29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 27, 2024

Contact us: [email protected]

CANNAVARO MWEUSI SOMO KWA WANASOKA TANZANIA

 Na SOSTHENES NYONI- DAR ES SALAAM              |        


MIAKA 12 ya Nadir Haroub katika klabu ya Yanga na Ligi Kuu ya soka Tanzania Bara imefikia tamati.

Beki huyu wa kati ameachana rasmi na soka kama mchezaji na tayari klabu ya Yanga imemtangaza kuwa meneja mpya wa timu hiyo, akichukua jukumu la Hafidh Salehe, atakayepangiwa majukumu mengine.

Mashabiki wengi wa soka wangependelea kuendelea kumuona Cannavaro uwanjani, lakini umri nao umeonekana kuwa kikwazo, hatua iliyomlazimisha kuondoka kwenye soka la ushindani.

Safari yake Yanga

Cannavaro alijiunga na Yanga mwaka 2006, akitokea klabu ya Malindi ya visiwani Zanzibar.

Baada ya kutua Yanga, Cannavaro hakuwa mchezaji aliyekubalika sana miongoni mwa mashabiki wa soka.

Staili yake ya uchezaji wa kutumia nguvu kupita kiasi ilionekana kutowafurahisha mashabiki wengi, hatua iliyomfanya akosolewe kwamba hatumii akilini katika kuwadhibiti washambuliaji wa timu pinzani.

Cannavaro alitambua hilo, hivyo akaanza kubadilika taratibu na kuanza kucheza soka la mchanganyiko wa matumizi ya akili na nguvu.

Hatua hii ilimfanya aanze kupendwa na mashabiki wa soka wa klabu yake ya Yanga.

Kwa wakati huo aliweza kuunda ukuta imara katika kikosi cha Yanga, akishirikiana na Salum Sued, wawili hao walikuwa wanacheza nafasi ya beki ya kati, yaani namba nne na namba tano.

Ni katika kipindi hicho alipachikwa jina la Cannavaro, akifananishwa na beki kisiki wa zamani wa Juventus na timu ya Taifa ya Italia ambaye katika fainali za Kombe la Dunia za mwaka 2006 zilizofanyika Ujerumani alichaguliwa kuwa mchezaji bora, huku taifa lake likitwaa ubingwa.

Wakati wote huo, Cannavaro alikuwa mtiifu ndani na nje ya uwanja, akionyesha nidhamu ya hali ya juu.

Hili lilimfanya azidi kupendwa na kuaminika kuanzia kwa mashabiki, viongozi na wachezaji wenzake.

Maximo amjumuisha Taifa Stars

Kutokana na mwenendo wake bora ndani na nje ya uwanja, baada ya kukabidhiwa jukumu la kuifundisha timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ mwaka 2007, kocha raia wa Brazil, Marcio Maximo, hakusita kumjumuisha katika kikosi chake kila alipokitangaza.

Licha ya kuitwa katika kikosi hicho, Cannavaro hakuwa na nafasi ya uhakika ya uchezaji, kwani wakati huo Taifa Stars ilikuwa na mabeki visiki, Victor Costa na Salum Sued, ambao walikuwa wakisimama kama mabeki wa kati.

Hili halikumkatisha tamaa Cannavaro, badala yake aliendelea kupambana, huku akiwa mtiifu.

Baada ya Costa kupata majeraha yaliyomfanya kuwa nje ya uwanja kwa muda mrefu, ndipo Cannavaro alipoanza kupata nafasi ya kucheza michezo mingi, akiichezea Taifa Stars.

Mchango wake uliiwezesha Taifa Stars kufuzu michuano ya kwanza ya fainali za Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wanaochezaji ligi za ndani ‘CHAN’, zilizofanyika mwaka 2008 nchini Ivory Coast na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC).

Maximo aliendelea kumwamini na kumjumuisha kila alipotangaza kikosi chake mpaka pale alipokabidhi jukumu  la kuinoa timu hiyo kwa raia wa Denmark, Jan Poulsen, hiyo ilikuwa mwaka 2009.

Hata baada ya Poulsen kufungashiwa virago na msaidizi wake, Kim Poulsen kukabidhiwa jukumu hilo, Cannavaro aliendelea kuitwa katika kikosi cha Taifa Stars.

Kuanzia mwaka 2007 hadi mwaka 2012, pia amekuwa akiitumikia timu ya Zanzibar ‘Zanzibar Heroes’.

Mafanikio Yanga

Akiwa mchezaji wa Yanga, ambayo ni klabu pekee aliyoichezea katika Ligi Kuu Tanzania Bara, Cannavaro amefanikiwa kutwaa mataji lukuki.

Lakini rekodi kubwa aliyoiweka ni kutwaa mataji matatu mfululizo ya Ligi Kuu, akiwa na kocha Mdachi Hans van der Pluijm, msimu wa 2014-15, 2015-16 na 2016-17.

Jambo la kujifunza

Limekuwa jambo gumu kwa wachezaji wa Tanzania kucheza soka kwa zaidi ya miaka 10, tena kwa kiwango cha juu na hasa katika klabu zenye presha kubwa kama Yanga na Simba.

Hiyo ni kutokana na wengi wao kushindwa kuishi maisha yanayoweza kuwafanya kulinda viwango vyao,  badala yake kuangukia kwenye starehe ambazo mwisho wa siku zinawamaliza.

Lakini pia nidhamu duni ndani na nje ya uwanja imekuwa kikwazo kingine kwa wachezaji wengi wa Tanzania.

Mara kadhaa imewahi kutokea mchezaji ametunishiana msuli na kocha wake au kiongozi wa klabu anayoichezea.

WASIFU

JINA KAMILI Nadir Haroub Ali ‘Cannavaro’
Tarehe ya kuzaliwa Februari 10,1982
Mahali Michenzani, Tanzania
Urefu Inchi tano
Nafasi Beki
- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles