32.1 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

JPM ATAJA SABABU KUMNG’OA BOSI TAKUKURU


Na ANDREW MSECHU

RAIS Dk. John Magufuli ameeleza sababu za kumtumbua aliyekuwa Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Valentino Mlowola juzi.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara kwenye viwanja vya Chuo cha Ualimu Tarime jana, Rais Magufuli alisema alipata tabu baada ya kufikiria kwa zaidi ya saa tano kufikia uamuzi huo, hadi ilipofika saa 11 alfajiri kuamkia Alhamisi Septemba 6 mwaka huu.

Rais Magufuli ambaye anaendelea na ziara yake katika mikoa ya Kanda ya Ziwa aliita sababu mojawapo za kumwondoa Mlowola ambaye sasa amemteuliwa kuwa balozi ni kutoshughulikia vitendo vya rushwa mkoani Mara.

“Nimekwenda pale Musoma mtu amenunua Musoma Hoteli kwa miaka kumi hashughuliki, anapewa kazi za kandarasi hamalizi. Waziri Mkuu alipita hapa Mara akatoa maagizo kwa Takukuru kwamba washughulike. Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Mara alilishughulikia na akamaliza tangu mwezi wa nne na akapeleka faili makao makuu lakini hadi leo mwezi wa tisa makao makuu bado hawajalishughulikia,” alisema.

Alisema makao makuu kulikalia faili hilo  ndiyo sababu iliyomfanya aone kuwa mkurugenzi huyo mkuu wa Takukuru lazima akae pembeni akafanye kazi nyingine.

Pamoja na hilo Rais Magufuli alisema pia aliangalia makosa yake mengine aliyokuwa akifikishiwa hivyo kuthibitisha uamuzi wake wa kumweka kando.

Katika hilo, aliwataka viongozi wote anaowateua wakatatue shida za wanyonge na wasioweza kufanya hivyo waandike barua au waache kazi, wasitake kazi ambazo hawaziwezi, kwa kuwa wanalipwa mshahara, wana magari lakini hawataki kuwashughulikia wananchi masikini, suala ambalo kwa zama zake hizi halivumiliki.

Alisema yeye mwenyewe kwa kipindi hichi alitakiwa awe nchini China kwa ajili ya mkutano wa marais wa Afrika lakini aliamua afanye ziara hiyo ya kuwasikiliza wananchi ambao ndio anaotakiwa kuwahudumia.

“Inawezekana nilifanya makosa kutokwenda nje, nimeamua kuchagua kutembea Tanzania kwa wale wanaotarajia kuniona naenda nje watasubiri sana. Niwaambie tu kwamba huko nje kila mahali ninapafahamu lakini watanzania wana shida nyingi mno hivyo ni lazima nizunguke kutatua matatizo yao, niwaombe viongozi wenzangu wawe wanawatembelea wananchi ili kuwatatulia shida zao,” alisema.

Alisema kuwa viongozi na watumishi wa Mamlaka ya Mapato (TRA) na wengine hawakupelekwa mikoani kwa ajili ya kujitajirisha na kuwataka watambue jukumu lao kuu ni kukusanya kodi akiwaomba wananchi pia kuwa tayari kulipa kodi kwa ajili ya kuisaidia Serikali kutekeleza majukumu yake.

Rais Magufuli aliendeela kuwalaumu wabunge wa upinzani ambao wamekuwa wakikataa kupitisha bajeti Mapato na Matumizi ya Serikali akieleza kuwa anawaona maadui wa maendeleo ya wananchi.

“Wapo wanaokataa kupitisha bajeti, wenzao wakisema ndiyo wao wanasema hapana. Ninawashukuru wale waliosema ndiyo kwa sababu iwapo wote wangesema hapana leo hizi barabara zisingekuwepo, japokuwa hata kura ya hapana ni demokrasia lakini siku nyingine wajifunze, sasa unakataa bajeti halafu unaniomba maji, unahoji vipi kitu ambacho ulikikataa?” alihoji.

