31.7 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Maji, mila vinakwamisha hedhi salama kwa wanafunzi Kilwa

Na YUSUFU AHMADI

MIONGONI mwa masuala yanayofanyiwa kampeni kubwa hapa nchini na katika nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara barani Afrika, ni juu ya hedhi salama kwa wanawake wakiwamo wanafunzi.

Hata hivyo, kampeni hizo zinakabiliwa na vikwazo vingi ambavyo visipotafutiwa ufumbuzi, huenda juhudi zote hizo zisizae matunda.

Utafiti wa mwaka 2010 wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) unaonesha kuwa kati ya wanafunzi 10 Afrika, mwanafunzi mmoja hutoroka shuleni wakati wa kipindi cha hedhi.

Nao Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) unaonesha kuwa wanafunzi wa kike hapa nchini wamekuwa wakitoroka shuleni kwa siku 60 ndani ya mwaka wanapokuwa kwenye hedhi.

Katika kampeni hizo moja ya kifaa muhimu kinachopiganiwa zaidi katika kuhakikisha uwapo wa hedhi salama ni upatikanaji wa taulo za kike.

Na tayari kwa upande wa Serikali umeshachukua hatua kujibu kampeni hizo.

Hatua hiyo ni  kuondoa kodi ya ongezeko la thamani (VAT) kwenye taulo hizo za kike (sanitary pads) ili kuwezesha upatikanaji wake kwa bei rahisi na kwa haraka.

Juhudi hizo za Serikali zinaenda sambamba na lengo namba 5 la malengo ya maendeleo endelevu(SDGs) kipengele cha 5.6 kinachohimiza afya ya uzazi, tendo la ndoa na haki za uzazi ambapo ni pamoja na masuala ya hedhi.

 

Ukosefu wa maji shuleni

Baadhi ya wanafunzi, walimu na kundi la marafiki wa elimu wilayani Kilwa mkoani Lindi, walibainisha kuwa changamoto kubwa kwa shule nyingi ni ukosefu wa maji ya uhakika na miundombinu rafiki katika suala la hedhi.

Mwalim Mkuu wa Shule ya Msingi Mkwanyule, iliyopo Kata ya Kilwa Masoko, Hamisi Kassinge, anasema ukosefu wa maji ya kutosha kwa shule nyingi wilayani humo bado ni kikwazo kuelekea hedhi salama.

“Licha ya suala la taulo za kike kupatiwa majibu, maji nayo ni muhimu katika matumizi ya taulo hizo ili kumfanya mtoto wa kike awe katika hali nzuri zaidi,” anasema Mwalim Kassinge.

Naye Lucy Mkapa ambaye ni rafiki wa elimu wilayani humo, anasema ubadilishaji wa taulo hauna budi uambatane na maji ili kumkinga mtoto na maradhi.

Mwalimu Mlezi wa Shule ya Msingi Mkwanyule, Bibiye Kaudunde, anasema maji ni muhimu katika hedhi salama kwani wapo wanafunzi hukumbwa na hali hiyo wawapo shuleni.

“Maji ni muhimu kwani kuna wakati inatokea binti yupo shuleni anapatwa na hiyo hali, kukiwa na maji inakuwa rahisi kwake kujisafisha na kuwa katika mazingira safi,” anasema Mwalimu Kaudunde.

 

Vyumba maalumu

Suala la vyumba maalum vya faragha vya kubadilishia taulo hizo nalo linapaswa kupewa kipaumbele.

Diwani Viti Maalumu (CCM) kata ya Kilwa Masoko, Fatuma Kindamba, anasema chumba cha kubadilishia taulo za kike ni muhimu ili kumpa mtoto wa kike nafasi ya kubadilisha taulo hizo.

“Kama hakutawekwa vyumba maalumu mwanafunzi atakaa nazo kutwa nzima mwilini, jambo ambalo si zuri kiafya na kwa maendeleo ya elimu yake,” anasema.

Anasema suala la uwapo wa choo ambacho kina miundombinu ya kuhifadhi taulo hizo ni muhimu kwa hedhi salama.

 

Mila na desturi

Katibu Mtendaji wa Asasi ya Tumaini Jipya la Wanawake Kilwa (TUJIWAKI), Pili Kiliwa, anasema wilayani humo kuna  mila iitwayo Mindule ambayo inamlazimisha mtoto wa kike kutumia nguo moja wakati wa hedhi katika maisha yake yote.

“Mtoto wa kike hukabidhiwa nguo maalumu kwa ajili ya hedhi ambayo atatakiwa kuitumia katika maisha yake yote hata akiwa ameolewa,” anasema.

Anasema nguo moja kutumika kwa matumizi ya hedhi ni jambo lisilofaa kiafya na kwamba wamekuwa wakitoa elimu juu ya jambo hilo.

Naye mhasibu na mwanasheria msaidizi kutoka Kitengo cha Msaada wa Kisheria kwa wanawake na watoto Kilwa (KIWOPAO), anasema tatizo la imani za kishirikina limekuwa kubwa.

“Tatizo hapa kuna imani za kishirikina, baadhi ya wazazi wamekuwa wakiwakataza watoto wao kutumia hizo taulo za kike wakisema zina mambo mabaya na wegine wakisema si nzuri kiafya,” anasema Boston.

Mtaalamu wa masuala ya afya kutoka Hospitali ya Tumbi Kibaha mkoani Pwani, Mwanaisha Mrisho, anasema jambo hilo linaweza kuleta madhara endapo nguo hiyo haitakauka vizuri inapofuliwa kwa sababu inasababisha bakteria kuzaliana.

 

Jitihada za hedhi salama

Kumekuwapo na jitihada kwa baadhi ya shule wilayani humo kutenga asilimia ya fedha za ruzuku kutoka serikalini (capitation grant) kwa ajili ya kuwahudumia wanafunzi wa kike.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mkwanyule, Kata ya Masoko, wilayani Kilwa mkoani humo, Hamisi Kassinge, anasema shule yake imeanza kutenga fedha kuwahudumia wanafunzi wa kike katika masuala ya hedhi salama kutokana na agizo la Serikali linalowataka wafanye hivyo.

Anasema shule yake imekuwa ikitenga kiasi cha Sh 50,000 kwa mwezi kwa ajili ya huduma ya hedhi salama.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles