29.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

RISASI ZARINDIMA MAHAKAMANI DAR

Na Waandishi Wetu -DAR ES SALAAM


RISASI zimerindima katika Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam, wakati askari magereza mmoja akijaribu kumzuia mtuhumiwa ambaye alikuwa ameachiwa huru.

Moja ya rasasi hizo ilimpata Gabriel Msuya (19), mkazi wa wa Mabibo Jeshini, ambaye alikuwa amefika mahakamani hapo kusikiliza kesi yake.

Tukio hilo lililotokea jana saa tano asubuhi, lilizua taharuki na watu kutawanyika kwenye eneo.

Baada ya kupigwa risasi, Msuya alikaa takribani dakika 15 akiwa amelala chini huku akiwa amezungukwa na askari.

Msuya alisikika akilalamika kuwa na maumivu, huku akiwaomba askari hao kumpeleka hospitali.

Baadaye alipandishwa katika gari la polisi na kupelekwa Hospitali ya Mwananyamala ambako alikaa kwa muda kabla kuhamishiwa Hospitali ya Mloganzila iliyopo Kibamba wilayani Ubungo.

Kabla ya kuchukuliwa na kupelekwa hospitali, mmoja wa askari hao alisikika akisema; “unaona sasa, haya ndiyo madhara, watu mnaachiwa mnakimbia ovyo.”

Baadaye askari aliyerusha risasi hizo, aliondolewa eneo hilo na polisi.

Kabla ya kuondoka, walifika askari kanzu ambao walitaka kumchukua, lakini walizuiwa na askari magereza wengine.

Mtuhumiwa aliyekuwa ameachiwa huru na mahakama, risasi zilivyopigwa alilala chini na baada ya hali kutulia walimkamata.

Hata hivyo, askari hao hawakutaka kutaja jina la mtuhumiwa huyo wala sababu za kutaka kumkamata tena baada ya kuwa ameachiwa huru.

Akizungumza na MTANZANIA, John Msuya, ambaye ni kaka wa Msuya, alisema ndugu yake alipatwa na tukio hilo baada ya kufika mahakamani hapo kusikiliza kesi yake iliyokuwa ikiendelea kutajwa.

“Nilikuja kumsindikiza ndugu yangu Gabriel ambaye alikuwa na kesi hapa mahakamani kwa ajili ya kusikilizwa, lakini kabla ya kesi yake kusomwa ilikatokea hili tukio katika mazingira ambayo hatukuyatarajia,” alisema.

Alisema baada ya Gabriel kujeruhiwa kwa risasi kiunoni, askari magereza waliamua kumchukua na kumwahisha katika Hospitali ya Rufaa Mwananyamala kwa matibabu.

MTANZANIA lilifika Hospitali ya Mwananyamala na kukuta majeruhi huyo akipatiwa huduma ya kwanza, huku askari wa doria wakiendelea kuzunguka ndani ya hospitali hiyo.

Hata hivyo, muda mfupi baadaye, majeruhi huyo alikimbizwa katika Hospitali ya Mloganzila.

Mmoja wa madaktari waliokuwa wakimpatia huduma majeruhi huyo, alipotakiwa kueleza kuhusu hali yake, alisema yeye si msemaji na alipotafutwa mganga mkuu, hakuweza kupatikana kwa taarifa kwamba yuko nje ya hospitali hiyo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Jumanne Muliro, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba ofisi yake kwa sasa inafanya uchunguzi kupata ukweli ili hatua za kisheria zichukuliwe.

Alisema kwa sasa wanafuatilia kuona mazingira ya tukio hilo hadi risasi hizo zilivyofyatuliwa ili kujiridhisha kisha kufuata taratibu za kisheria.

“Mimi sifanyi kazi kienyeji, siwezi kukamata kabla sijafanya uchunguzi. Ninasisitiza kwamba tunafanya uchunguzi, utakapokamilika tutawakamata watuhumiwa na kufuata taratibu zote za kisheria,” alisema.

Alitoa ufafanuzi kwamba katika mazingira yaliyopo, askari waliokuwepo eneo la tukio ni wa Jeshi la Magereza, ambao hata hivyo hawajakamatwa kwa hiyo taratibu zote za kisheria zitafuatwa uchunguzi utakapokamilika.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles