Anna Potinus, Dar es Salaam
Tanzania imesaini mkataba wa ujenzi wa daraja jipya la Salender jijini Dar es Salaam.
Mkataba huo umesainiwa leo Jumatatu Julai 23, na Rais John Magufuli na Waziri Mkuu wa Korea Kusini Lee Nak-yeon, Ikulu jijini Dar es Salaam.
Akizungumza mara baada ya kusaini mkataba huo, Rais Magufuli amesema daraja hilo litaunganisha eneo la Aga Khan katika Barabara ya Barack Obama na eneo la Ufukwe Coco Beach katika makutano ya Barabara za Kenyatta na Toure Drive.
“Mradi huu una lengo la kupunguza msongamano wa magari barabarani lakini pia kukuza uchumi wa nchi na utatumia muda wa miezi 36 (miaka mitatu) hadi kukamilika.
“Ni mategemeo yangu pamoja na kuwa mkataba ni miezi 36 ninaomba ikiwezekana hata ndani ya miaka miwili Waziri Mkuu aweze kutukabidhi daraja letu na watanzania waweze kunufaika,” amesema Magufuli.
Pamoja na mambo mengine, Rais Magufuli pia pia amesema daraja hilo la kisasa litakapokamilika litakuwa nembo ya mahusiano mazuri kati ya Tanzania na Korea.