27.2 C
Dar es Salaam
Friday, November 29, 2024

Contact us: [email protected]

WEMA AONJA MAHABUSU KWA DAKIKA 45

PATRICIA KIMELEMETA na JOHANNES RESPICHIUS


MSANII wa filamu nchini, Wema Sepetu, amekaa mahabusu kwa takribani dakika 45, baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kumtia hatiani kwa kosa la kutumia bangi na kuhukumiwa kwenda jela kwa mwaka mmoja au kulipa faini ya Sh milioni mbili.

Wema, ambaye alikuwa Miss Tanzania mwaka 2006, jana alikaa kwenye mahabusu ya mahakama hiyo wakati akisubiri taratibu za kulipwa kwa faini aliyotozwa.

Baada ya ndugu zake kulipa faini, msaani huyo alitoka mahabusu saa 7 mchana na kuondoka kwenye viwanja vya mahakama hiyo.

Awali akisoma hukumu hiyo, Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba, aliwaachia huru washtakiwa wengine wawili waliokuwa wanashtakiwa pamoja na Wema.

Washtakiwa hao, ambao ni wafanyakazi wake, ni Matilda Abass na Angelina Msigwa.

Hakimu Simba akisoma hukumu hiyo, iliyochukua takribani dakika 40, alisema upande wa mashtaka ulikuwa na mashahidi watano, huku upande wa washtakiwa katika kesi hiyo walijitetea wenyewe.

Alisema baada ya kusikiliza ushahidi uliotolewa pande zote mbili, mahakama hiyo imejiridhisha pasi na shaka kuwa mshtakiwa wa kwanza kwenye kesi hiyo, Wema Sepetu, anatumia dawa za kulevya aina ya bangi.

Alisema, awali wakati anasikiliza ushahidi wa mashahidi watano wa upande wa mashtaka, mashahidi hao walitoa vielelezo vya kuonyesha kuwa, Wema anatumia dawa hizo.

Alisema shahidi wa kwanza katika kesi hiyo, ambaye ni Mkemia kutoka Ofisi ya Mkemia Mkuu, Elias Mulima, alisema alipokea sampuli za vielelezo viwili, kimoja cha misokoto inayodhaniwa ni ya bangi na kingine ni mkojo uliohifadhiwa kwenye kikontena.

Alisema misokoto hiyo inadaiwa kukutwa nyumbani kwa Wema, baada ya kufanyiwa uchunguzi na askari polisi kutoka Kituo Kikuu cha Polisi (Central).

Alisema mkemia huyo baada ya kupewa vielelezo hivyo, alivifanyia vipimo kwa wakati tofauti, ambapo kilichodhaniwa kuwa ni bangi alikichanganya na dawa maalumu ambayo ilionyesha kuwa kweli ni bangi na baadaye kufanya kipimo cha pili kupitia mitambo maalumu na majibu yalikuwa hivyo hivyo.

Alisema shahidi huyo alipokea sampuli nyingine ya mkojo wa Wema, ambaye alipelekwa ofisini kwake akiwa chini ya ulinzi wa Inspekta Willy na askari mwanamke, aliyefahamika kwa jina moja la Marry.

Alisema mara baada ya kumfanyia vipimo, majibu yalionyesha kuwa na chembechembe za dawa za kulevya aina ya bangi ambazo zilikaa kwenye mkojo huo kwa siku 28.

Alisema shahidi wa pili, Inspekta Willy, aliieleza mahakama hiyo kuwa, waliongozana na WP Mary kupeleka vielelezo hivyo kwa Mkemia ili viweze kufanyiwa uchunguzi wa kimaabara.

Alisema, shahidi wa tatu, WP Mary, aliieleza mahakama hiyo kuwa, siku ya tukio aliambiwa aongozane na Wema kwenda nyumbani kwake, Ununio, kwa ajili ya kufanya upekuzi.

Alisema tukio hilo lilitokea baada ya Wema kutajwa kwenye orodha ya watu wanaodaiwa kutumia dawa za kulevya na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda na aliyekuwa Kamanda wa Kikosi cha Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro, ambaye kwa sasa ni Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP).

Alisema wakiwa njiani, alimuuliza mtuhumiwa (Wema) kama anatuma dawa za kulevya,  mtuhumiwa huyo alikiri na kudai kuwa, anatumia kama starehe.

Alisema shahidi wa nne katika kesi hiyo, Mjumbe wa nyumba 10, Stephen Ndonde, alidai mahakamani hapo kuwa, siku ya tukio aliitwa kushuhudia upekuzi nyumbani kwa Wema.

Alisema, shahidi huyo aliieleza mahakama kuwa wakati upekuzi unaendelea, walikuta kipisi cha msokoto katika chumba cha kuvaa nguo cha msanii huyo na chumba cha mfanyakazi wake walikuta kipisi kingine.

Hakimu Simba alisema shahidi wa tano, Koplo wa Polisi, Robert, aliieleza mahakama kuwa, alipokea maagizo kutoka kwa bosi wake ya kupeleka vielelezo kwa Mkemia Mkuu wa Serikali, ikiwamo msokoto mmoja na vipisi viwili vya dawa za kulevya idhaniwayo kuwa bangi.

Alisema walitoa ushahidi wao mahakamani hapo, ambako Wema alikana kutumia dawa za kulevya aina ya bangi na alisema hakuna mtu anayeweza kuingia chumbani kwake.

Pia alisema wakati wa upekuzi, polisi walikuta msokoto wa bangi.

Hakimu Simba alisema wakati polisi wanafika nyumbani kwa Wema kufanya upekuzi huo, wafanyakazi wake, Matilda na Angelina, walikuwa wameketi barazani.

Mara baada ya kusema hayo, mahakama hiyo ilimtia hatiani Wema kwa mashtaka ya kukutwa na kutumia dawa za kulevya aina ya bangi na kuwaachia huru wafanyakazi wake, Matilda na Angelina.

Upande wa mashtaka ukiwakilishwa na Wakili Constantine Kikula, aliiomba mahakama hiyo kutoa adhabu kali kwa mshtakiwa wa kwanza, Wema, ili iwe fundisho kwa wengine kwa sababu ni msanii na kioo cha jamii, lakini alikuwa anaweza kutumia dawa za kulevya, jambo ambalo linaweza kusababisha kuwashawishi wasanii wengine kufanya hivyo.

Wakili wa Utetezi, Albert Msando, aliiomba mahakama kumpunguzia adhabu mshtakiwa kwa sababu ni kosa la kwanza, hivyo anaweza kubadilika na kuwashawishi wananchi wasiweze kutumia dawa hizo.

Mara baada ya kujitokeza kwa malumbano hayo ya kisheria, Hakimu Simba alimhukumu Wema kwenda jela mwaka mmoja au kulipa faini ya Sh milioni mbili, kila kosa anatakiwa kutoa faini ya Sh milioni moja.

Alitoa onyo kali kwa msanii huyo kujirekebisha na kuacha kabisa kutumia dawa hizo pamoja na kutoa elimu kwa wananchi juu ya madhara yatokanayo na matumizi ya dawa za kulevya.

Hata hivyo, msanii hiyo alikidhi masharti ya hukumu hiyo na kuachiwa huru.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles