Na KHAMIS SHARIF-ZANZIBAR
CHAMA cha Wananchi (CUF) kimelalamikia hatua ya chama tawala CCM kukandamiza demokrasi ya vyama vingi visiwani Zanzibar.
Wamedai ukandamizwaji huo unafanywa na CCM jambo ambalo ni hatari kwa vyama vingine vya siasa vilivyopo visiwani hapa.
Akizungumza na MTANZANIA jana mjini Unguja, Makamu Mwenyekiti mstaafu wa CUF, Juma Duni Haji, alisema chama chao kimebaini njama alizodai za CCM kujifanya nyoka kumeza vyama vingine vya siasa.
Alisema historia inaonesha upinzani Zanzibar umekuwa ukifanya vizuri katika chaguzi zote tangu ulipoingia mfumo wa vyama vingi nchini ingawa yanayojitokeza ni uminywaji wa wazi wa demokrani unaofanywa na watawala.
“2015 upinzani Zanzibar ulifanya vizuri zaidi, lakini Serikali ilielekeza nguvu zake zote za kiharamu katika uchaguzi ule hadi kuona kwamba lisilowezekana kwao kuwa rahisi kuwezekana.
“Bado tunajipanga kuelekea uchaguzi mwingine 2020 na tayari kumekuwa na figisu figisu za CUF kutoshiriki ila bado tutaonesha ukomavu wetu kisiasa.
“Kama uchaguzi wa mwaka 2020 hali ya ukandamizaji itaendelea kama chaguzi zilizopita kwa kujawa vituko, watakutana na nguvu ya wananchi,” alisema.
Duni ambaye alikuwa mgombea mwenza wa urais kupitia Chadema mwaka 2015, alisema CUF kwa sasa inaangalia hatua mbalimbali za kuweza kujikomboa kwa kukataa kwa vitendo uburuzwaji wa demokrasi unaofanywa na CCM.
Alisema sasa umefika wakati kwa Tanzania kupata washauri wa masuala ya demokrasi jambo ambalo litasaidia kutekeleza misingi ya haki kwa vyama vyote kuweza kuwasiliana na wananchi bila hofu.
“Uchaguzi wa mwaka 2015 ulikuwa patashika nguo kuchanika, CUF kupitia Maalim Seif ni nani asiyejua nani alishinda kihalali,” alisema.
Katika uchaguzi huo ambao matokeo yake yalizua utata baada ya Maalim Seif kujitangazia ushindi, Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kupitia Mwenyekiti wake Jecha Salim Jecha ilitangaza kufutwa kwa matokeo hayo kwa kile kilichoelezwa kutawaliwa na vitendo vya udanganyifu.
ZEC ilitangaza uchaguzi wa marudio uliofanyika Machi 2016, lakini CUF ilitangaza kutoshiriki kuanzia ngazi ya urais, uwakilishi hadi udiwani hatua ambayo iliiwezesha CCM kushinda viti vyote na Dk. Ali Mohamed Shein kutangazwa mshindi kwa zaidi ya kura 300,000.