Na VERONICA ROMWALD – ALIYEKUWA MEATU
MWAKA 2003, Mariam James (22), Mkazi wa Meatu, alijaaliwa kujifungua mtoto wake wa kwanza, katika Hospitali ya Wilaya ya Meatu iliyopo nje kidogo ya Mkoa wa Simiyu.
Mariam hivi sasa ni mama wa watoto sita, anasimulia safari yake ya uzazi ilivyokuwa ngumu hadi kufikia hatua ya watoto wake wawili kati yao kujifungulia nyumbani kwa mkunga wa jadi.
“Ninaishi kijiji kilichopo umbali wa zaidi ya kilometa 10 hadi kufika hospitali, nakumbuka mwanangu wa kwanza nilikuwa nyumbani nilipohisi uchungu, bahati nzuri kulikuwa na mama mtu mzima ambaye alikuja kunisalimu, yeye ndiye aliyenisaidia kujifungua siku hiyo,” anasimulia.
Anasema mtoto wake wa pili naye alijifungulia nyumbani kwani hakuwa na mtu wa karibu kuweza kumpatia msaada kwa wakati huo.
“Mwanangu wa tatu nilijifungua njiani nilipokuwa nawahishwa katika Hospitali ya Wilaya ya Meatu, nilihuzunika lakini sikuwa na la kufanya, nikakubaliana na matokeo,” anasema.
Mariam anasema ujauzito wake wa nne na wa tano alijifungua salama hospitalini, kwani alipojihisi kufikia kujifungua alilazimika kuhamia jirani na hospitali ili apate msaada pale inapohitajika.
“Lakini mimba yangu ya sita, ingawa nilijifungua hapa hospitalini hata hivyo nilijifungua mwenyewe bila msaada wa mtaalamu wa afya,” anasema.
Akisimulia jinsi ilivyokuwa, Mariam anasema: “Mume wangu alinihamisha kama kawaida kutoka kule kijijini na kunileta hapa karibu na hospitali.
“Uchungu uliponishika dada yangu ambaye alikuja kukaa na mimi pale tulipopanga kwa muda, alinisaidia kunifikisha hospitalini. Siku hiyo nilikuta wajawazito zaidi ya 10 ambao nao walikuwa wanasubiri huduma ya kujifungua.
“Ingawa nilikuwa na dalili zote za kujifungua lakini niliwekwa katika wodi ya wagonjwa wa kawaida, pamoja na wale wenzangu.
“Muuguzi alitueleza tunapaswa kusubiri kwa muda kwani katika chumba cha kujifungulia kulikuwa na mjamzito mwingine ambaye alikuwa anajifungua,” anasimulia.
Anasema hawakuwa na jinsi zaidi ya kukubaliana na kauli ya muuguzi huyo, lakini yeye hakuweza kukaa muda mrefu akajikuta amejifungua pale pale.
“Sikuwa na jinsi, sikuweza kujizuia… unajua tena uchungu ukikolea huwa hauna simile. Nilihisi kusukuma mtoto, nikasukuma naye akatoka. Hakukuwa na muuguzi wala daktari pembeni yangu ambaye alinisaidia.
“Nilijifungua mwenyewe nashukuru Mwenyezi Mungu punde baada ya kujifungua wataalamu walikuja na kunisaidia kumuweka vizuri,” anasimulia.
Anaongeza: “Nikiwa pale nilishuhudia wajawazito watatu nao wakijifungua pale pale wodini na kuna mmoja ambaye alipoteza maisha kwa kupoteza damu nyingi, nilihuzunika mno.
Kwanini husubirishwa?
Sally Shaku ni Daktari Mfawidhi katika Hospitali ya Wilaya ya Meatu, anasema hulazimika kuwasubirisha wajawazito wodini hata kama wapo katika hali ya kutaka kujifungua kutokana na changamoto ya ufinyu wa wodi ya kujifungua.
Anasema kwa siku hupokea wajawazito kuanzia 10 hadi 19 ambao huhitaji huduma ya kujifungua katika hospitali hiyo.
“Lakini uwezo wa chumba cha kujifungua ni kupokea mama mmoja pekee kwa ajili ya kujifungua. Kutokana na hali hiyo, ndiyo maana huwa tunalazimika kuwaweka katika wodi ya kawaida.
Daktari huyo anasema kati ya wanaopokelewa, wajawazito wapatao 12 hadi 16 hujifungua kila siku.
“Utaona jinsi ilivyo changamoto. Wote hao wanajifungua lakini chumba chetu cha ‘labour’ ni finyu na kina uwezo wa kutoa huduma kwa mjamzito mmoja pekee, ndiyo maana wengi hujifungua katika wodi ya kusubiria,” anabainisha.
Anafafanua: “Kwa kawaida, tunategemea njia ya mama inapofunguka kwa sentimeta saba, akae katika ‘labour room’ tayari kwa ajili ya kujifungua kwani muda wowote mtoto anaweza kutoka.
“Kwa kawaida njia ya uzazi (cervix) hufungua kwa kiwango cha sentimeta moja kwa saa, wapo ambao hujifungua ndani ya saa tatu hadi nne na wengine zaidi ya hapo.”
Ajifungua watoto watano nyumbani
Leah Maheka, mkazi wa Meatu, ni mama aliyejaliwa kupata watoto sita katika ndoa yake, anasema kati ya watoto hao watano alijifungulia nyumbani na mmoja pekee alijifungulia hospitali.
“Ninakoishi ni mbali na hospitali, kule hakuna huduma nzuri za afya kama hapa wilayani. Ili mjamzito aletwe wilayani kujifungua usafiri unaotumika mara nyingi huwa ni baiskeli.
“Binafsi, nilikuwa natamani mno wanangu wote nijifungulie hospitalini lakini changamoto ilikuwa ni huo usafiri wa kutoka kule kijijini kuja hapa, hasa kipindi cha nyuma kulikuwa hakuna kabisa usafiri.
“Tulitumia zaidi baiskeli, kutokana na hali hiyo wengi tulilazimika kujifungua kwa mkunga wa jadi,” anasimulia.
Anasema siku chache baada ya kujifungua ndipo mama husika na mwanawe husafirishwa kutoka huko kijijini kuja katika Hospitali ya Wilaya ya Meatu kwa ajili ya kupewa huduma zaidi.
Maambukizi na vifo
Dk. Shaku anabainisha athari kubwa inayowakabili wakina mama na vichanga vyao kuwa ni kupata maambukizi ya bakteria au virusi vya magonjwa mbalimbali.
Anasema hiyo ni sababu kubwa ya vifo vitokanavyo na uzazi Meatu, huwa wanashuhudia idadi kubwa ya vifo hasa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita,” anasema.
Anasema kwa mwaka hospitalini hapo ilikuwa vinatokea vifo zaidi ya 19 vya uzazi.
Anasema hali hiyo iliwafanya watafute mbinu ya kuvikabili vifo hivyo na kuamua kutoa mafunzo na mbinu mbadala wataalamu wake wa afya.
“Tulifanya jitihada kubwa kuweza kupunguza idadi hiyo ya vifo, tukawapa mafunzo kazini na nje ya kazi watu wakajifunza jinsi ya kumsaidia mama kuepusha hatari ya vifo.
“Tuliweza kuvishusha hadi kufikia idadi ya vifo vitatu kwa mwaka, na katika kipindi cha mwaka juzi tukapata tena changamoto ya ongezeko la idadi ya vifo ambapo vilifikia 10,” anasema.
Anaongeza: “Mwaka jana tuliweza tena kuvishusha kufikia vifo viwili, bado tunaendelea kupambana na kujiimarisha kuhakikisha tunafikia lengo letu la kuwa na idadi ya vifo sifuri.
Aibu kikwazo
Daktari huyo anasema changamoto kubwa wanayoiona ni wajawazito kuchelewa kuhudhuria kliniki na kwamba hali hiyo ni kikwazo kwao katika kufikia lengo walilojiwekea.
“Tunapowahoji wapo wanaotueleza kwamba eti huona aibu kuja kliniki mimba ikiwa change, ndiyo maana hufika wakiwa umri wa mimba umekwenda kidogo, wakati mimba inapokuwa changa ndiyo mwafaka wa kuanza kliniki.
