27.5 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

MAALIM SEIF, LOWASSA WATIKISWA

AGATHA CHARLES Na Eliya Mbonea – Dar/ARUSHA


WAZIRI Mkuu wa zamani na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Edward Lowassa na Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, wamepata pigo baada ya wafuasi wao wa karibu kujiondoa ndani ya vyama vyao na kujiunga na CCM.

Wafuasi hao waliotangaza kujiunga na CCM jana kwa nyakati tofauti Arusha na Dar es Salaam, ni aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya CUF (upande wa Maalim Seif), Julius Mtatiro na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Monduli ambaye pia ni Diwani wa Monduli Mjini mkoani Arusha, Isack Joseph maarufu kwa jina la Kadogoo.

Kuondoka kwa Mtatiro na Kadogoo upinzani, ni pigo kubwa kwao kwa kuwa ni miongoni mwa waliokuwa mstari wa mbele kutekeleza na kuendeleza matakwa ya vyama hivyo, wakati mwingine kupitia umoja wao wa Ukawa.

Mtatiro ambaye amekuwa CUF kwa miaka 10, aliwahi kuwa Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, Katibu wa Ukawa katika Bunge Maalumu la Katiba na mtu mwenye ushawishi aliyefanya kazi kwa ukaribu zaidi na Maalim Seif hata baada ya chama hicho kuingia kwenye mgogoro.

Sifa za Mtatiro hazina tofauti za zile za Kadogoo, ambaye licha ya kuwa na ushawishi mkubwa katika siasa za Monduli, pia alikuwa karibu na Lowassa wakiwa CCM na hata alipohamia Chadema aliondoka naye, ambako aliukwaa udiwani na baadae kuwa mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya hiyo baada ya madiwani wengi kutokana na chama hicho.

Kuondoka kwa Kadogoo, sasa huenda kukairejesha halmashauri hiyo chini ya CCM  baada ya madiwani wanane wa Chadema kujiuzulu na kujiunga na chama hicho tawala.

Itakumbukwa katika Uchaguzi Mkuu wa 2015, Chadema ilipata madiwani 12 katika Jimbo la Monduli huku CCM ikiambulia wanane.

Kati ya madiwani wanane wa Chadema waliohamia CCM, watano ambao ilikuwa washiriki uchaguzi wa leo kupitia chama hicho tawala, wamepita bila kupigwa na mmoja tu ndiye anayeshiriki.

Diwani mwingine ni yule aliyetangaza kuhama na Kadogoo jana na kwa mantiki hiyo, Chadema sasa itakuwa imebakiza madiwani wanne wanaotokana na kata 20 za jimbo hilo.

MTATIRO

Akizungumza mbele ya waandishi wa habari, Dar es Salaam jana, Mtatiro, alisema kabla ya kuchukua uamuzi, alifanya tafakuri nzito ya mwezi mmoja na kupitia kwa ufasaha maeneo matano.

Akiyataja moja baada ya jingine, alisema  alifanya tafakari ya ushiriki na mchango wake katika siasa za CUF, mgogoro unaoendelea, ushiriki wake kama kijana na kiongozi katika kuchochea maendeleo, agenda muhimu za usimamizi na uendeshaji wa nchi pamoja na mustakabali wake kisiasa.

Alisema baada ya kutafakari huko, alipata majibu kuwa alikuwa na mchango mkubwa ndani ya CUF na alishiriki kukiuhisha huku mwaka 2015 zikifanyika jitihada kubwa na kusasabisha kupatikana kwa madiwani takribani 300 wakishirikiana na Ukawa.

Akizungumzia eneo la pili, Mtatiro alisema aligundua Mwenyekiti wa CUF anayetambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba, anafanya jitihada kuhakikisha chama hicho kinakufa kwa upande wa Bara.

“Nilitafakari katikati ya mgogoro huo, nimejiridhisha napaswa kuamua kwa uzito wa kipekee namna ya kuwatumikia Watanzania, kwa sasabu Mungu amenijalia utashi na akili ya kudumu, lakini pia amenipa muda maalumu wa kukaa hapa duniani,” alisema Mtatiro.

Alisema kabla ya kutangaza uamuzi wake huo, wiki hii alimjulisha Maalim Seif juu ya nia yake hiyo na siku mbili zilizopita alimwandikia barua rasmi.

Alipoulizwa kile alichojibiwa na Maalim Seif, alisema hakumjibu na hana budi kusonga mbele.

Akifafanua eneo la tatu, alisema ushiriki wake katika maendeleo ya nchi aligundua ulikuwa mdogo tofauti na alivyoisaidia CUF.

Alisema kutokana na kugundua hilo, alifikia uamuzi wa kufanya siasa za matendo za kujitolea ili kumsaidia Rais Dk. John Magufuli  pamoja na kumshauri na baada ya miaka mitano aweze kuonyesha alichokifanya.

“Naanza kushiriki kikamilifu kwa kutumia vipaji vyangu vyote vya uongozi, kuisaidia nchi yangu, Serikali yangu, Watanzania,” alisema Mtatiro.

Alisema alijiridhisha kuwa Watanzania wana matatizo mengi, lakini baadhi ya watatuzi muhimu wenye vipawa na uwezo akiwamo yeye, hawana majukwaa mwafaka ya kufanya hivyo.

“Kuanzia sasa nitaanza kufanya siasa za vitendo, siasa za maendeleo, za kujitolea kwa hali na mali, kuishauri Serikali, Rais na watendaji wake kwa njia mwafaka na za karibu zaidi.

