25.9 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 27, 2024

Contact us: [email protected]

FRED LOWASSA ACHUKULIWA FOMU UBUNGE MONDULI

 

Na JANETH MUSHI, ARUSHA


MTOTO wa Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, Fred Lowassa, amechukuliwa fomu kuwania ubunge Jimbo la Monduli, kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Ingawa Fred hakupatikana kuzungumzia suala hilo, dalili za kujitosa kwenye uchaguzi, zilianza kuonekana baada ya aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo kwa tiketi ya Chadema, Julius Kalanga, kujiuzulu na kujivua uanachama wa chama hicho kikuu cha upinzani nchini.

Baada ya kujiuzulu kwa Kalanga, baadhi ya vijana wa Chadema akiwamo Diwani wa Sombetini, Ally Bananga, waliandika kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii kuwa dawa yake ni kumpelekea Fred apambane naye kwenye uchaguzi mdogo.

“Huyu ndiye wa kwenda kumzima Kalanga, uchaguzi mdogo ukiitishwa nitakishawishi chama changu twende na Fred Lowassa, kampeni meneja nakamata mwenyewe mzee baba,” ilisema sehemu ya ujumbe kwenye ukurasa wa Instagram wa Bananga, ambaye ni mmoja wa vijana wenye ushawishi mkubwa ndani ya Chadema.

Uchaguzi wa jimbo hilo unatarajiwa kufanyika Septemba 16.

Jana akizungumza na MTANZANIA kwa simu, Katibu wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Amani Golugwa, alitaja watia nia wengine kuwa ni Cecy Ndosi ambaye ni Mwenyekiti wa Bawacha Mkoa wa Arusha na Diwani wa Viti Maalumu, Jimbo la Monduli na Yonas Laizer ambaye ni Diwani wa Kata ya Lepurko.

Golugwa ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Arusha, alisema wengine waliochukua fomu ni Erick Ngwijo na Lelubu Kivuyo.

Alisema baada ya watia nia hao kurejesha fomu hizo jana, kikao cha kupiga kura ya maoni kitafanyika Agosti 11 kabla ya Kamati ya Utendaji ya Wilaya kukaa na kutoa mapendekezo yake kisha kupelekwa Kamati Kuu ya chama hicho.

“Baada ya hapa Monduli, Jumamosi tuna mkutano wa wilaya wa kura ya maoni ambao utafanyika Kata ya Migungani, halafu siku hiyo hiyo Kamati ya Utendaji ya Wilaya itakaa na kuweka mapendekezo yake na yatachuliwa na ofisi yangu ya kanda na kupeleka makao makuu kwenye kikao cha Kamati Kuu ya chama kwa maamuzi,” alisema.

MGOMBEA CCM

Naye Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Monduli, Wilson Lengima, alisema katika jimbo hilo wana mtia nia mmoja ambaye ni Kalanga na kuwa alishachukua fomu na kuirejesha Agosti 7, mwaka huu na kuwa wako katika vikao na taratibu nyingine zinazofuata watazitoa baadaye.

MAKUNDI CCM

Monduli ina historia ndefu kisiasa kufuatia kuongozwa na mawaziri wakuu maarufu, Edward Sokoine aliyefariki Aprili 12 mwaka 1984, na Edward Lowassa aliyeongoza jimbo hilo kwa zaidi ya miaka 20 kabla ya kugombea urais mwaka 2015.

Kalanga ambaye alikuwa mbunge wa jimbo hilo kupitia Chadema kwa kipindi cha kwanza mwaka 2015, alishinda kwa kupata kura 35,024 dhidi ya mpinzani wake ambaye ni mtoto wa Sokoine, Namelok Sokoine (CCM) aliyepata kura 29,925.

Julai 31, mwaka huu Kalanga alitangaza kurejea CCM alikohama mwaka 2015 kabla ya Uchaguzi Mkuu kufanyika.

Alidai sababu zilizomfanya kujiuzulu Chadema ni siasa za uhasama, malumbamo na chuki na kudai kuwa anajiunga na CCM ili kuunga mkono juhudi za Rais Dk. John Magufuli.

Agosti 7, mwaka huu, kundi la wanachama wa CCM lilijitokeza hadharani kupinga Kalanga kurejeshwa kugombea ubunge kupitia chama hicho pasipo kura ya maoni kufanyika.

Baadhi ya wanachama wa CCM kutoka kata za Isilalei, Monduli Juu na Sepeko, waliandamana hadi ofisi za chama hicho wakimtuhumu Mwenyekiti wa chama hicho Wilaya ya Monduli, Wilson Lengima, kwamba kwa kushirikiana na viongozi wengine, wanapanga njama ili Kalanga apitishwe kuwa mgombea ubunge pasipo kufanyika kura ya maoni.

Hata hivyo, Lengima alikanusha madai hayo akisema chama hicho kina utaratibu wa kuwapata wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi, hivyo kuwataka wana-CCM kuwa watulivu.

Katika uchaguzi mdogo wa ubunge katika majimbo ya Kinondoni, Dar es Salaam na Siha, Kilimanjaro, waliokuwa wabunge (Maulid Mtulia – CUF) na Dk. Godwin Mollel – Chadema) waliojiengua na kujiunga na CCM, waliteuliwa pasipo kupitia utaratibu wa kura ya maoni kuwa wagombea.

KALANGA ALIVYOPENYA CCM

Oktoba 2, 2015 aliyekuwa mgombea urais kwa tiketi ya Chadema, Lowassa, alimnadi Kalanga kugombea Monduli, huku akieleza kuwa angezungumza na mgombea ubunge wa CCM, Namelok kuona kama angekubali kupanda ‘basi’ la Chadema chini ya mwamvuli wa Ukawa.

Katika mkutano wake wa kwanza wa kampani Monduli, uliofanyika Mto wa Mbu, Lowassa aliulizwa na wananchi kuhusu mustakabali wa Namelok ili wajue kama wamchague Kalanga au binti huyo wa waziri mkuu wa zamani, Sokoine.

Lowassa alisema angekutana na Namelok siku hiyo hiyo ili waelewane kwa kuwa asingependa kuvunja umoja wao wa muda mrefu.

“Kuhusu suala la ubunge, nimekuwa mbunge kwa miaka 20, hivyo natakiwa nijue mbunge atakayefuata. Nitakubaliana na Namelok, akikataa kupanda basi hili basi,” alisema Lowassa huku baadhi ya vijana wakitaka kujua wamfanye nini.

Lowassa alisema anataka Monduli ibaki ileile yenye amani na utulivu na ambaye hataki kupanda kwenye basi lake ataachwa.

Wakati Lowassa akizungumzia suala la kujadiliana na mtoto huyo wa Sokoine, Kalanga alikuwepo akisubiri kunadiwa.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles