Na waandishi wetu |
RAIS Dk. John Magufuli amesema uongozi katika awamu yake ni msalaba, kwahiyo yeyote anayepewa nafasi awe tayari kuwajibika wakati wowote.
Akizungumza katika utiaji saini wa ujenzi wa meli mpya, chelezo cha kisasa na ukarabati wa meli mbili jijini Mwanza jana, Rais Magufuli alisema ni wajibu wa viongozi kuwa mbele kuwasaidia watu masikini, kujibu hoja zao na matatizo yao badala ya kujijibu wao na matatizo yao, kwa kuwa Watanzania wote wanawategemea kusimamia utatuzi wa matatizo yao.
“Ndiyo maana nimekuwa nikizungumza siku zote kwamba uongozi ni msalaba, na hasa uongozi wa awamu yangu ni msalaba, nasema kwa dhati, ukiwa kiongozi ukae mguu upande mguu sawa kwa sababu hata mimi mguu mwingine uko upande mwingine sawa, ni lazima tutimize malengo ya wananchi,” alisema.
Rais Magufuli alisema anashangazwa na hatua iliyofikiwa kwa kutia saini ujenzi wa meli mpya katika Ziwa Victoria, suala lililoshindikana kwa zaidi ya miaka 22 iliyopita na kwamba anajisikia faraja kushuhudia tukio hilo ambalo awali lilishindikana pamoja na Serikali zilizopita kutoa ahadi mara kadhaa.
“Tangu kuzama kwa meli ya MV Bukoba karibu miaka 22 iliyopita, Serikali iliahidi kutengeneza meli mpya, lakini haikuwezekana kutokana na sababu mbalimbali kwa miaka yote hiyo, hivyo kufanya usafiri katika Ziwa Victoria kuwa wa shida na matatizo, hasa baada ya meli nyingine kubwa za MV Victoria na MV Butiama pia kusitisha huduma kutokana na matatizo ya kiufundi,” alisema.
Alisema kutokana na matatizo hayo, Ilani ya CCM ya mwaka 2015 ilitoa ahadi ya kutekeleza ujenzi wa meli mpya kubwa ya kisasa katika Ziwa Victoria iwapo chama hicho kitapewa ridhaa ya kuongoza nchi, suala ambalo lilionekana kuwa gumu.
Rais Magufuli alisema alipokuwa Mwanza na wabunge na madiwani walizungumza hilo katika kampeni, lakini hakuwa na uhakika kwamba litafanikiwa kwa kuwa alijiuliza iwapo wenzake waliopita hawakuweza kuna kitu gani kinachowafanya washindwe.
Kwa habari zaidi jipatie nakala yako ya gazeti la MTANZANIA.