Na THERESIA GASPER-DAR ES SALAAM
Timu ya Azam FC, inatarajia kucheza tena mchezo mwingine wa kirafiki dhidi ya Reha FC kesho katika Uwanja wa Chamazi Dar es Salaam.
Huo utakuwa ni mchezo wa tatu tangu kusimama kwa Ligi Kuu Tanzania Bara, kupisha mchezo wa timu ya Taifa ambao wanacheza dhidi ya Uganda.
Katika mchezo wa awali Azam walicheza dhidi ya Transit Camp FC na kuambulia kipigo cha mabao 2-1, katika Uwanja wa Uhuru Dar es Salaam, huku wa pili dhidi ya Arusha United walitoka suluhu ya kutofungana kwenye dimba lao la nyumbani.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Meneja wa timu hiyo, Philip Alando, alisema kocha wao, Hans van der Pluijm, anaendelea kuwapima nyota wake kabla ya ligi kuendelea.
“Mechi itachezwa saa mbili asubuhi katika uwanja wetu wa Azam Complex, hii itakuwa ni mechi ya tatu baada ya kucheza mbili tayari kwani benchi la ufundi linataka kukiweka sawa kikosi kabla ya ligi kuendelea ukizingatia kwa sasa imekuwa na ushindani mkubwa,” alisema.
Alisema mechi hizo ni maandalizi ya mchezo unaowakabili mbele yao dhidi ya Mwadui FC, unaotarajiwa kupigwa Septemba 15, mwaka huu mjini Shinyanga.
Azam FC wanashika nafasi pili katika msimamo wa ligi wakijikusanyia pointi sita kati ya mechi mbili walizocheza wakiwa sawa na Simba, Mtibwa Sugar na Stand United, wakitofautiana kwa idadi ya mabao ya kufunga na kufungwa.