NA ADAM MKWEPU-DAR ES SALAAM
TIMU ya soka ya Taifa, ‘Taifa Stars’, jana ilifufua matumaini ya kucheza fainali za Afrika mwakani nchini Cameroon, baada ya kuichapa Cape Verde mabao 2-0 katika mchezo uliochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Boa la kwanza la Taifa Stars lilifungwa katika dakika ya 29 na Simon Msuva
wakati la pili  likifungwa dakika ya 57 na Mbwana Samatta.
Mchezo huo wa marudiano ulichezwa baada ya ule wa Oktoba 12 mwaka huu na Stars ikifungwa mabao 3-0 ikiwa ugenini Cape Verde.
Ushindi huo unaifanya Stars kupaa hadi nafasi ya pili katika msimamo wa Kundi L wakati ikisubiri matokeo kati ya Uganda na Lesotho ambao walicheza jana saa 1:00 usiku nchini Lesotho.
Stars kwa sasa imefikisha pointi tano wakati vinara wa kundi hilo Uganda (The Crane) wakiwa na pointi saba kabla ya mchezo wa jana, huku Cape Verde ikishika nafasi ya tatu ikiwa na pointi nne, Lesotho ikishika mkia na pointi mbili.
Katika mchezo wa jana Stars iliingia uwanjani ikihitaji pointi tatu muhimu kujihakikishia kufuzu hatua inayofuata ambayo mara ya mwisho timu hiyo kushiriki ilikuwa mwaka 1980.
Lakini Cape Verde ilianza mchezo huo kwa kasi huku dakika ya nane ikikosa kufunga bao la mapema hali ambayo ingesababisha kuivunja moyo Stars.
Safu ya ushambuliaji ya Cape Verde ambayo ilikuwa ikiwaunganisha Ricardo Gomez na Rodrigas, ilionekana kuwa hatari kwa Stars baada ya kulishambulia lango la timu hiyo mara kwa mara.
Dakika ya 10 alimanusura Cape Verde ipate bao la kuongoza kupitia kwa Rodrigaz ambaye mpira wake wa  kichwa aliopiga akiwa eneo la hatari ulitoka nje akimalizia krosi iliyopigwa na Ricardo.
Kosakosa hiyo iliwashtua Stars ambayo dakika ya 13 ilitaka kupate bao la kuongoza hata hivyo mpira wa kichwa uliopigwa na Msuva akiwa ndani ya eneo la hatari akiunganisha krosi ya Samatta, ulitoka nje.
Stars ilionekana kuelewana vema eneo la kati iliyokuwa ikiunganishwa na kiungo Mudathiri Yahya akisaidiana Msuva na  Samatta kusogeza mashambulizi mbele.
Dakika ya 16, Rodrigaz alitaka kuipatia timu yake bao lakini shuti lake alilopiga akiwa ndani ya eneo la hatari lilitoka nje.
Dakika ya 21, beki wa Cape Varde alionyeshwa kadi ya njano baada ya kumfanyia madhambi Msuva akiwa eneo la hatari, dakika ya 22, Samatta alikosa mkwaju wa penalti baada ya shuti lake kugonga mwamba wa juu.
Stars haikukata tamaa licha ya kuendelea kulishambulia lango la Cape Verde bila mafanikio.
Dakika ya 29, Msuva aliipatia Stars la kwanza akiwa eneo la hatari akimalizia mpira uliopigwa na Samatta ambaye alifanya kazi ya ziada ya kuukokota mpira hadi eneo la hatari akitokea upande wa kushoto.
Dakika ya 38, Msuva alitaka kufunga bao la pili akiwa ndani ya 18 lakini shuti lake lilitoka nje baada ya kupokea pasi kutoka kwa Samatta.
Licha ya kuelemewa na mashambulizi ya mara kwa mara, dakika ya 44 Cape Verde walitaka kusawazisha bao kupitia kwa Gomez, lakini shuti lake liliokolewa na kipa Aishi Manula.
Dakika 45 zilimalizika huku Stars ikiwa mbele kwa bao 1-0.
Kipindi cha pili Stars ilianza kwa kasi ikionekana kulisaka bao la pili lakini ilipata wakati mgumu kutokana na uimara wa safu ya ulinzi ya Cape Verde.
Dakika ya 48, Samatta alikosa bao akiwa eneo la hatari baada ya kupiga shuti na kupaa juu ya lango akijaribu kutumia vema pasi ya Msuva.
Akionekana kudhamiria kutafuta pointi tatu muhimu, Kocha Emmanuel Amunike, alimpumzisha beki, Abdul Banda na nafasi yake kuchukuliwa na mshambuliaji, John Bocco.
Mabadiliko hayo yalionekana kuongeza morali kwa Stars kuendelea kulishambulia lango la Cape Verde mara kwa mara hali ambayo iliwafanya mabeki wake kufanya makosa ya kizembe.
Dakika ya 57, Samatta aliiongezea bao la pili Stars baada ya kuachia shuti akiwa nje kidogo ya eneo la hatari akiwa amepokea pasi ya kiungo Mudathiri Yahaya.
Dakika ya 59, kocha Amunike aliamua kumpumzisha Yahya na nafasi yake kuchukuliwa na Feisali Toto.
Dakika ya 62, John Bocco ilibaki kidogo  aipatie Stars bao la tatu lakini shuti lake lilipita pembeni ya lango la Cape Verde.
Kuingia kwa Feisal Toto na John Bocco kulionekana kuimarisha safu ya ushambuliaji ya Stars.
Dakika ya 75, Samatta alipania kuipatia bao la tatu Stars lakini uimara wa safu ya ulinzi ya Cpae Verde ulisaidia kuokoa hatari hiyo.
Timu hizo ziliendelea kushambuliana kwa zamu huku Cape Verde ikionekana kusaka bao ambalo lingefufua matumaini ya kupata ushindi katika mchezo huo.
Dakika 90 zilimalizika Stars ikiibuka na ushindi wa mabao 2-0.
Kikosi cha Stars kilichoanza kilikuwa, Aishi Manula, Shomari Kapombe, Abdi Banda/John Bocco, Aggrey Morris, Kelvin Yondani, Erasto Nyoni, Himid Mao, Mudathir Yahya/Feisal Salim, Mbwana Samatta/Rashid Mandawa, Simon Msuva pamoja na Gadiel Michael.
Cape Verde wao walikuwa Graca Theirry, Almeid Tiago/Rocha Nuno, Rodrigues Carlos, Barros Admilson, Tavares Ianique, Fortes Jeffry, Macedo Elvis, Rodrigues Garry, Soared Luis/Ramos Heldon, Semed Jorge pamoja na Gomes Ricardo/Silva Gilson.