Na ELIYA MBONEA
Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha, Ramadhani Ng’anzi ametembelea mazoezi ya timu ya Taekwondo na huko amejionea sehemu ya mazoezi (Gym), Onyesho la Taekwondo pamoja na kusikiliza changamoto mbalimbali zinazoikabili timu hiyo.
Kamanda huyo pia amewapongeza wachezaji wa timu hiyo walioshiriki michezo ya majeshi ya polisi kwa Nchi za Afrika Mashariki na Kati (EAPCCO) yaliyofanyika Dar es Salaam ambapo walipata medali mbili ya Shaba na Fedha.
‘‘Mfanye mazoezi ya kutosha kwa kuwa lengo la mchezo huu ni kujenga ukakamavu na kujilinda name kuanzia wiki ijayo nitajumuika nanyi, mwisho wa siku na mimi nivae mikanda kama yenu,’’ alisema Kamanda Ng’anzi.
Baada ya kuahidi kujumuika nao kwenye mazoezi huku akiahidi kufanyia kazi changamoto za vifaa na muda wa mazoezi kutokana na kuingiliana na muda wa kazi.
“Nitakaa na viongozi wenzangu kuona jinsi ya kutatua changamoto hizi kwa uwa zipo ndani ya uwezo wetu,” alisema RPC Ng’anzi.
Naye kocha wa timu hiyo, Shija Makoye alisema timu hiyo ina wachezaji 15 wanaojifunza mbinu mbalimbali za kujijengea ukakamavu na uwezo binafsi wa kujilinda pindi watakapokabiliwa na adui.