Aliwaomba Watanzania kuilinda amani kwa gharama zote kwa kuwa ni kitu muhimu katika mambo yote, huku akivipongeza vyombo vya ulinzi nchini kwa kuendelea kulinda amani.

MATAJIRI JEURI AWAONYA

Aidha Rais Magufuli alisema hatawavumilia matajiri ambao wamekuwa wakidhani kwamba wanaweza kufanya lolote na kwamba katika zama hizi, lazima watambue kwamba wanaweza kufanywa lolote tofauti na walivyozoea siku zilizopita.

“Mimi nitaendelea kuongea ukweli hata kama mkiamua kunifukuza CCM nitakapomaliza muda wangu lakini lazima ifike kipindi tubadilike ,” alisema.

“Mimi ninataka kubadilisha haya mambo, nataka mwenye cheo amuheshimu asiye na cheo na asiye na cheo amuheshimu mwenye cheo watu wote wako sawa mbele ya macho ya Mungu, hiyo ndiyo Tanzania ninayoitaka,”  aliswema.

Alisema kwa sasa anapigania  ukombozi wa kiuchumi baada ya baba Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere kuleta ukombozi dhidi ya ukoloni.

 

MWANAFUNZI ‘JASIRI’ AIBUKA KWENYE ZIARA YAKE

Awali, akiwa katika Kijiji cha Nyamongo, mwanafunzi Monica Dungu wa kidato cha tano Shule ya Sekondari ya Ingwe mkoani Mara alimuorodheshea  changamoto wanazokumbana nazo wanafunzi wa shule hiyo.

Rais Magufuli alikuwa akizungumza na wananchi wa Nyamongo aliposimama kwa dharura wakati akielekea Tarime.

Mwanafunzi huyo ‘jasiri’ ambaye alitumia nafasi hiyo kuorodhesha changamoto kadhaa ikiwamo ukosefu wa maabara, mabweni, maktaba, upungufu wa walimu, vyumba vya madarasa, vitanda, vitabu na nishati,  alianza kwa kumuhoji Rais Magufuli sababu za kutozungumzia suala la elimu katika hotuba yake jambo lililomfanya Rais aongoze harambee ya kuchangisha fedha.

Harambee hiyo ilifanikisha kuchangisha kiasi cha zaidi ya Sh  milioni 24 kwa ajili ya kutatua changamoto za shule hiyo.

Awali alipokabidhiwa kipaza sauti, Monica alianza kwa kusema kuwa shule hiyo inakumbana na changamoto nyingi ikiwamo upungufu wa walimu pamoja na vitabu.

“Shule yetu imeanza mwezi wa saba tarehe 30 kama High School lakini shule yetu ina upungufu wa walimu na vitabu kwa o-level na advanced level,” alisema mwanafunzi huyo.

Pia alieleza kuwa wana uhaba wa mabweni, hali inayosababisha wanafunzi kuchangia vitanda.

“Tuna bweni moja ambalo ‘tunashea’ wanafunzi wa o-level na advanced wa kike, katika bweni hilo tuna vitanda vichache ambapo inasababisha kitanda cha futi mbili na nusu tunalala wanafunzi watatu,” alisema.

Pia ametaja mambo mengine kuwa ni upungufu wa vyumba vya madarasa, viti, maji, umeme na ukosefu wa gari la wagonjwa.

“Tunakosa vitabu rejea kwa kidato cha tano na cha sita na inatufanya kutumia kitabu kimoja kwa kuchangia na vitabu hivi shuleni havipo. Mheshimiwa Rais tunatoka katika familia maskini tunaomba ututatulie tatizo hili,” alisema.

Baada ya kusikiliza kero hizo, Rais Magufuli aliwataka viongozi wakiwamo wabunge, mawaziri na madiwani waliokuwapo katika msafara huo kuchangia fedha kwa ajili ya kutatua changamoto hizo.

“Sasa hivi nataka uchangie hapa ili kusudi na mimi nichangie na mawaziri wangu nitawachangisha hapahapa,” alimwambia mbunge wa Tarime Vijijini (Chadema), John Heche ambaye alikuwa ni miongoni  mwa waliochangia Sh. 500,000.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles