23.9 C
Dar es Salaam
Monday, October 2, 2023

Contact us: [email protected]

AKINA MBOWE WAKWAMA MAHAKAMA KUU

Na PATRICIA KIMELEMETA


MAHAKAMA Kuu  ya Tanzania imetupilia mbali maombi yaliyowasilishwa na viongozi tisa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ya  kupitia, kuitisha na  kuchunguza kumbukumbu za mwenendo wa kesi namba 112, iliyofunguliwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, ili kujiridhisha na usahihi na uhalali wa amri zilizotolewa.

Shauri hilo lilisikilizwa na Jaji Rehema Sameji, huku upande wa waleta maombi (Chadema) ukiwakilishwa na mawakili Peter Kibatala, huku upande wa wajibu maombi (serikali) ukisimamiwa na mawakili, Paul Kadushi, Faraja Nchimbi na Wankyo Simon.

Viongozi waliofungua shauri hilo ni Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, Katibu Mkuu, Dk. Vincent Mashinji na Manaibu wake, John Mnyika (Bara) na Salum Mwalimu (Zanzibar).

Wengine ni Mchungaji Peter Msigwa, ambaye ni Mbunge wa Iringa Mjini, Esther Matiko (Mweka Hazina wa Bawacha), Halima Mdee (Mbunge, Kawe), John Heche (Mbunge, Tarime Vijijini) na Ester Bulaya (Mbunge, Bunda).

Akisoma uamuzi huo mahakamani hapo jana, Jaji Sameji alisema, amepitia hoja zilizowasilishwa na waleta maombi (Chadema) na kubaini kuwa, kifungu namba 372 kilichowasilishwa mahakamani hapo kina utata, hali iliyosababisha mahakama kujikuta kwenye wakati mgumu.

Alisema kwa kuwa shauri la msingi bado linaendelea Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kwamba sheria inakataza maombi madogo kuombewa marejeo kwenye mahakama hiyo, jambo hilo limewafanya wasiwe na mamlaka ya kusikiliza maombi hayo.

Alisema kutokana na hali hiyo, ameamua kutupilia mbali maombi hayo na kuwataka waleta maombi (Chadema) kufungua rufaa ikiwa hawajaridhika na uamuzi huo.

“Mahakama imeamua kutupilia mbali maombi yaliyowasilishwa na viongozi wa Chadema, wakiiomba Mahakama Kuu kupitia, kuitisha na kuchunguza kumbukumbu za mwenendo wa kesi namba 112, iliyofunguliwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kwa sababu haina mamlaka ya kisheria kufanya hivyo wakati shauri bado linaendelea Mahakama ya Kisutu,” alisema Jaji Sameji.

Hata hivyo, mawakili wa waleta maombi (Chadema) tayari wamewasilisha notisi ya kukata rufaa Mahakama ya Rufaa, wakipinga uamuzi huo.

Katika shauri hilo, viongozi wa Chadema, walifungua maombi Mahakama Kuu ya kuiomba mahakama hiyo kupitia mwenendo wa kesi ya jinai inayowakabili viongozi hao, iliyopo Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Katika kesi ya msingi namba 112 ya mwaka 2018, viongozi hao walisomewa mashtaka 13, yakiwamo kufanya mikusanyiko, vurugu na maandamano yasiyo halali na kusababisha kifo cha aliyekuwa Mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwilini.

Viongozi hao wanadaiwa kutenda makosa hayo Februari 16, mwaka huu, katika Barabara ya Kawawa, eneo la Kinondoni Mkwajuni.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,770FollowersFollow
575,000SubscribersSubscribe

Latest Articles