21.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, October 4, 2022

VYAKULA VYA KUEPUKA UNAPOMALIZA KUTUMIA DAWA

VYAKULA na dawa ni vitu ambavyo havikwepeki, vimekuwa vikitumika kila siku katika maisha ya mwanadamu.

Vyakula vimekuwa vikitumika kuupatia mwili nguvu, joto, mafuta, madini na virutubisho vinavyosaidia kuulinda na kuujenga mwili. Uhitaji wa vyakula muhimu mwilini unahitajika wakati wote, si tu pale unapougua.

Kutokana na mwanadamu kutokuwa mkamilifu, zinatokea nyakati ambazo  yanajitokeza magonjwa na matatizo ya kiafya. Ili kurekebisha changamoto hizo, matibabu huanzishwa ambapo pamoja na matumizi ya vyakula vinavyoshauriwa kutumika kulingana na aina ya ugonjwa, pia dawa huwa ni sehemu muhimu inayoponya tatizo husika.

Matumizi ya dawa mara nyingi husababisha maudhi ya hapa na pale, na wakati mwingine yanaweza kujitokeza hata mara baada ya mgonjwa kumaliza dawa alizokuwa akizitumia.

Kwa ujumla, maudhi hayo husababisha baadhi ya watu kuwa na mitazamo hasi juu ya matibabu yanayohusisha umezaji wa dawa au matumizi ya dawa kwa ujumla wake na hasa hasa zile za viwandani zinazotumika katika vituo vya kutolea huduma za afya – kwa maana ya hospitali, vituo vya afya na zahanati.

Hali hii kwa namna moja ama nyingine inaweza ikasababishwa na kuziona dawa za aina fulani kuwa hazifai na hata daktari inapotokea akakuandikia, basi unamuona kama muuaji au mtu asiyekuwa na nia nzuri na afya au usalama wako.

Kwanza kabisa, katika mazoea na tabia za wanadamu, mara nyingi watu wanajikita katika kuangalia mabaya na si mazuri. Hii ipo katika mambo mengi hata yale yanayohusu maendeleo ya mtu mmoja mmoja na hata ya kijamii. Mtu atasimama kukosoa na mara chache pongezi zitatolewa.

Kadhalika na kwa upande wa afya na matibabu, dawa zinazotumika pamoja na mazuri yote ya kutibu magonjwa, huwa zina maudhi kwa mtumiaji.

Maudhi hayo yanaweza kujitokeza pindi dawa inapotumika au baada ya kumaliza dozi. Maudhi yote hayo hutatuliwa kwa kufuata ushauri na maelekezo ambayo huenda sambamba na aina ya dawa zilizotolewa kwa mgonjwa.

Moja ya maudhi ambayo yamekuwa yakijitokeza kwa watu ni kuvurugika kwa mfumo wa uyeyushaji/mmeng’enyo wa chakula tumboni, ambapo mtu anaweza kuharisha mara baada ya kumaliza dawa hasa zile za jamii ya viuavijisumu (Antibiotics).

Dawa jamii ya antibiotics hutumika katika kutibu magonjwa mbalimbali na hasa yale yanayosababishwa na vimelea vya magonjwa ambao ni bakteria. Dawa hizi huwa na uwezo tofauti katika kuua hawa vimelea wasababishao maradhi, lakini pia ni vyema kufahamu kwamba katika mwili wa binadamu wapo viumbe wengine (normal flora) – kwa lugha rahisi huitwa bacteria, ambao uwapo wao mwilini husababisha mwili ufanye kazi yake vizuri inavyopaswa.

Zinapotumika wakati mwingine huweza kuathiri uwapo wa hawa bakteria wasiokuwa waharibifu na matokeo yake kusababisha baadhi ya vitu mwilini kushindwa kufanya kazi vizuri, mfano ni mtu kuanza kuharisha pale anapomaliza matumizi au dozi.

Ili kuepuka maudhi kama hayo, inafaa kutumia vyakula ambavyo vitasaidia kurejesha mfumo wa mwili ukae vizuri pamoja na uwapo wa bakteria au viumbe wanaosaidia mwili ufanye kazi vizuri. Mfano wa vyakula vinavyoshauriwa kutumika mara baada ya kumaliza dozi ya dawa ni matumizi ya vyakula vinavyosindikwa (Fermented foods) au kwa kutumia jamii ya bakteria katika uandaaji mfano, maziwa mtindi pamoja na jibini.

Matumizi ya dawa yatalazimika ili kuimarisha afya ya mgonjwa, lakini maudhi yanayoweza kujitokeza hutatuliwa kwa kufuata ushauri sahihi kutoka kwa wataalamu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
202,654FollowersFollow
554,000SubscribersSubscribe

Latest Articles