Na MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM
IDARA ya Uhamiaji imesema inaendelea kuchunguza uraia wa Askofu wa Jimbo Katoliki la Rulenge, Wilaya ya Ngara mkoani Kagera, Severine Niwemugizi (62).
Maelezo hayo ya Uhamiaji yametokana na gazeti hili kutaka kujua hatua ambayo imefikiwa na idara hiyo baada ya kuwapo ukimya tangu askofu huyo alipohojiwa kuhusu uraia wake Novemba 28 na Desemba 4 mwaka jana.
Akizungumza na gazeti hili kwa simu, Msemaji wa Idara ya Uhamiaji, Ally Mtanda, alisema uchunguzi wa uraia wa Askofu Niwemugizi bado unaendelea na ukikamilika kutakuwapo mawasiliano kati yake na idara hiyo.
Mtanda alisema suala la uraia ni haki ya mtu, kwa mantiki hiyo, Idara ya Uhamiaji huwa haikurupuki katika kufanya uchunguzi, bali hufuata taratibu zinazotakiwa ili kupata matokeo sahihi na kumtendea haki mlengwa.
“Sio kwamba tunachelewa kutoa matokeo ya uchunguzi, bali tuna taratibu zetu za kufanya na hatukurupuki kuchunguza kwa sababu tunatambua suala la uraia ni haki ya mtu.
“Kwa kutambua kuwa suala la uraia ni haki ya mtu, wakati mwingine huwa tunavuka mpaka kwenda upande wa pili kwenye nchi ambayo mlengwa anahusishwa ili kukusanya taarifa zaidi za kujiridhisha,” alisema Mtanda.
Katika simulizi yake kwa gazeti hili mwaka jana, Askofu Niwemugizi alisema; “Niliombwa kibali kinachoniruhusu kuwa nchini, nikashangaa, nikasema mimi ni Mtanzania, nikaambiwa nilete ‘document’ (nyaraka).
“Nilipeleka hati ya kusafiria, kitambulisho cha kupigia kura na cheti cha kuzaliwa, wakasema wataniita tena.
“Baada ya kuitwa mara ya pili, nilipewa fomu ya kujaza. Waliniita tena wakasema bado wanataka kujiridhisha.”
Askofu Niwemugizi ambaye aliwahi kuwa Makamu wa Rais wa Baraza la Maaskofu wa Katoliki (TEC), aliwahi kusimulia alivyokuwa akihojiwa Uhamiaji na kujibu kama ifuatavyo:
Swali: Je, ulizaliwa wapi?
Jibu: Nilizaliwa katika Kitongoji cha Kayanza, Kijiji cha Kabukome, Kata ya Nyarubungo, Wilaya ya Biharamulo.
Swali: Ulizaliwa tarehe ngapi?
Jibu: Nilizaliwa Juni 3, mwaka 1956.
Swali: Ulibatizwa wapi?
Jibu: Nilibatizwa katika Parokia ya Katoke, Biharamulo.
Swali: Elimu ya Msingi na Sekondari ulisoma wapi?
Jibu: Nilisoma Shule ya Msingi Katoke, Biharamulo na Shule ya Sekondari Nyakato Bukoba (O-level).
Baada ya kumaliza ‘O-level’ niliingia Seminari Kuu ya Ntungamo, Bukoba halafu nikatoka hapo nikaenda Kipalapala, Tabora.
Swali: Wazazi wako walizaliwa wapi?
Jibu: Walizaliwa sehemu mbalimbali. Mama alizaliwa Lusahunga na baba alizaliwa katika Tarafa ya Nyarubungo, Kijiji cha Kabukome, Kitongoji cha Kayanza.
Swali: Katika maisha yako yote je, ulishawahi kuhisiwa kuhusu uraia wako?
Jibu: Sijawahi kuulizwa, muda wote nimetumia passport (hati ya kusafiria) ya Tanzania na hakuna aliyewahi kuniuliza suala la uraia.
Swali: Je, unafikiri kwanini hili linajitokeza sasa?
Jibu: Baada ya hivi karibuni kutoa ushauri, kwamba ni vizuri mchakato wa Katiba ukarejewa, watu wali-react, sasa naweza kupata picha nini kimesababisha nianze kuhojiwa.
Swali: Je, Baraza la Maaskofu wa Katoliki (TEC) wana taarifa kwamba umeitwa Uhamiaji?
Jibu: Sijawataarifu kwa sababu suala hili lilionekana bado liko chini chini, lakini nafikiri nitatafuta namna ya kuwafahamisha juu ya jambo hili.
Swali: Je, mbali na kuwa askofu, uliwahi kushika nafasi gani katika Kanisa Katoliki?
Jibu: Niliwahi kuwa Rais wa TEC, kuanzia mwaka 2000 hadi 2006 na baadaye nikawa Makamu wa Rais kuanzia mwaka 2012 hadi 2015.
Swali: Je, una hofu yoyote juu ya usalama wako?
Jibu: Mimi sina hofu na usalama kwa sababu ninajua kufa ni mara moja. Kwahiyo, ninabaki kivulini, ninazungumza tu ninavyowajibika kama askofu.
UCHUNGUZI WATU WENGINE MAARUFU
Mbali na Askofu Niwemugizi, MTANZANIA Jumapili lilimuuliza Mtanda hatua iliyofikiwa juu ya uchunguzi wa uraia wa Mkurugenzi wa Taasisi inayojishughulisha na tafiti ya Twaweza, Aidan Eyakuze na Mwenyekiti wa Mtandao wa Wanafunzi Tanzania (TSNP), Abdul Nondo na akasema uchunguzi wao bado unaendelea.
Alipoulizwa kuhusu uchunguzi wa uraia kwa watu wengine maarufu kama Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu, Sheikh Issa Ponda, Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallance Karia, katibu wake Kidau Wilfred, Askofu Mkuu wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship (FGBF) Zakaria Kakobe na Mkurugenzi wa Kituo cha Utetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) Onesmo Olegurumwa, Mtanda alisema utendaji wa idara hiyo hautambui umaarufu wa mtu bali unafanya kazi kwa misingi ya sheria na taratibu zilizowekwa.
Mbali na kutoa ufafanuzi huo, alisema uchunguzi wa uraia kwa Askofu Kakobe na Olengurumwa bado unaendelea.
Alisema kwa upande wa Sheikh Ponda na viongozi wote wawili wa TFF, uchunguzi ulishakamilikwa na walishapewa barua za uthibitisho wa uraia wao.
Katika muktadha huo huo, gazeti hili lilimwomba takwimu za idadi ya watu wanaohojiwa na kuchunguzwa uraia wao katika kipindi cha miezi tisa hadi Agosti, mwaka huu, lakini alikataa kwa kusema taarifa hizo hubaki ndani ya idara kwa utendaji zaidi.