“Nimefanya uamuzi huu ili baada ya miaka mitano hadi kumi mtu akiniuliza nimweleze nimelifanyia nini taifa langu na nionyeshe kwa vitendo,” alisema Mtatiro.

Alisema anajulikana kama mwanasiasa mkubwa, lakini aliyefanya zaidi CUF tofauti na vijana wengine wadogo waliofanya makubwa kwa taifa kwa kuwa tu walikuwa kwenye majukwaa sahihi.

“Lengo la kuzaliwa hapa duniani sio kupigania vyama ni kupigania nchi. Ndani ya miaka kadhaa ijayo lazima mtu nimjibu kwa vitendo na si kwa maneno kuwa nilipiga kelele kiasi gani, nilimshughulikia mtu kiasi gani, nimeona haina tija,” alisema Mtatiro.

Kuhusu eneo la nne ambalo ni agenda muhimu za usimamizi na uendeshaji wa nchi, alisema aligundua kuwa ajenda zote muhimu zilibebwa na Serikali ya awamu ya tano.

Alisema moja ya vitu ambavyo Ilani ya CUF ilitaka vifanyike, ni pamoja na utoaji wa elimu bure, watendaji kufanya kazi pamoja na kushughulikia rushwa kubwa kubwa jambo ambalo alikiri linafanyika katika awamu hii.

Mtatiro alisema tafiti mbalimbali zinaonyesha kiwango cha rushwa kimepungua, huku watuhumiwa wakubwa wakifikishwa mahakamani.

Alisema yapo mengi mazuri yanayofanywa na Rais Magufuli, lakini wakati mwingine hayasemwi kutokana na misimamo ya vyama wanavyokuwa.

Mtatizro alisema wakati akitafakari, aliangalia vyama vyote ambavyo alikiri kuvifahamu vyema, lakini kwa kuzingatia aina ya siasa alizoamua kuzifanya, alihitaji jukwaa la CCM.

Alisema haendi CCM kutafuta nafasi au ukuu, bali ni uamuzi wa kutafuta jukwaa sahihi kwani kama alivyojiunga na CUF mwaka 2008, hivyo hivyo anapaswa kuondoka kwenda kwingine.

Alipoulizwa na waandishi iwapo naye amenunuliwa kama inavyodaiwa kwa baadhi ya wanaohama upinzani, Mtatiro alisema hawezi kununuliwa kwa kuwa hana bei bali ni uamuzi binafsi.

Katika hilo, pia alisema hajawahi hata kuwasiliana na viongozi wa CCM na kwamba hata wakati wa Bunge la Katiba alidiriki kuacha fedha nyingi, hivyo kwake hoja hiyo haina nafasi.

Kuhusu kama uamuzi wake huo ni kutaka CUF ife, Mtatiro alisema ameondoka akiwa ameingiza vijana wengi kutoka vyuo vikuu, hivyo hana nia ya kuiua.

MTANZANIA Jumapili lilimtafuta Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole ili kujua iwapo Mtatiro atapokewa ndani ya chama hicho, lakini hakuweza kupokea simu wala kujibu ujumbe mfupi aliotumiwa.

KADOGOO

Kwa upande wake, Kadogoo alitangaza rasmi kujivua uanachama wa Chadema na kujiunga na CCM wakati wa mkutano wa Katibu Mkuu Dk. Bashiru Ally aliyekuwa akizungumza na wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya ya Monduli.

Kadogoo aliingia ukumbini hapo wakati Dk. Bashiru akiwahutubia wajumbe hao na kuamsha shangwe zilizomlazimisha kusitisha kwa muda kuzungumza.

Mmoja wa waliompokea ni mgombea wa ubunge wa Monduli kupitia CCM ambaye wiki iliyopita alijiengua Chadema, Julius Kalanga, ambaye alimkimbilia na kumkumbatia na kuanza kutokwa machozi.

Kadogoo hakuhama peke yake, bali pia na wanachama wengine wa Chadema akiwamo aliyekuwa Mwenyekiti wa zamani wa CCM Mkoa wa Arusha, Yona Nnko aliyeongozana na wazee wa mila wa Kishiri kutoka Wilaya ya Arumeru.

Mwingine aliyetambulishwa kwenye mkutano huo ni aliyekuwa Katibu Mkuu wa NCCR- Mageuzi, Danda Juju.

Itakumbukwa makada hao, Mtatiro na Kadogoo, kwa nyakati tofauti waliwahi kuonyesha kuwa hawakuwa na nia ya kujiunga na CCM.

Desemba mwaka jana, Mtatiro aliwahi kukanusha uvumi wa kujiunga na CCM, kwamba hakuwa na mpango wa kuhama CUF.

Agosti 5 mwaka huu, Kadogoo akiwa kwenye mkutano wa hadhara wa kumnadi mmoja wa wagombea udiwani, alimweleza Mwenyekiti  wa Chadema, Freeman Mbowe kuwa waliingia wakiwa madiwani 19, lakini walibaki madiwani wa kata watano na wale wa viti maalumu watano.

Katika mkutano huo alisema alikuwa akipata hati safi mfululizo ndani ya halmashauri hiyo  na hivyo akiona yamemshinda ni bora arudi nyumbani akachunge ng’ombe kwa kuwa Chadema ilimpokea kwa heshima.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles