|Mohamed Hamad, Manyara
Mkuu wa Wilaya ya Mbulu, Chelestino Mofuga leo amesimamia shughuli ya kuteketezwa kwa moto kwa nyumba sita wilayani humo kwa kukaidi agizo la serikali la kuondoka ndani ya siku saba katika maeneo ya hifadhi.
Miongoni mwa nyumba zilizoteketezwa kwa moto ni pamoja na ya Diwani wa Kata ya Eshkesh, Rumay Ologa ambaye baada ya kupata taarifa hizo alijisalimisha Kituo cha Polisi cha Hydom.
Akizungumza wakati shughuli hiyo ikiendelea, Mofuga amesema njia hiyo itasaidia kulinda hifadhi hiyo.
“Nawataka wavamizi wote wa maeneo ya hifadhi yetu iliyopo Mbulu kuhama kwa hiari yao ndani ya siku saba, kwani taarifa wanazo wanakaidi,” amesema.
Pamoja na mambo mengine, Mofuga amesema operesheni ya kuwaondoa wavamizi hao kwa kushirikiana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya na Jeshi la Polisi, watu hao baada ya kuchomewa nyumba zao watachukuliwa hatua za kisheria ikiwamo kuwapeleka mahakamani.