25.8 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 27, 2024

Contact us: [email protected]

Wadau wa michezo, sanaa washtushwa Mo kutekwa

Na THERESIA GASPER-DAR ES SALAAM

MWEKEZAJI wa Simba na mfanyabiashara maarufu nchini, Mohamed Dewji ‘Mo’, amezua taharuki miongoni mwa wadau wa michezo na burudani baada ya jana kutekwa na watu wasiojulikana wakati akielekea katika mazoezi ‘gym’.

Tukio hilo, ambalo limethibitishwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, Mulilo Ramadhan, lilitokea saa 11 alfajiri wakati Mo akiingia katika gym ya Coliseums, iliyopo Oysterbay, jijini Dar es Salaam.

Vyanzo kutoka eneo la tukio vililiambia MTANZANIA kuwa, watekaji walifanikisha mpango wao wa kumteka Mo ambaye pia ni mwanachama wa Simba mwenye kadi namba 7,062, baada ya kufyatua risasi hewani kwa ajili ya  kuwatisha walinzi wa hoteli hiyo.

Mshambuliaji wa Simba, John Bocco, aliandika kupitia ukurasa wake wa Instagram: “Mungu akusimamie na kukulinda huko uliko inshaallah, atakuepusha na changamoto zote na kurudi salama.”

Beki wa Simba, Shomari Kapombe, aliandika: “Eee God (Mungu) nenda ukamtie nguvu na kumlinda na awe katika ushindi kwenye hili, tunakuombea na Mungu atakufanyia wepesi.”

Pascal Wawa, ambaye pia ni beki wa Simba aliandika: “Our prays are with you” (Maombi yetu tumeyaelekeza kwako)”, huku mshambuliaji wa timu hiyo Mganda, Emmanuel Okwi akiandika: “All will be well (kila kitu kitakuwa sawa).

Msanii wa muziki wa Bongo fleva, Rehema Chalamila ‘Ray C’, aliandika katika ukurasa wake wa instagram: “Hii si Tanzania ninayoijua mimi, inauma, inakera, inasikitisha, inatisha, utakuwa sawa Mo, tunakuombea kaka.”

Msanii wa muziki wa hip hop, ambaye pia ni Mbunge wa Mikumi, Joseph Haule, ‘Professor Jay’, aliandika: “Watu wasiojulikana tena, tunakuombea sana kaka”, huku msanii Nurdin Bilal ‘Shetta’ akiandika “Inshallah utakuwa sawa boss.”

Mbunge wa Jimbo la Iramba Magharibi mkoani Singida, Mwigulu Nchemba, aliandika: “Comrade, this too shall pass, nakuombea uwe salama.”

Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa Simba, Haji Manara, aliandika: “Insha Allah kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu na kwa jitihada za vyombo vyetu vya ulinzi na usalama, Khalifa wetu Bwana Mohamed Dewji ‘Mo’ atapatikana haraka iwezekanavyo akiwa mzima na salama na watekaji nao kutiwa mikononi.”

Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa Yanga, Dismas Ten, alisema: “Kitengo hicho ni cha kusikitisha sana, ukiangalia mtu kama Mo analeta maendeleo katika soka, kila mtu anaumizwa na hili, tunamuombea kwa Mungu aweze kupatikana akiwa salama na kurejea katika shughuli zake za kila siku.”

Mwigizaji Steve Mangele ‘Steve Nyerere’,  aliandika: “Pole kwa familia, najua na kutambua kila mtu sasa hivi anaongea lake, cha muhimu ni kuwapa ushirikiano Jeshi letu la Polisi, kaka yetu, rafiki yetu apatikane, jambo hili halina ushabiki wa Simba wala Yanga, wote tunaungana kumuombea Mo Dewji apatikane akiwa salama. Mungu ibariki Tanzania. Amina.”

Simba wasitisha mazoezi

Wakati huo huo, kikosi cha Simba jana hakikuweza kuendelea na mazoezi ya kujiandaa na michezo yao ijayo ya Ligi Kuu Tanzania Bara, kutokana na taharuki iliyotokana na tukio hilo.

Meneja wa Simba, Abass Ally, alisema kutokana na tukio hilo, wameamua kusitisha programu yao ya mazoezi ambayo ilipaswa kufanyika jioni.

“Hatutaonekana watu wa kawaida kama imetokea hali hii, alafu tukaendelea na mazoezi, hivyo kwa siku ya leo tumeamua kupumzika ,” alisema.

Kujihusisha kwake na soka

Mo alishinda zabuni ya uwekezaji wa klabu ya Simba uliomwezesha kumiliki asilimia 49 za hisa, huku nyingine 51 katika mchakato wa mabadiliko uliochukua takribani miaka miwili.

Lakini kabla ya hapo, aliwahi kuwa mfadhili wa Simba na kuisaidia kufuzu robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kuibwaga Zamalek ya  Misri iliyokuwa bingwa mtetezi  hatua ya makundi.

Pia amewahi kuwa mwenyekiti wa kamati maalumu ya Saidia Taifa Stars Ishinde na kuiwezesha kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wanaocheza ligi za ndani (CHAN), michuano iliyofanyika nchini Ivory Coast mwaka 2008.

Shughuli nyingine aliyowahi kuifanya katika michezo, hususan soka, ni kuwa mmiliki wa klabu ya African Lyon kabla ya kuiuza kwa mfanyabiashara Rahim Zambunda.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles