28.8 C
Dar es Salaam
Thursday, December 12, 2024

Contact us: [email protected]

MAKALA: SERIKALI LAWAMANI UFUNDISHAJI ELIMU MAALUM

Na MAREGESI PAUL, ALIYEKUWA SONGE


SERIKALI imekuwa na mkakati maalum wa kuhakikisha inatoa elimu bora kuanzia shule za awali hadi vyuo vikuu.

Chini ya mkakati huo, imekuwa ikiboresha mitaala ya elimu huku ikihakikisha walimu na vitendea kazi shuleni, vinakuwapo ili elimu inayotolewa iende na wakati na kuwafanya wahitimu kuwa na uwezo wa kushindana katika soko la ajira la kimataifa.

Pamoja na mikakati hiyo, mazingira ya utolewaji wa elimu maalumu inayohusisha wanafunzi wasioona na wenye uoni hafifu katika Manispaa ya Songea, Mkoa wa Ruvuma, yanawakatisha tamaa wanafunzi na walimu kwa kuwa elimu hiyo inatolewa katika mazingira yanayokatisha tamaa.

Katika mahojiano na mwandishi wa makala haya yaliyofanyika hivi karibuni katika manispaa hiyo, walimu, wanafunzi na viongozi wa idara ya elimu katika manispaa hiyo, wanaeleza kwa masikitiko jinsi mazingira ya elimu hiyo yanavyotolewa.

Mmoja wa walimu hao ambaye ni Mkuu wa Idara ya Wanafunzi Wenye Ulemavu katika Shule ya Msingi Luhira, Humange Nickson, anasema shuleni hapo kuna wanafunzi wenye uoni hafifu 44 ambao wanaishi shuleni hapo wanaofundishwa na walimu sita wenye elimu maalumu.

Katika maelezo yake, Mwalimu Nickson anasema wanafunzi wenye uoni hafifu na wenzao wasioona, wanasoma katika mazingira magumu kwa kuwa Serikali inaonekana kutoipa kipaumbele elimu maalumu.

“Hapa tunao watoto 44 wenye uoni hafifu na pia tunao wenye ulemavu wa ngozi 13 ambao wote wanaishi hapa shuleni kwa sababu shule yetu inafundisha elimu maalum.

“Watoto hao wenye mahitaji maalumu wakiwamo wenye uoni hafifu, wanahudumiwa na Serikali ambapo kila mwezi zinaletwa Sh milioni 1.8.

“Fedha hizo unaweza ukaona kama ni nyingi, lakini ukweli ni kwamba hazitoshi kabisa kwani tunazitumia kulipa mishahara ya watumishi, mlinzi pamoja na wapishi.

“Kutokana na ufinyu wa bajeti hiyo, wanafunzi wanalazimika kula ugali na maharage kila siku ila mara moja moja sana wanabadilisha mlo,” anasema Mwalimu Nickson.

Akizungumzia vifaa vya ufundishaji, anasema vipo ila haviletwi kwa wakati na kwamba tatizo kubwa wanalokabiliana nalo ni upatikanaji wa lenzi za kukuzia maandishi.

“Kuna mambo mengine ukiyasikia huwezi kuamini, kwa mfano, kwa upande wa wanafunzi wenye uoni hafifu, wao ukubwa wa matatizo yao unatofautiana, lakini tukiomba lenzi serikalini kwa ajili ya kukuzia maandishi, tunaletewa lenzi zinazofanana utadhani matatizo ya watoto yanafanana.

“Hata wakati wa mitihani, mitihani ya watoto hao inapochapishwa, inakuja ikiwa katika maandishi yenye ukubwa unaofanana wakati matatizo yao ni tofauti.

“Kwa kuwa watoto hawa wana mahitaji maalum ya usomaji, mwaka jana tuliomba meza maalum za kusomea, lakini hadi sasa hatujaletewa.

“Kwa ujumla, matatizo ni mengi ambayo yanahitaji kutatuliwa na Serikali kama kweli imedhamiria kulisaidia kundi hili maalum,” anasema Mwalimu Nickson.

Kuhusu unyanyapaa, anasema haupo kwa sababu wamekuwa wakiwaelimisha wanafunzi wao umuhimu wa kupendana na kuheshimiana.

Wakati mwalimu huyo akisema hayo, walimu wa elimu maalum katika Shule ya Sekondari ya Wavulana Songea (Songea Boys), nao wanasema Serikali inaonekana kuisahau elimu maalum licha ya jitihada zake za kutaka kuiimarisha.

Mmoja wa walimu hao, Wenston Ngewe, anasema utaratibu wa kuwataka walimu wa elimu maalumu wafundishe na wanafunzi wengine, unawafanya wakose muda wa kuwafuatilia walengwa ambao wanahitaji ukaribu katika ufundishaji.

“Mimi binafsi nimesomea elimu maalumu, lakini mimi na wenzangu wenye taaluma maalumu, tunapangiwa majukumu mengine na tunalazimika kufundisha na madarasa yasiyokuwa na wanafunzi wanaohitaji elimu maalumu, jambo ambalo linatufanya tushindwe hata kuwafuatilia wanafunzi husika.

“Yaani, kama unafundisha mwanafunzi mwenye uoni hafifu au asiyeona kabisa, lazima utumie muda wako mwingi kumfundisha na baadaye kumfuatilia kwa karibu hadi utakapoona ameelewa.

“Lakini, utaratibu wetu wa kufundisha masomo mengi, unatufanya tushindwe kufanya kazi vizuri kulingana na taaluma yetu.

“Kwa hiyo, lazima Serikali ikubali kubadilika kwani isipokuwa makini, wanafunzi wetu watashindwa kuendelea na masomo kwa sababu mazingira ya utolewaji wa elimu maalum ni magumu kwani hatuna hata ramani mguso kwa ajili ya wasioona na wenye uoni hafifu,” anasema Mwalimu Ngewe.

Naye Mwalimu Geofrey Mwaikunda wa shuleni hapo, anasema shule hiyo ina wanafunzi 15 wenye uoni hafifu wanaofundishwa na walimu 13 wenye mafunzo ya elimu maalum.

“Hapa kwetu wanafunzi maalum tunawapata kutoka mikoa yote ya nyanda za juu kusini na wote wako ‘boarding’.

“Pamoja na taaluma tuliyonayo, hatujui ukubwa wa matatizo ya wanafunzi kwa sababu hakuna nyaraka zinazoonyesha matatizo yao yalivyo ili tuweze kuwafundisha kulingana na hali zao.

“Kwa hiyo, tunachokifanya darasani ni kuwaweka kwenye viti vya mbele wale wenye uoni hafifu ili waweze kuwa jirani na ubao.

“Pamoja na kwamba Serikali ndiyo inayogharamia elimu maalum, watoto hawana lenzi maalum za kukuzia maandishi, hawana vitabu maalum vya masomo yao, hawana mashine za kutosha za nukta nundu na pia miundombinu ya shule siyo rafiki kwao.

“Kutokana na mazingira hayo, hata ufaulu wao ni mdogo kwa sababu mazingira ya ufundishwaji na ujifunzaji hayaridhishi.

“Kwa hiyo, kama Serikali inataka watoto wenye mahitaji maalumu wasome vizuri, lazima ikubali kuwekeza na pia ikubali kutupunguzia majukumu walimu wenye elimu maalumu ili tuwe na muda wa kutosha wa kuwasaidia wanafunzi wetu,” anasema Mwalimu Mwaikunda.

Kwa upande wake, Kaimu wa Kaimu Mkuu wa Shule hiyo ambaye pia ni Katibu wa Idara ya Taaluma, Mwalimu Oreda Ng’olo, kama walivyosema wenzake, naye anasema yanahitajika mageuzi ya haraka ili kuboresha utolewaji wa elimu maalum.

“Kwa ujumla, mazingira ya ufundishaji ni magumu na walimu wanalazimika kutoa notsi mapema ili wenye uoni hafifu, wasaidiwe na wenzao kwa muda watakaokuwa wakiupata.

“Kuhusu masuala ya unyanyapaa, hayapo kwani wanafunzi wote wanapendana na wanashirikiana katika masuala mbalimbali.

“Ila tatizo tulilonalo hapa ni kwamba, wazazi na walezi wenye watoto wenye uoni hafifu na wasioona, hawawafuatilii watoto wao ili kujua wanaendeleaje na wakati mwingine tunapofunga baadhi yao wanabaki shuleni kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne na hao wanajiita wagumu,” anasema Mwalimu Ng’olo.

WANAFUNZI WANASEMAJE

Kwa upande wao, wanafunzi wa shule hizo zinazotoa elimu maalum, wanasema Serikali inachangia kwa kiasi kikubwa wao kushindwa kufanya vizuri katika masomo yao kwa kuwa inaonekana imewatelekeza.

Mmoja wanafunzi hao anayesoma darasa la sita katika Shule ya Msingi Luhira, Irene Milinga, anasema amekuwa akisoma kwa shida kwa kuwa amekuwa akitokwa machozi kila wakati kutokana na kutokuwa na lenzi maalum za kukuzia maandishi.

“Kwa kifupi mazingira ya usomaji siyo mazuri kwa sababu hatuna vitabu, hatuna lenzi maalum na pia ulaji wetu ni wa shida kwa sababu tunakula chakula cha aina moja kila siku,” anasema Irene na kuungwa mkono na mwenzake Said Kalonga anayesoma darasa la tano.

Wakati Irene na Kalonga wakisema hayo, wenzao walioko Songea Boys, Tafiti Regnas wa kidato cha nne na Hamza Masoud wa kidato cha tatu, wanasema kwa nyakati tofauti, kwamba wanashindwa kufanya vizuri darasani kutokana na mazingira mabovu ya usomaji.

Wanafunzi hao ambao wanasema wana uwezo wa kufika chuo kikuu, wanasema wanaweza wasifanikiwe katika malengo yao kwa sababu shule yao haina vitabu vya kujisomea, hawana mashine za kutosha za nukta nundu na pia walimu wao hawawafuatilii kimasomo kutokana na sababu ambazo hawazijui.

Kutokana na hali hiyo, wanasema kuna haja kwa Serikali kuwekeza zaidi katika elimu maalum kwa sababu wasipofaulu, uwezekano wa kumudu kuendesha maisha yao ni mdogo.

OFISA ELIMU, ELIMU MAALUM

Kwa upande wake, Ofisa Elimu, Elimu Maalum Manispaa ya Songea, Rehema Nyagawa, anasema pamoja na nia njema ya Serikali ya kuwapa elimu watoto wenye mahitaji maalum, bado kuna changamoto nyingi zinazotakiwa kutatuliwa.

“Kwa ujumla, bado kuna changamoto nyingi zinazotakiwa kutatuliwa na Serikali kwani walimu wenye elimu maalum ni wachache na vitendea kazi shuleni havitoshi.

“Pamoja na hayo, nashauri Serikali irudishe utaratibu wa kutoa nauli za watoto hao kila wanapotoka kwao kuja shuleni na kutoka shuleni kwenda kwao kwa sababu baadhi yao wanaacha masomo kutokana na wazazi wao kukosa nauli.

“Katika suala la chakula hasa pale Luhira Shule ya Msingi hali ni mbaya kwa sababu fedha tunazowapa hazitoshi na wanafunzi wanalazimika kula mlo mmoja kila siku.

“Tatizo jingine tulilonalo ni walimu wenye elimu maalum kufanya kazi nyingi tofauti na walizosomea kama ilivyo kwangu ambapo kuna wakati nafanya majukumu tofauti na niliyosomea.

“Nasema hivyo kwa sababu mwanafunzi anayehitaji elimu maalumu wakiwamo wenye uoni hafifu na wasioona, wanatakiwa kufundishwa na kufuatiliwa kwa ukaribu zaidi.

“Kwa hiyo, unapokuwa na walimu ambao unawapa majukumu mengi zaidi ya wanayotakiwa kuyafanya, uzitegemee mafanikio zaidi,” anasema Nyagawa.

MKURUGENZI WA MANISPAA

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Manispaa ya Songea, Tina Sekambo, anasema changamoto zinazoikabili elimu maalum anazifahamu na zitatatuliwa awamu kwa awamu.

“Kuhusu tatizo la ukosefu wa vitabu na upungufu wa walimu, hilo litashughulikiwa na Serikali kwa kufuata taratibu zitakazowekwa kwa sababu changamoto hizo haziwezi kutatauliwa kwa mara moja,” anasema Sekambo.

 

 

 

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles