiyo,” alisema IGP Sirro.

MAJIBU YA IGP SIRRO BAADA YA MASWALI

Akijibu maswali ya waandishi wa habari, Sirro alisema wanashirikiana vizuri na Polisi wa Kimataifa (Interpol) katika suala hilo.

Hata hivyo, alikwenda mbali kwa kusema hoja ya nani aje kusaidia katika uchunguzi, vyombo vya dola ndivyo vinavyoweza kuona sababu na kujua namna ya kumshauri Rais katika hilo.

Alisisitiza kuwa, kwa sasa hawaoni sababu ya kuomba msaada na ni vyema kulinda heshima ya nchi, kwa kuwa vyombo vya ndani vya usalama vina uwezo na weledi wa kutosha kutekeleza majukumu yake, bila msaada kutoka kwa vyombo vya nje.

Alisema anakutana na vyombo vingi vya usalama vya mataifa mbalimbali na kusisitiza kuwa, vyombo vya ndani vya Tanzania viko vizuri kwa sababu kuna matukio mengi yametokea nchini na wameyashughulikia kwa weledi wa hali ya juu.

Alipoulizwa kama uchunguzi wao huo wa awali umebaini malengo ya watekaji na kama Mo yupo hai, Sirro alisema hana uhakika na kwamba watafahamu hayo yote watakapowakamata watekaji.

Alisema hana majibu kuhusu iwapo gari hilo lililotumika kumteka Mo kama bado liko ndani ya nchi au limeshavuka mipaka na kuwaomba wananchi wenye taarifa na wenye kamera katika makazi yao wawasaidie kuweza kupata taarifa zaidi.

“Mimi huwa ni muwazi sana, huyu anayetaka kuharibu taswira ya nchi yetu tukimkamata atajua hii ni Tanzania, na niwape salamu tu huenda kuna waandishi wa habari mnawajua, mimi ninasema nitawagonga kwa mujibu wa sheria, huyu anayetufanya sisi tunazunguka na watu wangu hawalali, tukimkamata atajua hii ni Tanzania,” alisema.

Kwa wanaotoa taarifa za uongo, alisema si jambo jema na kuwataka Watanzania kuwa wazalendo kwa kuwatendea haki polisi na nchi yao kwa kutoa taarifa zinazotoa mwelekeo.

Alisema suala la kudhibiti masuala ya utekaji ni la kimkakati na linahitaji uwekezaji kwenye suala la kamera, kwa kuwa teknolojia hiyo inasaidia sana kubaini.

Alipoulizwa kuhusu kuchezewa kwa kamera za CCTV katika Hoteli ya Colosseum, Sirro alisisitiza kuwa, hazikuchezewa, bali siku ya tukio na muda ulisababisha picha kuonekana zikiwa zimefifia.

Kuhusu kupotea watu wengine kama ilivyotokea kwa akina Ben Saanane na Azori Gwanda, alisema tayari yameshazungumzwa na mengi na kwamba wapo wengi wanaopotea kwa sababu mbalimbali, suala ambalo ni tofauti na kutekwa kwa Mo.

Alieleza kuwa, suala la kupeleleza kesi si suala la kuzurura barabarani, bali ni suala linalohitaji utaalamu, muda na rasilimali ili kupata ukweli kuhusu kile kinachopelelezwa.

Mfanyabiashara Mohammed Dewji (Mo) alitekwa nyara na watu wasiojulikana alfajiri ya Oktoba 11, mwaka huu, alipokuwa akiingia mazoezini katika Hoteli ya Colosseum, iliyopo Oysterbay, jijini Dar es Salaam.

Habari hii imeandaliwa na Aziza Masoud, Andrew Msechu na Evans Magege.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles