NA MWALI IBRAHIM, DAR ES SALAAM
WEKUNDU wa Msimbazi, Simba, tayari wametua mkoani Tanga kamili kuchukua pointi sita ambapo wamepania kuanza kuzisaka kwa African Sports ‘Wana Kimanumanu’, wanaokutana nao kesho, Uwanja wa Mkwakwani.
Simba itacheza michezo miwili ikiwa mkoani humo, ambapo baada ya kumalizana na Wana kimanumanu hao itakaa kuwasubiria Mgambo JKT, ambayo watakutana nayo Septemba 16, kwenye uwanja huo.
Timu hiyo imeondoka jana, huku ikimkosa mchezaji Abdi Banda, ambaye atakuwa nje ya uwanja kwa mwezi mmoja, akiendelea na matibabu yake ya nyama za paja huku wachezaji wengine wakiwa kikosini, akiwemo Jonas Mkude, ambaye alikuwa majeruhi.
Mchezo huo wa ligi utakuwa wa kwanza kwa kocha Dylan Kerr, ambaye amechukua mikoba ya Goran Kopunovic, aliyemalizana na Simba baada ya Ligi Kuu msimu uliopita kumalizika wakiwa nafasi ya tatu.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Kaimu Katibu Mkuu wa klabu hiyo, Collins Frisch, alisema timu yao imeondoka jana ikiwa kamili, huku wakiwa na nguvu ya kuhakikisha wanarudi na pointi zote sita walizozifuata.
“Tumekwenda kusaka pointi sita, tatu kwenye mchezo wetu wa kwanza na African Sports, nyingine kwa Mgambo na tunaamini tutazichukua kutokana na
ari tuliyokuwa nayo,” alisema.
Alisema, wana imani na usajili walioufanya msimu huu chini ya kocha huyo ambaye alipewa jukumu la kuangalia viwango vya wachezaji, ili kumchagua atakayeridhishwa naye na ndio hao waliosajiliwa.
Collins alisema sambamba na hilo, pia maandalizi yote ya timu yalifanywa kulingana na mahitaji ya kocha, ambapo pamoja na yote, mechi za kirafiki waliweza kujipima na timu 11, zikiwemo timu za Uganda.