KAMPALA, Uganda
RAIS Yoweri Museveni, amesema kwamba amekasirika na kuumizwa na vifo visivyo vya lazima kwa wananchi wake ambavyo vinajitokeza mara kwa mara nchini humu, lakini akasema kwamba ana uhakika hatua za haraka zitachukuliwa ili kuwashughulikia wahalifu hao.
Rais Museveni alitoa kauli hiyo juzi wakati akiwahutubia maofisa usalama baada ya kukutana nao Ikulu ya nchi hii iliyopo mjini Entebbe.
Alisema wahalifu wamekuwa wakitumia mwanya wa asili ya upole walionao raia wa nchi hii na akawataka maofisa hao kuwa macho na watu hao.
“Wahalifu wanatumia faida ya upole walionao raia wa Uganda,” ila nawataka watu wote kuwa macho,” alisema Rais Museveni.
Katika mkutano huo ambao ni wa pili kulihutubia taifa ndani ya wiki moja, Rais Museveni, alisema kwamba mpaka sasa watuhumiwa 66 wameshatiwa mbaroni wakihusishwa na mauaji ya viongozi wa dini, watu wenye majina makubwa na hata watu wengine wa kawaida.
Hotoba hiyo ya Rais Museveni imekuja zikiwa ni siku chache, baada ya Kamanda wa zamani wa Polisi wa Wilaya ya Buyende, Muhammad Kirumira, kuuawa na watu waliokuwa wakitumia pikipiki, ikiwa ni baada ya kutokea mauaji mengine ya Mbunge wa Jimbo la Arua, Ibrahim Abiriga, Mkuu wa Polisi, Andrew Felix Kaweesi, Meja Muhammad Kiggundu na Mwanasheria wa Serikali, Joan Kagezi.
Mbali na vigogo hao pia Mhasibu, Susan Magara na wanawake wengine katika miji ya Entebbe, Nansana na Masaka na walipoteza maisha katika mauaji tofauti tofauti.
Akizungumzia vifo hivyo, Rais Museveni, alisema kwamba wengi wa wahusika wameshafikishwa mahakamani na kuhukumiwa huku wengine wakiwa wanaendelea kusakwa.