27.1 C
Dar es Salaam
Thursday, January 2, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

MAKONDA ATUA KANISANI KUZUIA MNADA WA MAKONTENA

  • Asema atakayenunua atalaaniwa na Mungu, arusha kombora TRA
  • Ahoji jina lake, asema kama hawalipendi waliondoe  kwenye makontena

Na MWANDISHI WETU, NGARA


SIKU moja baada ya makontena 20 yaliyo bandarini kwa jina la Paul Makonda, ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salam kufanyiwa mnada na kukosa wateja, amefanya ibada  akiomba yakose wateja.

Juzi, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), ilifanya mnada makontena hayo katika eneo la bandari kavu ya Malawi Cargo, lakini yalikosa wanunuzi baada ya waliojitokeza kushindwa kufika bei iliyotakiwa.

Jana Makonda alikwenda katika Kanisa la Anglikana wilayani Ngara, Mkoani Kagera ambako iliendeshwa ibada maalumu ya kuzuia mnada wa makotenda yenye samani za walimu wa Mkoa wa Dar es Salaam.

Makonda ambaye yupo kwenye msiba wa mama mkubwa wa mkewe, alishiriki ibada hiyo na aliwaambiwa waumini wa kanisa hilo kuwa amesali pamoja nao kwa sababu anaamini Mungu ndiye aliyempa makotenda hayo kwa ajili ya walimu wa Mkoa wake.

Alionya kuwa atakayenunua makontena hayo atalaaniwa yeye na uzao wake wote kwa sababu vya madhabahuni havichezewi.

“Nimeamua kufanya ibada hii kuhakikisha makontena hayo hayapati wateja kwani naamini Mungu alinipa kwa ajili ya walimu wa Dar es Salaam, wanaofanya kazi katika mazingira magumu ikiwa ni jitihada zangu binafsi kuboresha mazingira yao na ni sehemu ya kumuunga mkono Rais John Magufuli.

“Rais alitambua umuhimu wa elimu na ndiyo maana kama msaidizi wake sikuona sababu ya kukaa kimya wakati mazingira ya walimu si rafiki na kusubiri kuwalaumu walimu pale watoto wanapofeli bila kufanyia kazi changamoto zao,” alisema Makonda.

Alisema Serikali ya Awamu ya Tano iliamua kutoa elimu bure na kwamba kwa sasa kila mwezi inatumia Sh bilioni 20 kusaidia sekta ya elimu hivyo aliamua kutumia nafasi yake na uhusiano wake binafsi kusaidia juhudi hizo.

“Kama mtakumbuka nilizindua operesheni ya kuinua na kuondoa changamoto kwenye sekta ya elimu ikiwemo ujenzi wa madarasa, ofisi za walimu na fedha hizi zilichangwa na Watanzania, kazi hii ilifanywa na Watanzania wenyewe mimi kama kiongozi nilitoa dira.

“Niliomba msaada wa vifaa kutoka kwa Watanzania waliopo nje ya nchi ili waweze kunisaidia samani za ofisi na madarasa, vifaa hivi sipeleki nyumbani kwangu, simpelekei mama yangu.

“Bali vinaenda kusaidia walimu na wanafunzi ambao wanajitolea kufanya kazi usiku na mchana katika mazingira magumu ili kuwasaidia watoto masikini.

“Cha kushangaza leo vinapigwa mnada ili kutoza kodi kwa kuwa tu makontena yameandikwa Makonda basi kama jina langu hawalipendi watafakari mzigo alionao mwalimu wa Dar es Salaam anayegombea kiti na mwanafunzi anayekaa chini.

“Inasikitisha sana leo TRA inapiga simu kuomba shule binafsi zikanunue vifaa vilivyoletwa kwa msaada na Watanzania kwa ajili ya Watanzania wenzao.

“Ninachoweza kusema tu waliopewa madaraka wawe na hofu ya Mungu, mimi sikalii viti hivyo hata kama msingi wake ni chuki mchukieni Makonda lakini si walimu,” alisema Makonda.

Alisema samani hizo za walimu wa Mkoa wa Dar es Salaam zinazouzwa na TRA ikumbukwe ni msaada alioutafuta kutoka kwa Watanzania waishio Marekani ili kuboresha mazingira ya walimu.

“Watanzania waishio Marekani wakajitolea kama mchango wao kwa kampeni ya Makonda ya ujenzi wa Ofisi za Walimu, TRA imefikia uamuzi huo kwa Makonda kushindwa kulipia kodi ya Sh bilioni 1.2 kama mtu binafsi wakati furniture hizo ni msaada kwa walimu wa shule za serikali,” alisisitiza.

Akizungumza na MTANZANIA jana akiwa Wilayani Ngara, Makonda alisema amelaaniwa mtu yule atakayenunua thamani hizo za walimu.

“Kwa sababu Mungu ndiye aliyewawezesha watu wakakubali kujitolea, nakuhakikishia atakayenunua hivi vifaa vya walimu amelaaniwa yeye na uzao wake.

“Na kamwe hatafanikiwa katika maisha yake. Nayasema haya nikiwa na uhakika kwani vya madhabahuni havichezewi.

“Hili wazo la kutafuta msaada huu, aliweka Mungu ndani ya moyo wangu juu ya ujenzi wa ofisi za walimu kama sehemu ya kuboresha mazingira yao. Kwa utukufu wake Mungu akaandaa watu kuchangia tena kutoka nje na ndani ya nchi na utukufu wake umejidhihirisha.

“Kwa Watanzania kuchagia wakiwemo JKT kujitolea kujenga bure, mabenki wakanunua safuji na viwanda vimetoa mabati, nondo huku wengine wakijitolea masinki, mabomba na taa.

“Nchi ya China nao wamejenga ofisi na ndugu zetu kutoka Marekani wakaleta samani za walimu makontena  zaidi ya 20.  Wananchi na vyombo vya habari wakajitolea na kuendelea kuhamasisha huku walimu wakichanga kama sehemu ya kujikomboa, leo TRA wameamua kuuza  samani za walimu kwa wamiliki wa kumbi za starehe ili walimu waendelee kugombania madawati na vyoo na wanafunzi .

“Mimi Paul Makonda nimefanya kwa sehemu yangu kilichobaki ni mwenye wazo atasimama siku moja kujitetea,”alisema.

Kutokaa na hali hiyo MTANZANI, ilimtafuta Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa TRA, Richard Kayombo alisema ndiyo anarudi kutoka safarini na kwamba hajafuatilia namna mnada ulivyokwenda.

“Ndiyo narudi kutoka safarini, ngoja nifuatilie kwanza halafu nitakwambia ilivyokuwa,” alisema Kayombo.

HISTORIA YA MAKONTENA

Mei 12 mwaka huu, tangazo la TRA lilichapwa kwenye gazeti la Serikali la Daily News, likiwataka wamiliki wa mali zilizokaa bandarini kwa zaidi ya siku 90 kujitokeza kuzilipia.

Katika tangazo hilo, lililokuwa na orodha ya makontena zaidi ya 800, jina la Paul Makonda lilijitokeza mara 20 akiwa mpokeaji wa makontena 20 yaliyopo katika bandari kavu ya DICD yakiwa na bidhaa kadhaa kama samani.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles