27.2 C
Dar es Salaam
Friday, November 29, 2024

Contact us: [email protected]

Butiku: Kuna viashiria vya uvunjifu wa amani

Asema Taasisi ya Mwalimu Nyerere imekutana na viongozi wakuu wa Serikali, wa dini, vyama vya siasa kujadili njia ya kutatua hali hiyo

 

ANDREW MSECHU na LATH MBONEA – dar es salaam

MWENYEKITI wa Wakfu wa Mwalimu Nyerere (MNF), Joseph Butiku, amesema taasisi yake imebaini kuwapo viashiria vinavyoweza kusababisha uvunjifu wa amani, hivyo kuamua kukutana na viongozi wa vyama vya siasa kujadili hatua za kuchukua.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano maalumu baina ya MNF na viongozi wakuu wa vyama vya siasa Dar es Salaam jana, Butiku alisema kufuatia mwenendo wa mambo nchini, walibaini viashiria na dalili za mambo yanayoweza kuvunja misingi ya amani iliyojengwa, hivyo wakaona kuna sababu ya kukutana na viongozi wa kada zote ili kujadiliana nao.

“Kuhusu mambo yanayoweza kudhoofisha amani yetu huko mnakotoka mnayafahamu, ndiyo maana tumeona tuite mkutano huu wa vyama vya siasa ambao ni maalumu kwa ajili ya wenyeviti na makatibu, ili kutafakari pamoja hali yetu, hasa tukiangalia zaidi kwenye viashiria vya amani, je viko sawa katika miaka 56 ya uhuru wetu?” alisema.

Alisema mambo yanayotajwa kukwaza amani ni malalamiko ya kutoheshimiwa kwa utawala wa sheria na katiba na kubadili sheria kwa masilahi binafsi na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kutoheshimu sheria za uchaguzi.

Alitaja viashiria vingine ni kulegalega katika kusimamia mfumo wa demokrasia ya vyama vingi kwa kuzuiwa mikutano ya vyama vya siasa na kunyanyaswa kwa wanasiasa wa upinzani na kukosekana kwa uadilifu kwa viongozi wa umma ambao wanapindisha sheria kwa makusudi, wakiwemo wakuu wa mikoa na wilaya.

Viashiria vingine ni kulegalega katika kusimamia misingi ya katiba kwa kukiuka utoaji wa haki za msingi za raia ambazo ni ujenzi wa usawa, umoja, utu na heshima kwa kila mtu, kuibuka kwa woga na hofu ya kudadisi, kuhoji na kukosoa.

Butiku alisema hata viongozi wastaafu wamekuwa hawawezi tena kukemea au kukosoa Serikali kama alivyofanya Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere kwa masilahi ya ustawi wa taifa.

Alisema tangu kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu mwaka 2015, walikutana na viongozi wakuu wa Serikali ya Zanzibar, Serikali ya bara na kamati za ulinzi na usalama katika mikoa mbalimbali.

“Tumefanya hivyo ili kuona namna ya kudhibiti dalili na viashiria vinavyoweza kudhoofisha au kuvunja misingi ya amani,” alisema.

Butiku alisema iwapo viashiria hivyo vikipuuzwa na kufikia katika hatua ya ugonjwa kamili, nafasi ya kuleta maendeleo kama taifa itapotea.

Alisema Taasisi ya Mwalimu Nyerere imeendelea kuchukua hatua kadhaa baada ya kuona ipo haja ya kufanya mashauriano na kuhimiza umuhimu wa kuzingatia misingi ya tunu za taifa kama zilivyotajwa katika katiba ya nchi.

“Sisi kama wakfu tunasisitiza kwamba kuendelea kuwepo pamoja na kulindwa kwa misingi hiyo ndiyo siri ya amani na umoja wa taifa tangu kupata uhuru. Kinyume chake, kuvunjwa au kupuuzwa kwa misingi hii ni chanzo cha kutoweka kwa amani, umoja na utulivu wa nchi,” alisema.

Akitoa ufafanuzi, Butiku alisema katika maandalizi ya kikao cha jana waliendesha vikao vya kimya kimya na baadhi ya wanasiasa, viongozi wakuu wa kidini na viongozi wa Serikali waliopo madarakani na ambao walishatoka madarakani.

Alisema walizungumza nao kuhusu mtazamo wao juu ya taifa linavyokwenda, hasa kwa kuangalia eneo muhimu ambalo ni viashiria vya amani na umoja wa taifa.

“Tulizungumza na Makamu wa Rais na Spika wa Bunge la Zanzibar, kwa upande wa Tanzania Bara tulizungumza na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano na Waziri Mkuu.

“Pia tulipata nafasi ya kuonana na Rais, lakini yeye tulikwenda kumsalimu tu na baadaye tuliona upo umuhimu wa kuzungumza na wale tuliodhani ndio wenye watu, ambao ni viongozi wa kidini na wanasiasa.

“Tulifanya hivyo kwa sababu ukiondoa familia yako unakotoka kila mtu tuko katika kundi fulani. Yapo makundi makubwa ya viongozi, ipo Serikali, zipo taasisi za dini, wote tunakwenda makanisani na kwenye misikiti kumwomba Mungu asalimishe roho zetu.

“Hivyo tulifanya mazungumzo nao, ambapo tulikutana na makardinali, maaskofu masheikh na mufti kwa faragha,” alieleza Butiku.

Alisema walifanya hivyo wakielewa kuwa mfumo wa utawala wa nchi unaeleza wazi kuwa siasa yake itaendeshwa kwa mujibu wa vyama vingi.

Kutokana na hali hiyo, alisema walienda kwenye vyama ambavyo vinakwenda kwa wananchi na kuwaomba wapewe fursa ya kutawala na ndiko wanakotoka viongozi, hivyo waliongea nao wote kila mmoja kwa nafasi yake wengine kwa njia ya simu na baadhi ana kwa ana.

Butiku alisema katiba ya nchi ambayo ndiyo inayosimamia misingi ya haki, inatakiwa iheshimiwe kwa kuwa misingi iliyowekwa ndiyo mhimili wa taifa.

Alisema ni wajibu wa viongozi wote kutekeleza na kuishi misingi hiyo, kwa kujadili kwa kina misingi ya amani kwani mazungumzo na majadiliano ndiyo njia ya msingi ya kufikia maelewano.

 

KAULI YA MASHINJI

Katibu Mkuu wa Chadema, Vincent Mashinji alisema miongoni mwa mambo yanayokwaza kwa sasa ni ukandamizaji wa demokrasia, kuzuiwa kwa mikutano ya kisiasa na matumizi makubwa ya dola dhidi ya raia katika mambo yanayohusu siasa.

Alisema taifa kwa sasa linapitia katika wakati mgumu kwa kushuhudia utungwaji wa sheria ngumu za habari, sheria mbaya ya takwimu na kujaribu kubana uhuru wa kupashana habari kupitia sheria ngumu za mitandao.

Mashinji alisema kutokana na hali hiyo Watanzania wanahitaji kurejea katika misingi ya taifa kwa kuangalia ni namna gani mambo hayo yanaweza kurejeshwa na kuendela kudumisha amani ya nchi.

“Kuna mzunguko ambao unalinda amani dhidi ya vita na inapofikia hatua kunakuwa na watu wachoyo na wasiowapenda wenzao, tunahitaji kuwa na kiongozi anayeweza kusimama na kuwaweka pamoja watu. Amani hailindiwi kwa silaha wala majeshi bali inalindwa kwa kutenda na kusimamia haki,” alisema.

 

ZITTO KABWE

Kiongozi Mkuu wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe alisema Tanzania haina tofauti na nchi nyingine zinazoizunguka ambazo zina vurugu na hazina amani.

Alisema sababu zinazosababisha kukosekana amani huko zinaweza pia kusababisha amani kutoweka nchini.

“Waasisi wa nchi walihakikisha wanajenga misingi ya haki ambayo inaweza kusababisha watu kukaa chini na kuzungumza kunapotokea tofauti na kupata suluhisho.

“Huu ni mwanzo na kutokana na kuminywa kwa demokrasia, uhuru wa habari na demokrasia, misingi ya uwajibikaji imeanza kupotea, tunahitaji kufanya jambo kurejesha hali ya uwajibikaji,” alisema.

Alieleza kuwa kuna mtindo wa watu kutumbuliwa kama njia ya kuwafanya wawajibike, lakini kutumbua tu si jawabu la uwajibikaji, ila zinatakiwa kuchukuliwa hatua zaidi kwa wanaohujumu taifa ikiwemo waliojihusisha na ufisadi wa uchapishaji wa noti Benki Kuu, ulioripotiwa hivi karibuni, waliohusika katika kuhujumu elimu na wengine wanaofanana na hao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles