MOHAMED MHARIZO Na ADAM MKWEPU-DAR ES SALAAM
WAKATI Ligi Kuu Tanzania Bara ikitarajia kuanza Agosti 22, mwaka huu, suala la mdhamini mkuu wa ligi hiyo limekuwa kitendawili.
Kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom Tanzania, ambao wamekuwa wadhamini wakuu wa ligi hiyo, wamekuwa kimya tangu kutangazwa kuanza ligi hiyo, jambo ambalo si la kawaida.
Mkataba wa Vodacom kudhamini Ligi Kuu Tanzania Bara uliosainiwa Agosti Mosi, 2015, ulimalizika Julai 31, mwaka huu na tangu hapo, inaelezwa kuwapo mazungumzo kati ya wadhamini hao na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Vodacom walisaini mkataba wa miaka mitatu na TFF kuendelea kuusaidia mpira wa Tanzania kwa mkataba wenye thamani ya Sh bilioni 6.6.
TFF imekuwa kimya kumtangaza mdhamini mkuu wa ligi hiyo, wakidai mazungumzo kati yao na Vodacom yanaendelea.
Lakini hata hivyo, TFF kupitia Ofisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi (TPLB), Boniface Wambura, jana ilituma barua ya udhamini wa ligi hiyo kwenda kwa timu shiriki, kuonyesha mchanganuo wa fedha za wadhamini waliopo hadi sasa.
Katika barua hiyo kwa timu za Ligi Kuu, Wambura alieleza kwamba, hadi sasa ligi hiyo ina wadhamini wawili pekee, ambao ni Azam Pay TV wenye haki za matangazo pamoja na benki ya KCB, ambao ni wadhamini wenza.
Barua hiyo pia ilieleza, malipo stahiki kwa kila timu kwenye msimu wa 2018/19 kutokana na udhamini huo ni Sh 162,624,000 kutoka kwa Azam TV na Sh 15,000,000 kutoka kwa KCB.
Malipo kutoka kwa Azam TV yatalipwa kwa awamu nne, wakati yale ya KCB Tanzania yakilipwa kwa awamu mbili.
Wadhamini pekee waliopo hadi sasa kwenye ligi hiyo ni pamoja na KCB, ambao Julai mwaka huu, waliingia mkataba na TFF wenye thamani ya Sh milioni 420 na Azam TV.
Akizungumza kuhusu suala la mdhamini mkuu wa ligi hiyo jana, ambaye mara nyingi amekuwa ni Vodacom, Mwenyekiti wa Lipuli FC, Ramadhani Mahano, alisema kuwa, barua hiyo ilipelekwa na fedha za matangazo kutoka Azam Sh milioni 20 ikiwa wiki moja kabla ya Ligi Kuu kuanza.
“Julai 20 mwaka jana tulipewa fedha za matangazo Sh milioni 46, huku wadhamini wakuu ambao walikuwa Vodacom wakitupa Sh milioni 23 pamoja na vifaa.
“Tofauti na sasa kwa namna inavyoonekana, Vodacom wamejitoa na kiasi tulichopewa ni kidogo, hivyo kwa vyovyote vile ligi itakuwa ngumu kama hali ikiwa hivi, hatuwezi kupambana na timu zenye uwezo kifedha, hii ni hali mbaya sana si kwetu tu, bali katika maendeleo ya mpira wetu,” alisema Mahano.
Mkuu wa Kitengo cha Masoko wa Vodacom, Nandi Mwiyombella, amenukuliwa na gazeti hili akisema kuwa bado wanaendelea na mazungumzo kati yao na TFF.
“Vodacom Tanzania tumejizatiti katika kukuza vipaji vya vijana, hili tumekuwa tukilifanya kupitia programu mbalimbali na michezo, hii ni pamoja na kudhamini Ligi Kuu ambayo tumekuwa wadhamini wakuu kwa zaidi ya miaka saba sasa.
“Udhamini huu utaendelea na kwa sasa tunaendelea na majadiliano kati yetu na TFF, mazungumzo yakikamilika tutakuja na jibu sahihi,” alisema.