Na BENJAMIN MASESE – MWANZA
HALI ya sitofahamu na mvutano mkali imeibuka kati ya Halmashauri ya Jiji la Mwanza na Wakala wa Barabara za Vijiji na Mijini Tanzania (Tarura), baada ya kuonekana kunyang’anyana majukumu na vyanzo vya mapato, huku wakurugenzi na meya wakitishia kusimamisha baadhi ya shughuli.
Mvutano huo uliibuka jana, katika kikao maalumu kilichoitishwa na Tarura Mkoa wa Mwanza kwa ajili ya kutambulisha majukumu yao sambamba na uzinduzi wa mfumo wa kielekitroniki wa ukusanyaji wa kodi ya maegesho ya vyombo vya usafiri na shughuli nyingine zinazofanywa kwenye hifadhi za barabara.
Viongozi waliohudhuria uzinduzi huo ni wakurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Ilemela, wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama, ambapo kila mmoja alionyesha hisia zake juu ya mfumo uliozinduliwa kwa kudai utasababisha migogoro kama tahadhari hazitachukuliwa.
Awali akitambulisha majukumu na uzinduzi wa mfumo huo, Mratibu wa Tarura Mkoa wa Mwanza, Kayoya Fuko, alisema majukumu mahususi ya taasisi hiyo mpya ni kujenga barabara, kukarabati na kuimarisha miundombinu ya wilaya na miji.
Pia aliyataja mengine ni kukusanya tozo za maegesho ya vyombo vya moto katika miji na wilaya, huku akisisitiza kuwa, taasisi nyingine ambazo zinafanya shughuli zake kwenye hifadhi za barabara kama Tanesco, TTCL, Cable, bodaboda na wengine watatakiwa kuilipa Tarura.
Alisema mfumo uliozinduliwa jana ni wa majaribio ya miezi minne, wakati wakiendelea kutatua changamoto zitakazojitokeza na baadaye utakuwa wa kitaifa.
“Tumeingia makubaliano na Kampuni ya NPK Technologies Ltd, ambayo inashirikiana na watu kutoka Uholanzi, ambapo kamera zitafungwa mitaa yote, pia kutakuwa na pikipiki za umeme zitakazokuwa zinatembea mitaa yote kukusanya taarifa zote na kuzituma moja kwa moja chumba maalumu.
“Kwa hiyo suala la maegesho ya vyombo vya usafiri litakuwa chini ya Tarura na kila dereva wa gari binafsi atakuwa analipia maegesho akiwa nyumbani na kuachiwa eneo lake, pesa zote za malipo zitakuwa zinakwenda kwenye Mfuko wa Barabara, ambapo sisi Tarura tutakuwa tunazipata huko.
“Shughuli ya tozo za mabango zinafanywa na Serikali Kuu, yaani hayo ni majukumu ya TRA, tunataka kubadilisha mfumo wa kukusanya mapato ya Serikali, tumefanya utafiti awa awali tumebaini hivi sasa Jiji la Mwanza linakusanya Sh milioni 500 hadi 600 kwa mwaka ya maegesho, lakini sisi kwa mfumo huu mpya tunaweza kukusanya Sh bilioni 2.5 kwa mwaka,” alisema.
Baada ya Tarura kuwasilisha hayo, Mwenyekiti wa kikao hicho, ambaye ni Ofisa Usalama wa Taifa Mkoa wa Mwanza (RSO), Everist Mkude, aliruhusu mjadala ama maoni juu ya kile kilichowasilishwa ambapo Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ilemela, John Wanga, alihoji sababu ya Tarura kuchukua majukumu ya halmashauri kama ukusanyaji wa ushuru wa maegesho na usafi, ikiwa ni sehemu ya vyanzo vyake vya mapato.
Kutokana na hilo, alitishia kuwasimamisha watu wanaofanya usafi katika eneo lake la uongozi.
Wakati Wanga akiendelea kuhoji na kuwataka Tarura kukaa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) ili wabomoe baadhi ya majengo yao katikati ya jiji la Mwanza na kutengeneza maegesho, naye Naibu Meya wa Jiji la Mwanza, Bhiku Kotecha, alisimama na kutaka maeneo ambayo yanamilikiwa na jiji yasiguswe na Tarura na kuwataka kujishughulisha na barabara tu.
Mvutano huo uliendelea kupamba moto baada ya Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Mwanza, Ernest Makale, kuhoji mfumo huo kufuatilia taarifa za gari binafsi ambazo zinapaswa kulipa tozo ya maegesho ilhali zipo baadhi ya taasisi za Serikali zinazotumia gari binafsi.
Pia askari wa JWTZ na Zimamoto nao walihoji ikiwa umeme utakosekana kwa siku nzima ama mitandao ya simu za mikononi ikisumbua wakati mwenye gari anataka kulipa, na zaidi atakavyosaidiwa mgeni atakayeingia Mwanza ambaye hajui mfumo unavyotumika, licha ya taarifa kwamba kutakuwepo na ofisi chache za kulipia ana kwa ana katika maeneo maalumu.
Kutokana na hoja hizo, RSO Mkude alilazimika kuahirisha kikao hicho na kuwataka Tarura kuendelea kukaa na taasisi hizo kwa miezi minne ili kuelimishana na kuweka mambo sawa.
Alisema hakuna haja ya taasisi za Serikali kugombana wakati wanajenga nyumba moja kwa lengo la kuleta maendeleo kwa wananchi na kuongeza mapato.