23.3 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

KOREA KASKAZINI YADAIWA KUENDELEZA MRADI WA SILAHA ZA NYUKLIA

KOREA Kaskazini


RIPOTI mpya ya siri ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa imefichua kuwa, Korea Kaskazini haijaachana na mradi wake wa kutengeneza silaha za nyuklia pamoja na makombora ya kivita, hivyo kukiuka vikwazo vilivyowekwa na Umoja huo kama njia ya kupatikana mwafaka.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo iliyowasilishwa juzi kwenye Baraza hilo mjini New York, nchini Marekani, imedai kuwa Serikali ya Korea Kaskazini imeongeza kiwango cha utengenezaji wa silaha za nyuklia, kusafirisha mafuta na kuuza silaha nje ya nchi.

Kwa upande wao, Serikali ya Korea Kaskazini haijasema lolote kuhusiana na ripoti iliyowasilishwa kwenye Baraza hilo, kwa madai hakuna taarifa rasmi iliyowasilishwa kwao.

Wiki iliyopita, maofisa wa Serikali ya Marekani walisema Korea Kaskazini inaendelea na mpango wa kujenga mitambo mipya ya makombora ya kivita, licha ya hivi karibuni kupewa onyo na Rais Donald Trump wa Marekani kuachana na mipango hiyo haraka.

Taarifa zinasema kuwa, baadhi ya maofisa wa Serikali ya Marekani ambao hawakuwa tayari kutajwa majina yao wamefichua kuonekana kwa setelaiti ya Korea Kaskazini ikiendelea na shughuli zake za uchunguzi na mawasiliano ya kituo cha urushaji wa makombora.

Mnamo Juni mwaka huu, Rais Trump alikutana na kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong-un nchini Singapore, ambako viongozi wote wawili walikubaliana kusitisha utengenezaji wa nyuklia, lakini hawakueleza kwa undani mbinu zitakazotumika kuhitimisha hilo.

Aidha, Korea Kaskazini imewekewa vikwazo na Jumuiya ya Kimataifa na Marekani kutokana na hatua yake ya utengenezaji wa silaha za nyuklia pamoja na majaribio ya makombora ya kivita.

Nyaraka za ripoti hiyo zimetayarishwa na timu ya wasimamizi wa utekelezaji wa vikwazo vya Umoja wa Mataifa dhidi ya Korea Kaskazini. Imetolewa jana kwa baadhi ya vyombo vya habari.

“Korea Kaskazini haijasitisha mradi wake wa nyuklia na uzalishaji wa makombora ya kivita, imepuuza maazimio ya Baraza la Usalama, imeongeza kiwango cha usafirishaji wa mafuta ya petroli kwa njia ya meli pamoja na makaa ya mawe kwa kipindi cha mwaka huu.”

Imeongeza kwa kusema: “Imejaribu kuuza silaha ndogo ndogo na vifaa vingine vya kijeshi kwenda nje ya nchi kupitia mataifa mbalimbali ili kupeleka Libya, Yemen na Sudan.”

Wachunguzi wa Baraza hilo wamesema vitendo vinavyofanywa na Korea Kaskazini vinastahili kuwekewa vikwazo vya kifedha haraka iwezekanavyo.

Aidha, ripoti hiyo imewasilishwa ikiwa ni siku chache baada ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Mike Pompeo, kusema Marekani ina matumaini makubwa kwamba mpango wa kuteketeza silaha za nyuklia za Korea Kaskazini utafanikiwa.

Akizungumza kabla ya kuanza mkutano wa Jumuiya ya Mataifa ya Kusini-Mashariki mwa bara la Asia (Asean) unaofanyika nchini Singapore, amesema: “Kazi imeshaanza. Mchakato wa kufanikisha uteketezwaji wa silaha za nyuklia katika rasi ya Korea ni mojawapo ya mambo ninayofikiri yatachukua muda kufanikisha. Lilikuwa jambo muhimu kulinda shinikizo la kidiplomasia na kiuchumi, kabla ya kukamilisha kuteketeza silaha hizo”.

Pompeo amesema ameona ripoti ya Urusi inayoruhusu Korea Kaskazini kutumia mipaka yake na kupuuza vikwazo vya Baraza la Usalama.

“Napenda kuzikumbusha nchi zote zinazounga mkono azimio hili kwamba ni jambo nyeti mno na tutalizungumza pamoja na Serikali ya Urusi. Tunategemea Urusi na nchi nyingine zitaunga mkono azimio la Baraza la Usalama na kuchochea vikwazo dhidi ya Korea Kaskazini,” alisema Pompeo.

Kwa upande wa Serikali ya Urusi, imekanusha taarifa za kuiruhusu Korea Kaskazini kutumia mipaka yake pamoja na kuchukua wafanyakazi kutoka Pyongyang.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles