Na THERESIA GASPER-DAR ES SALAAM
ALIYEKUWA kocha msaidizi wa Simba, Masoud Djuma, ameitega Yanga baada ya kusema kuwa yupo tayari kuinoa timu hiyo, lakini kwa sharti la kuwa kocha mkuu.
Simba ilimtupia virago Djuma hivi karibuni, baada ya kutokuwapo kwa maelewano kati yake na kocha mkuu wa timu hiyo, Patrick Aussems.
Kaimu Rais wa Simba, Salim Abdalah ‘Try Again’, akizungumza siku moja kabla ya kumtimua kocha huyo, alisema uongozi wa klabu yake ulifanya jitihada za kutafuta suluhu ya maelewano duni kati ya kocha wao mkuu na msaidizi lakini uligonga mwamba.
Baada ya kutimuliwa, alihusishwa na kujiunga na Yanga ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikihusishwa kutamani kufanya kazi na klabu hiyo.
Kuhusishwa kwake na Yanga kulianza baada ya aliyewahi kuwa kocha wa timu hiyo, George Lwandamina, alipoamua kuikacha na kurejea katika klabu yake ya zamani ya Zesco inayoshiriki Ligi Kuu ya Zambia.
Hata hivyo, Yanga kwa sasa inanolewa na kocha Mkongomani, Mwinyi Zahera, ambaye katika msimu huu wa Ligi Kuu Tanzania Bara ameiongoza kushinda mechi tano na kutoka sare moja, hivyo kuvuna pointi 16 zilizoiweka katika nafasi ya tatu katika msimamo.
Mbali ya Yanga, Djuma amesaini mkataba wa mwaka mmoja na klabu ya As Kigali inayoshiriki Ligi Kuu nchini Rwanda, baada ya aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Erick Nshimiyiman, kujiuzulu.
Akizungumza na MTANZANIA akiwa Kigali, Djuma alisema si Yanga pekee, lakini kwa sasa atakuwa tayari kuinoa timu yoyote kwa sharti la kuwa kocha mkuu na si msaidizi.
“Ni kweli nimemalizana na klabu ya AS Kigali kama ulivyosikia na kila kitu kinakwenda sawa.
“Nafahamu Yanga wana kocha mzuri tu, lakini kama watanihitaji mimi kwa sasa sipo tayari kuwa msaidizi kama ilivyokuwa nyuma,” alisema.
Kocha huyo raia wa Burundi, kabla ya kujiunga na Simba alikuwa akiinoa Rayon Sports ya Rwanda ambayo alifanikiwa kuipa makombe mawili ya ubingwa wa ligi na Kombe la Amani.