Na Willbroad Mathias
MFUMO rafiki wa sheria za makosa ya jinai ni kati ya haki za watoto ulioainishwa katika vifungu vya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mfumo rafiki ni maboresho yaliyofanyika katika miaka ya karibuni kwa kufuta Sheria ya zamani ya Watoto na Vijana ya mwaka1937 na kutungwa kwa Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009 ambayo pamoja na mambo mengine ilianzisha Mahakama ya Watoto.
Kuanzishwa kwa mfumo huu rafiki wa sheria za kijinai kwa watoto ni kipimo sahihi cha namna Serikali inavyoweza kutekeleza matakwa mbalimbali ya mikataba ya kimataifa na sheria na sera za watoto.
Mbali na lengo hilo mfumo huu ulikuwa na lengo la kuondoa ukatili kwa watoto na kujenga mfumo mbadala ambapo haki zao zitazingatiwa na pia watalindwa dhidi ya ukatili wakati wote.
Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (TAWLA) kinasema pamoja na kuwapo na nia njema ya Serikali kupambana na hali hiyo, bado kuna upungufu.
TAWLA inasema licha ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania kutoa haki za kijumla kuhusiana na masuala ya makosa ya jinai kama haki ya kutokuonekana mhalifu mpaka uhukumiwe, haki ya dhamana, haki ya kupata msaada stahiki wa kisheria na haki ya kusikilizwa na kutoa maoni, bado kuna pengo linalohitaji kujazwa hasa kuhusiana na haki za watoto wenye kukinzana na sheria.
Inasema katika eneo hilo, yapo masuala maalumu kuhusiana na watoto wanaoingia katika kukinzana na sheria ambayo si rahisi kuyashughulikia katika mfumo wa jinai uliopo katika Katiba ya sasa ambao unatazama na kushughulikia zaidi haki za watu wazima.
Wataalamu hao wanasema, baadhi ya masuala hayo maalumu ni pamoja na kutazama masilahi mapana ya watoto na ulinzi wao, hivyo Katiba kama sheria mama ni lazima itambue vigezo hivi muhimu wakati wa kutunga ibara zinazomgusa mtoto.
TAWLA inasema kwa kufanya hivyo, Tanzania itakuwa inaingiza katika Katiba kanuni muhimu zinazohusu watoto kama zinavyotambuliwa na mikataba ya kimataifa kuhusu watoto.
“Vilevile ni vizuri kufahamu kuwa madhumuni ya kuwa na mfumo rafiki wa jinai kwa watoto ni kuwarekebisha watoto waliohukumiwa kwa jinai na kuwafanya wawe raia wema. Hivyo kuna tofauti kubwa sana na mfumo wa kawaida wa jinai unaolenga kumfanya mtu atubu, asifanye uhalifu tena na usiolenga katika kumrekebisha mtuhumiwa na kumbadili awe raia bora,” inasema moja ya taarifa za utafiti wake wa hivi karibuni.
Chama hicho cha wanasheria kinasema, ni vizuri pia kutambua kuwa vipo viwango vya kimataifa kuhusu mfumo rafiki wa jinai kwa watoto unaotokana na mikataba mbalimbali.
TAWLA inasema, viwango hivi vinaelekea sasa kuwa sheria za asili za kimataifa na kwa kutambua hili nchi nyingi duniani zimeanza kuvizingatia kama viwango ambavyo ni lazima nchi na taasisi mbalimbali katika nchi hiyo ivifikie wakati wa kutunga sheria na taratibu za kuongoza mfumo rafiki wa jinai kwa watoto.
“Tunatambua pia maboresho yaliyofanyika katika siku za karibuni kwa kufuta Sheria ya zamani ya Watoto na Vijana ya mwaka1937 na kutunga Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009 ambayo pamoja na mambo mengine ilianzisha Mahakama ya Watoto. Hata hivyo, sheria hii mpya tayari imeonyesha kuwa na mapungufu yanayohitaji kufanyiwa kazi,” inasema ripoti hiyo.
Wanasheria hao wanasema, katika utafiti uliofanyika mwaka 2011 imeonekana kuwa hakuna mfumo maalum wa kuwalinda Watoto na ukatili na kudhalilishwa ikiwa ni pamoja na ukosefu wa huduma tofauti kwa wahalifu wengine.
Wanasema hali hii inahitaji matamko na nguvu za ziada kuhakikisha uwepo wa mfumo utakaohakikisha haki za watoto zinalindwa na kuzingatiwa na wakati huo bora.
TAWLA wanasema upungufu huo pia ndio umekuwa ukichangia pia kukosekana hata mazingira hayo rafiki katika Mahakama ya Watoto.
Wanasema pamoja na sheria za uanzishwaji wa mahakama hizo kueleza kuwa mambo mengi ikiwamo na mashauri ya watoto kusikilizwa kwenye majengo tofauti na zinaposikilizwa kesi za watu wazima, lakini katika tafiti zao mbalimbali wamekuwa wakikuta hali tofauti na maelekezo ya sheria hiyo.