Ajuza wa miaka 85 abakwa na kijana wa miaka 21

0
1125

Na Upendo Mosha- Rombo

JESHI la polisi mkoani Kilimanjaro linamshikilia     Charles Colner (21) kwa tuhuma za kumbaka ajuza   wa miaka 85  wilayani Rombo.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Koka Moita, alisema tukio hilo lilitokea Oktoba 15   jioni katika Kijiji cha Kingachi, Kata ya Kingachi wilayani humo.

Alisema mwanamke huyo ambaye jina lake limehifadhiwa, alibakwa na kijana huyo baada ya kumvamia na kuvunja mlango wa nyumba yake.

Alisema baada ya kuvunja mlango  kijana huyo alimvuta nje mwanamke huyo na   kumfanyia kitendo hicho.

“Baada ya kuingia ndani alimvuta nje na baadaye alimlaza kando ya nyumba hiyo na  kumfanyia kitendo hicho,”  alisema.

Alisema baada ya kijana huyo kufanya kitendo hicho, alikimbia na raia wema walitoa taarifa polisi.

Baada ya msako mkali polisi waliweza kumkamata na kumfikisha katika Kituo cha Polisi Moshi, alisema.

“Kwa sasa tumemhifadhi na baada ya uchunguzi kukamilika tutamfikisha mahakamani  kujibu shitaka linalomkabili,”alisema Kamanda.

Wakati huo huo, Jeshi la polisi mkoani hapa limewakamata  wahamiaji haramu zaidi 11 kutoka  Ethiopia  kwa kuingia nchini kinyume cha sheria.

Kamanda Moita alisema wahamiaji hao haramu walikamatwa Oktoba 15   jioni katika eneo la Kisangiro Mforo-Kati, Kata  Mwanga  wilayani Mwanga wakati askari wakiwa doria.

“Askari wetu waliwakamata  wahamiaji haramu 11 kutoka   Ethiopia.

“Watu hao walikutwa wakiwa wamefungiwa  kwenye nyumba ya mtu mmoja,   Hemed   Kauva (31), dereva bodaboda mkazi wa Kisangiro.

“Mbali na kuwakamata hao pia tumemkamata kijana huyo ambaye ndiye alikuwa mwenyeji wao,”alisema.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here