Na Upendo Mosha- Rombo
JESHI la polisi mkoani Kilimanjaro linamshikilia Charles Colner (21) kwa tuhuma za kumbaka ajuza wa miaka 85 wilayani Rombo.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Koka Moita, alisema tukio hilo lilitokea Oktoba 15 jioni katika Kijiji cha Kingachi, Kata ya Kingachi wilayani humo.
Alisema mwanamke huyo ambaye jina lake limehifadhiwa, alibakwa na kijana huyo baada ya kumvamia na kuvunja mlango wa nyumba yake.
Alisema baada ya kuvunja mlango kijana huyo alimvuta nje mwanamke huyo na kumfanyia kitendo hicho.
“Baada ya kuingia ndani alimvuta nje na baadaye alimlaza kando ya nyumba hiyo na kumfanyia kitendo hicho,” alisema.
Alisema baada ya kijana huyo kufanya kitendo hicho, alikimbia na raia wema walitoa taarifa polisi.
Baada ya msako mkali polisi waliweza kumkamata na kumfikisha katika Kituo cha Polisi Moshi, alisema.
“Kwa sasa tumemhifadhi na baada ya uchunguzi kukamilika tutamfikisha mahakamani kujibu shitaka linalomkabili,”alisema Kamanda.
Wakati huo huo, Jeshi la polisi mkoani hapa limewakamata wahamiaji haramu zaidi 11 kutoka Ethiopia kwa kuingia nchini kinyume cha sheria.
Kamanda Moita alisema wahamiaji hao haramu walikamatwa Oktoba 15 jioni katika eneo la Kisangiro Mforo-Kati, Kata Mwanga wilayani Mwanga wakati askari wakiwa doria.
“Askari wetu waliwakamata wahamiaji haramu 11 kutoka Ethiopia.
“Watu hao walikutwa wakiwa wamefungiwa kwenye nyumba ya mtu mmoja, Hemed Kauva (31), dereva bodaboda mkazi wa Kisangiro.
“Mbali na kuwakamata hao pia tumemkamata kijana huyo ambaye ndiye alikuwa mwenyeji wao,”alisema.