25.9 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 27, 2024

Contact us: [email protected]

MAJALIWA AKEMEA WATUMISHI WASIOWAJIBIKA

Na IREN BWIRE (OWM),MWANZA


WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amekemea tabia ya kutowajibika miongoni mwa watumishi kwa kisingizio cha mgawanyo wa madaraka.

Waziri mkuu alitoa onyo hilo juzi wakati akizungumza na wanaushirika na mamia ya wakazi wa Jiji la Mwanza waliohudhuria maadhimisho ya Siku ya Ushirika Duniani yaliyofanyika kwenye viwanja vya Furahisha, jijini hapa

Alisema kuna maafisa ushirika ambao hawataki kuwajibika kwa sababu wameajiriwa TAMISEMI na wengine wako chini ya Tume ya Maendeleo ya Ushirika.

“Ofisa Ushirika wa Wilaya yuko mkoani ambako ni chini ya TAMISEMI, Mrajis Msaidizi wa mkoa yuko wizarani. Serikali ni moja, kwa hiyo wote bado mnawajibika kwa Mrajis Msaidizi wa Mkoa,” alisema.

Aidha Majaliwa aliwataka wakurugenzi wa halmashauri nchini wasiwapangie kazi nyingine zilizo nje na taaluma yao maofisa ushirika wa wilaya na wahakikishe wanatoa taarifa kwenye vikao vya halmashauri zao.

“Msimpe kazi ya kufundisha Ofisa Ushirika kwa sababu hakuna mtu mwingine. Ofisa Ushirika aachwe afanye kazi ya ushirika na atoe taarifa kwenye vikao vyenu. Madiwani mnapokutana kwenye baraza, mpeni nafasi Ofisa Ushirika aeleze maendeleo ya ushirika yakoje katika wilaya yenu,”alisema.

Changamoto nyingine zinazoikabili sekta ya ushirika aliitaja kuwa ni wizi na ubadhirifu miongoni mwa watendaji wa vyama vya ushirika waliopewa dhamana ya kuvisimamia na kuviendesha vyama hivyo.

Aliitaja changamoto nyingine kuwa ni ukosefu wa elimu ya kutosha ya ushirika miongoni mwa wanachama, viongozi na watendaji wa vyama vya ushirika, kuporomoka kwa imani ya ushirika miongoni mwa jamii na kwa baadhi ya wanachama kutokana na vyama vya ushirika kushindwa kukidhi mahitaji ya wanachama wake.

Nyingine ni uwepo wa madeni makubwa katika baadhi ya vyama vya ushirika nchini na baadhi ya viongozi wa kisiasa na wafanyabiashara kuwa na mtazamo hasi kwenye ushirika kwa malengo ya upotoshaji kwa maslahi yao binafsi.

Wakati huo huo Waziri Mkuu Majaliwa aliwataka viongozi wa vyama vya msingi (AMCOS) waajiri mameneja wenye sifa ili kuepuka ubadhirifu ndani ya vyama hivyo.

 

Alisema watumishi ambao wamepata nafasi za juu katika AMCOS ni lazima wawe na elimu ya ushirika kutoka Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU).

“Utumishi katika hivi vyama mara nyingi unaenda na uaminifu. Kama chama kikiona kina mtu wanayemwamini, ni lazima kimpeleke chuoni ili apate sifa stahiki,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles