28.2 C
Dar es Salaam
Sunday, October 2, 2022

MAJALIWA AMWAGIZA OCD IGUNGA KUWAKAMATA WALIOHUJUMU MRADI

Na Mwandishi Wetu – Tabora


WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amemwagiza Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Igunga, Ally Mkalipa, awakamate watu wote waliohusika katika ubadhirifu uliofanyika katika mradi wa mashine ya kukobolea mpunga ya Kijiji cha Chomachankola.

Halmashauri ya Igunga ilitoa Sh milioni 35 kwa ajili ya kukiwezesha kijiji hicho kununua mashine ya kukoboa mpunga lengo likiwa ni kuwawezesha wakulima kuliongezea thamani zao hilo kwa kukoboa mpunga na kuuza mchele.

Agizo hilo alitoa juzi jioni baada ya Mbunge wa Manonga, Seif Gulamali, kumlalamikia kuhusu fedha zilizotolewa kwa ajili ya mradi wa mashine ya kukoboa mpunga ya kijiji hicho zilizotolewa miaka mitano iliyopita lakini hadi sasa mradi haujaanza.

Majaliwa alisema watu wote waliohusika na ubadhirifu huo ambao ni Katibu wa Kamati ya mradi huo, Daudi Mwangaluka, John Fumbuka (mjumbe), Yusta Thomas (mweka hazina) na Hansa (mkandarasi), wakamatwe na kufikishwa mahakamani.

Alisema Serikali haiwezi kukubali kuona fedha za wananchi zilizotolewa kwa ajili ya miradi ya maendeleo zikitafunwa na watu wachache wasiokuwa waaminifu.

Pia alikemea vitendo vya watoto wa kike kukatishwa masomo kwa kupewa ujauzito na aliwataka wazazi na walezi wahakikishe wanasimamia elimu ya mtoto wa kike ili aweze kumaliza masomo yake.

Alisema watoto wa kike wanatakiwa kuheshimiwa katika jamii kwa kuachwa waendelee na masomo yao bila ya usumbufu wa aina yoyote na atakayebainika kukatisha masomo atachukuliwa hatua kali za kisheria.

“Kila mkazi wa wilaya hiyo hususani vijana wawe walinzi wa watoto wa kike na ni marufuku kuoa mwanafunzi au hata kumweka kinyumba kwa kuwa ni kinyume na sheria na atakayebainika Serikali imeweka adhabu kali ambayo ni kifungo kisichopungua miaka 30 gerezani.

“Hapa wanafunzi wengi wanashindwa kuendelea na masomo yao kwa ajili ya kupewa ujauzito, sasa kabla ya kutenda jambo hilo ni lazima ujifikirie maana adhabu yake ni kubwa. Ukimpa ujauzito mwanafunzi au kumuoa jela miaka 30, ni bora ukaachana kabisa na wanafunzi,” alisema.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
202,491FollowersFollow
554,000SubscribersSubscribe

Latest Articles