KATIKA hali isiyo ya kawaida, ingawa isiyoshangaza sana kutokana na utamaduni uliopo nchini India kuhusu ng’ombe, Serikali ya Jimbo Madhya Pradesh, katikati mwa India imetangaza mpango wa kuanzisha wizara ya masuala ya ng’ombe.
Waziri Mkuu wa Jimbo la Madhya, Pradesh Shivraj Singh Chouhan, anasema hatua hiyo itachangia kuongezwa kwa fedha za kusaidia uhifadhi wa ng’ombe.
Taarifa zinasema Chouhan, ambaye anatoka Chama cha BJP, amechukua hatua hiyo kama moja ya njia za kujaribu kumzidi mgombea wa chama cha upinzani cha Congress kuwavutia wapiga kura wa jimbo hilo, wanaowathamini ng’ombe kama mungu.
Alitoa tangazo hilo siku chache baada ya kiongozi wa Chama cha Congress katika jimbo hilo, Kamal Nath, kuahidi kuanzisha makao ya kutoa hifadhi kwa ng’ombe iwapo chama chake kitashinda uchaguzi.
Anasema amesikitishwa na vifo vya ng’ombe ambao mara kwa mara hugongwa na magari wakivuka barabara katika ya jimbo hilo.
Lakini Chama cha BJP kimemshutumu mgombea huyo na kusema imekuwa ni sera ya Chama cha Congress kutoa ardhi ya malisho kwa watu wengine na hivyo kupunguza malisho ya ng’ombe.
Jimbo hilo limekuwa na bodi ya kuangazia maslahi ya ng’ombe yanayofahamika kwa jina la Gau Samvardhan, lakini Chouhan anaamini kwamba wizara ndiyo itakayofaa zaidi kutetea maslahi ya ng’ombe.
“Bodi hii inakumbwa na matatizo ya kifedha lakini kukiwa na wizara tatizo hilo halitakuwapo tena,” amenukuliwa na gazeti la Hindustan Times akisema.
Ng’ombe hutambulika kuwa mnyama mtakatifu na waumini wa dini ya Kihindu walio wengi nchini India na kwamba mauaji ya viumbe hao ni haramu katika majimbo mengi nchini humo.