“Ili kukabili hilo, tunashirikiana na maofisa afya ngazi ya jamii, ambao kwa kawaida wao ndiyo huenda kule vijijini mara kwa mara kuelimisha jamii umuhimu wa kuwahi kliniki kupata huduma,” anasema.
Uhaba wa watumishi
Anasema changamoto nyingine inayoikabili hospitali hiyo ni uhaba wa watumishi kwa kiwango cha zaidi ya asilimia 60.
“Kwa hospitali hii tunahitaji watumishi wapatao 200 hadi 300 lakini tuliopo ni 127, hivyo kwa sisi tuliopo tumejitahidi kujitawanya wenyewe. Katika wodi ya uzazi tumeweka wauguzi 13 ambao ni wengi zaidi kuliko wodi zingine kwani ndiyo yenye changamoto kubwa,” anabainisha.
UNFPA yaokoa jahazi
Meneja Mradi wa Afya ya Mama na Mtoto wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Idadi ya Watu (UNFPA-Tanzania), Felister Bwana, anasema kutokana na changamoto ya ufinyu wa wodi inayokabili hospitali hiyo, shirika hilo liliona ni vema kuwasaidia.
“Wilaya ya Meatu ni miongoni mwa wilaya zilizopo pembezoni mwa Mkoa wa Simiyu, ambayo kwa muda mrefu haikufikiwa na huduma za afya hasa mama na mtoto, ilikuwa na changamoto kubwa.
“Kutokana na hali hiyo, ndiyo maana UNFPA tuliona vema kuiwezesha hospitali hii ambayo imekuwa ikihudumia idadi kubwa ya wagonjwa na kuwa msaada hata kwa vituo vingine vya afya vinavyoizunguka.
“Tukaamua kuiboresha miundombinu yake kwa kujenga majengo mawili ya kisasa ambayo yana vyumba maalum vya upasuaji na maabara,” anabainisha.
Felister anasema katika vyumba hivyo, UNFPA itafunga mashine za kisasa za uchunguzi na matibabu na kwamba mradi huo umegharimu kiasi cha zaidi ya Sh milioni 250 kuukamilisha.
“Ili kuboresha zaidi huduma, tumepanga kuwapatia mafunzo wataalamu wa hospitali hii hasa namna ya kutumia vifaa tutakavyofunga kwa ajili ya kuwasaidia wagonjwa,” anasema.
Anasema katika vyumba hivyo vya upasuaji, chumba kimoja kitakuwa ni maalum kwa ajili ya kuwafanyia upasuaji wajawazito watakaohitaji huduma ya dharura.
“Yaani ikitokea mjamzito anahitaji huduma ya dharura basi apelekwe mapema katika chumba hicho na kusaidiwa tofauti na ilivyo sasa ambapo wanalazimika kusubiria,” anasema.
Dk. Shaku anaishukuru UNFPA kwa msaada huo kwani utawasaidia kukabiliu vifo vitokanavyo na uzazivinavyotokana na changamoto ya ufinyu wa chumba cha kujifungua.
“Tutakapoanza kuvitumia, itatuwezesha kutoa huduma kwa wajawazito watatu kwa wakati mmoja, tofauti na ilivyo sasa ambapo tunatoa huduma kwa mjamzito mmoja,” anabainisha.
Kauli ya wizara
Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), anayehusika na masuala ya Afya, Dk. Zainabu Chaula, anasema serikali inasimamia kwa ukaribu maboresho hayo ya miundombinu kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwamo UNFPA.
“Lakini lazima tuhamasishe wakina mama kuhudhuria kliniki, takwimu zinaonesha pia asilimia 80 hujifungua kwa njia ya kawaida, lakini asilimia 20 iliyobaki huhitaji huduma za upasuaji za dharura.
“Lazima tuwahamasishe kuhudhuria kliniki mapema, na tunajitahidi kuboresha miundombinu yetu. Mkoa wa Simiyu una vituo vya afya 13 na kati ya hivyo vitano pekee ndivyo vilikuwa na uwezo wa kutoa huduma za dharura za upasuaji ili wapate msaada pale itakapohitajika tuokoe maisha yake,” anasema.
MWISHO.