Na DERICK MILTON-BUSEGA
WAZIRI wa Nishati, Dk. Merdad Kalemani, amewataka wakandarasi wote nchini wanaotekeleza mradi wa Umeme Vijijini Awamu ya Tatu (REA III), kuhakikisha wanaweka umeme katika nyumba zote zikiwamo za tembe huku akipiga marufuku kurukwa.
Akizungumza wakati akiwasha umeme katika vijiji vya Lukungu, Nyakaboja na Bukabile vilivyoko Wilaya ya Busega, Simiyu, alisema wamekuwa wakipata taarifa za wakandarasi waliopewa kazi ya kutekeleza mradi huo kuwa wamekuwa wakiziruka nyumba hizo kwa madai hazifai kupata huduma hiyo.
Aliwataka wakandarasi hao kuhakikisha wanapeleka umeme katika kila kijiji na kila kitongoji ili wananchi waweze kuondokana na adha kubwa wanayokumbana nayo ya kukosa nishati ya umeme.
“Nimepata taarifa kuwa wananchi wenye nyumba za tembe wanarukwa, maagizo yangu ni marufuku kuruka nyumba ya tembe, tena nyumba hizo zipewe kipaumbele cha kwanza kupata umeme na hakuna kuruka kijiji, kitongoji au nyumba yoyote,” alisema Kalemani.
Alisema Serikali haitaongeza muda, siku wala saa kwa mkandarasi yeyote atakayeshindwa kutekeleza mradi huo kwa muda mwafaka waliopewa na Tanesco na aliwataka kutekeleza mradi huo hadi kukamilika kwake kwa muda mwafaka.
Alisema mkandarasi White City anayetekeleza mradi huo Simiyu kasi yake ni ndogo na alimtaka kuongeza kasi zaidi ili kuhakikisha vijiji 152 mkoani humo vinapata umeme.
Alisema katika Wilaya ya Busega kupitia mradi huo vijiji vyote 54 vilivyoko wilayani humo vitapata umeme na aliwataka wananchi kuhakikisha wanalipia gharama ya Sh 27,000 ili kupatiwa huduma hiyo.
Pia alizitaka halmashauri zote nchini kuhakikisha wanafunga mfumo wa umeme katika taasisi za umma zikiwemo shule na vituo vya kutolea huduma za afya.
“Wakati sisi tukihangaika kuleta umeme kwa kila mwananchi, niwatake wakurugenzi wa halmashauri pamoja na madiwani kupitia vikao vyao, watenge bajeti kuhakikisha taasisi zote za umma zinafungiwa mfumo mzima wa umeme kwa ndani,” alisema Kalemani.
Awali, Mbunge wa Busega, Dk. Rafel Chegeni, alisema bado kuna baadhi ya vitongoji na vijiji vimerukwa na mkandarasi anayetekeleza mradi huo.
Dk. Chegeni alisema kilio kikubwa cha wananchi wa jimbo hilo ni ukosefu wa umeme na alimwomba Kalemani kutatua changamoto hiyo iliyodumu kwa muda mrefu.